Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-18 19:29:23    
Satellite ya hali ya hewa ya kizazi kipya ya China kuinua kwa ufanisi kiwango cha utabiri wa hali ya hewa

cri

Hivi karibuni, China ilifanikiwa kurusha satellite ya kwanza ya Fengyun No.3 ambayo ni satellite ya hali ya hewa ya kizazi kipya, satellite hiyo itatoa huduma bora ya hali ya hewa kwa China na nchi nyingine duniani.

Satellite ya kwanza ya Fengyun No. 3 ilirushwa kwa mafanikio tarehe 27 mwezi Mei kwenye kituo cha kurushia satellite cha Taiyuan, China. Kwa mujibu wa usanifu wake, satellite hiyo itazunguka dunia kwa kufuata mwelekeo wa longitudo na itamaliza mzunguko mmoja kila baada ya dakika 102 kwa kupita kwenye ncha mbili za dunia. Mkurugenzi wa kituo cha satellite za hali ya hewa cha China Bw. Yang Jun alisema, ikilinganishwa na satellite za zamani za aina hiyo, uwezo na kiwango cha kuaminika kwa satellite ya kwanza ya Fengyun No. 3 zote zimeinuka kwa kiasi kikubwa. Bw. Yang Jun alisema:

"Satellite za zamani zinachunguza kwa njia ya kupiga picha, ambazo zinaonesha hali ya sehemu ya juu tu, kwa mfano haziwezi kuonesha muundo wa ndani wa kimbunga. Hivi sasa satellite ya Fengyun No. 3 imekuwa na uwezo huo. Kwa hivyo satellite hiyo itatoa mchango katika kuboresha kiwango cha usahihi wa utabiri wa hali ya hewa nchini China."

Imefahamika kuwa China ilianza kusanifu na kutengeneza yenyewe satellite ya hali ya hewa kwenye miaka ya 70 ya karne iliyopita. Hadi sasa China imefanikiwa kurusha satellite 9 za hali ya hewa, na kuwa moja ya nchi chache duniani zenye satellite za hali ya hewa zinazopita kwenye njia ya ncha za dunia na njia ya juu ya Ikweta. Mtaalamu wa kituo hicho Bi. Dong Chaohua alisema, satellite za hali ya hewa kwenye njia hizo mbili zinaweza kuinua kwa kiasi kikubwa kiwango cha uchunguzi wa hali ya hewa. Bi. Dong Chaohua alisema:

"Satellite ya hali ya hewa inayopita juu ya ncha mbili za dunia inaweza kuchunguza hali ya hewa ya kote duniani, yaani ni kituo cha hali ya hewa kinachohamahama kwenye anga ya juu, lakini satellite inayopita kwenye njia juu ya Ikweta ni kama kituo kilichotulia kwenye anga ya juu, satellite ya aina hiyo inaweza kuchunguza robo moja au theluthi moja ya eneo la dunia."

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kituo cha satellite za hali ya hewa cha China Bw. Yang Jun, ili kuinua kiwango cha uchunguzi, satellite ya Fengyun No.3 inabeba vifaa zaidi ya 10 vyenye kiwango cha kimataifa, kwa kutumia vifaa hivyo satellite hiyo si kama tu inaweza kufanya uchunguzi kwa saa 24 kila siku kote duniani, bali pia inaweza kufanya utabiri wa hali ya hewa kwa siku 10 hadi 15 zijazo, kiwango cha usahihi wa utabiri huo pia kitainuka.

Bw. Yang Jun alisema, zamani utabiri wa hali ya hewa nchini China kwa kawaida ulikuwa unaweza kufikia muda wa wiki moja tu. Hata hivyo utabiri huo mara kwa mara ulikuwa tofauti na hali halisi. Matumizi ya satellite ya Fengyun No. 3 yatabadilisha hali hiyo. Bw. Yang Jun alisema:

"kwa mfano, zamani kiwango cha usahihi cha utabiri wa hali ya hewa kilikuwa ni siku tatu, sasa tunaweza kukifikia utabiri wa siku tano; hivi sasa utabiri wa siku zilizo karibu zaidi, kiwango cha usahihi kitakuwa juu zaidi. Katika siku za baadaye kiwango cha usahihi cha utabiri wa siku tatu kitafikia kile cha utabiri wa siku moja."

Mbali na kuinua usahihi wa utabiri wa hali ya hewa, satellite hiyo pia inaweza kuisaidia China kukabiliana kwa ufanisi na hali mbaya za hewa zilizosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, na itatoa mchango mkubwa katika kuzuia na kupunguza hasara za maafa. Bw. Yang Jun alieleza, kutokana na kuongezeka kwa halijoto duniani, hali mbaya za hewa zikiwemo tufani na dhoruba ya vumbi zitaweza kutokea mara nyingi zaidi. Kama hali hizo zikitokea, satellite hiyo itaweza kutuma mara moja data husika ili kuzisaidia idara husika kuchukua hatua mwafaka. Bw. Yang Jun alisema:

"Tunapokea data za satellite ya Fengyun No. 3 kwa kupitia vituo vinne nchini, pamoja na kituo kimoja cha satellite kilichojengwa kwa ushirikiano kati ya China na Sweden kwenye sehemu ya ncha ya kaskazini. Vituo hivyo vitatumia data hizo kwa kituo cha satellite za hali ya hewa cha China, baada ya kushughulikiwa, data hizo zitatolewa kwa idara mbalimbali husika."

Mtaalamu wa kituo hicho Bi. Dong Chaohua alisema, satellite ya Fengyun No. 3 inaweza kutumika kwa pamoja duniani. Katika siku za baadaye, watumiaji wengi wa kimataifa pia wataweza kupokea moja kwa moja na kutumia data zilizotumwa na satellite hiyo. Bi. Dong Chaohua alisema:

"Satellite ya hali ya hewa inatoa huduma za umma, inafanya uchunguzi huku ikituma duniani data ilizopata. Kwa hivyo kama una vifaa vya kupokea ishara za satellite, utaweza kupokea data zake. Kwa hiyo nasema satellite hiyo inatumika kwa pamoja duniani."

Imefahamika kuwa satellite hiyo imechukuliwa na Shirika la hali ya hewa duniani kwenye mtandao mpya wa satellite za hali ya hewa zinazopita kwenye ncha za dunia. Satellite hiyo pamoja na satellite za aina hiyo za Ulaya na Marekani zitafanya uchunguzi wa mfululizo kuhusu hali ya mazingira ya hewa, bahari na ardhi duniani.

Habari zinasema satellite ya kwanza ya Fengyun No. 3 hivi karibuni imetuma duniani picha yake ya kwanza, picha hiyo inaonekana vizuri sana. Ofisa husika wa idara kuu ya hali ya hewa ya China alisema, vifaa vilivyoko kwenye satellite hiyo vyote vitaanza kufanya kazi baada ya wiki kadhaa. Michezo ya Olimpiki ya Beijing itakayofanyika mwezi Agosti, itakuwa ni shughuli kubwa ya kwanza itakayohudumiwa na satellite hiyo. Satellite hiyo itatoa huduma sahihi zaidi ya hali ya hewa kwa ajili ya michezo hiyo.