Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-19 17:03:52    
China yaadhimisha Siku ya urithi wa utamaduni kwa shughuli mbalimbali

cri

Tarehe 14 Juni ni Siku ya urithi wa utamaduni katika mwaka wa tatu nchini China. Kila mwaka katika siku hiyo Wizara ya Utamaduni na idara za utamaduni katika ngazi zote zinafanya shughuli za kila aina ili kuwakumbusha wananchi wauthamini na kurithisha utamaduni wao wa jadi. Mwaka huu wasanii kutoka mkoa wa Sichuan uliokumbwa na maafa ya tetemeko kubwa la ardhi pia walikuja Beijing kuonesha utamaduni wao huku wakionesha moyo wao wa kupamabana na maafa. Hapa Beijing maonesho na shughuli za aina mbalimbali zaidi ya mia moja ikiwa ni pamoja na maonesho ya vitu vya kale, michezo ya sanaa na mihadhara inafanyika ili kuwafahamisha wananchi na wageni utamaduni unaong'ara wenye historia ndefu.  

"Siku ya Urithi wa Utamaduni nchini China ilianza kuadhimishwa mwaka 2006. Ili kuenzi na kuwafanya wananchi wauthamani na kurithisha utamaduni wao mkubwa, serikali ya China iliamua kuwa jumamosi ya pili ya mwezi Juni iwe Siku ya Urithi wa Utamaduni ya China. Tangu mwaka 2006 katika siku hiyo serikali katika kila ngazi inafanya shughuli za kila aina".

Siku ya Urithi wa Utamaduni wa China mwaka huu inaandaliwa tofauti na miaka mingine. Tarehe 12 Mei tetemeko kubwa la ardhi lilitokea mkoani Sichuan na kusababisha hasara kubwa za mali na watu wengi kupoteza maisha yao, na mabaki yautamaduni pia yaliharibiwa vibaya. Katika mikoa iliyoathiriwa na tetemeko hilo Sichuan, Shanxi na Gansu ilipata uharibifu mkubwa ambao haujawahi kutokea hapo kabla. Naibu mkurugenzi wa Idara ya hifadhi wa mabaki ya kale Bw. Dong Baohua alisema,

"Hadi kufikia tarehe 5 Juni tulipata ripoti kuhusu uharibifu wa utamaduni wa jadi kwenye majengo 169 ya urithi wa utamaduni wa ngazi ya taifa, na kati yao mawili yaliorodheshwa na UNESCO katika urithi wa utamaduni duniani, na majengo 250 ya urithi wa utamaduni wa ngazi ya kimkoa yaliharibiwa kwa viwango tofauti, vitu vya kale 2,766 vilivyotunzwa katika majumba ya makumbusho viliharibiwa, kati ya vitu hivyo vitu 292 ni adimu."

Pamoja na mabaki ya kale ya utamaduni, majumba manne ya ya kutunza utamaduni usioonekana yaliharibiwa vibaya. Naibu waziri wa utamaduni wa China Bw. Zhou Heping alikwenda mkoani Sichuan kukagua hali ya uharibifu wa mabaki ya kale ya utamaduni mara tu baada ya tetemeko la ardhi kutokea. Alisema wizara ya utamaduni ilitaka kufuta maonesho ya utamaduni wa jadi wa mkoa wa Sichuan, lakini wasanii wa mkoa huo uliokumbwa na maafa ya tetemeko la ardhi wanashikilia kufanya maonesho yao hapa Beijing. Alisema

"Wasanii wenyeji wa mkoa wa Sichuan walisema, katika wakati huu mgumu wanataka zaidi kuonesha utamaduni wao mkubwa usioonekana na kuonesha moyo wao wa ushupavu dhidi ya maafa. Tarehe 14 Juni jioni wasanii hao walionesha michezo yao ya jadi. Kati wasanii hao, wasanii 23 wa kabila la Waqiang waliathiriwa zaidi na maafa."

Wizara ya Utamaduni iliandaa maonesho 46 ya michezo ya sanaa. Naibu mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Sanaa ya China Bw. Zhang Qingshan alisema, maonesho katika siku za mwanzo wa siku ya urithi wa utamaduni ni ya wasanii kutoka mkoa wa Sichuan, ambayo ni sanaa ya kienyeji inayogusa sana hisia za watazamaji. Bw. Zhang Qingshan alisema,

"Maonesho ya wasanii wa mkoa wa Sichuan yanagawika katika sehemu nne, ya kwanza ni nyimbo za hodiya, ambazo zinaimbwa kwa kutia harambee wakati wa kufanya kazi ngumu. Sehemu ya pili ni nyimbo na ngoma za kabila la Waqiang, sehemu ya tatu ni sanaa za kabila la Wayi na sehemu ya nne ni sanaa ya kabila la Watibet."

Bw. Zhang Qingshan alisema kati ya wasanii wa kabila la Waqiang wanne walifiwa na jamaa zao katika tetemeko la ardhi, hata hivyo wanashikikilia kushiriki kwenye maonesho hayo. Moyo kama huo ndio sababu ya utamaduni wa jadi wa China wenye historia ndefu unaweza kurithishwa kizazi kwa kizazi.

Kuanzia tarehe 4 Juni shughuli za aina kwa aina zinafanyika katika wilaya zote mjini Beijing kwenye majumba ya makumbusho na sehemu za wakazi. Tarehe 14 ilipoanza kudhimishwa Siku ya urithi wa utamaduni ya China shughuli hizo zilipamba moto na zitaendelea hadi michezo ya Olimpiki ya Beijing itakapomalizika. Mkueugenzi wa Idara ya Utamaduni ya Beijing Bw. Xiang Gongmin alisema.

"Shughuli hizo zitaendelea toka mwezi Juni hadi Septemba, zikiwa ni pamoja na ufunguzi wa michezo ya Olimpiki, maonesho ya michezo ya sanaa na maonesho kwenye majumba ya makumbusho na mihadhara, kati ya maonesho hayo maonesho muhimu ni kuonesha vitu vya kale vya Beijing na sehemu mbalimbali nchini China."

Katika kipindi cha Siku ya Urithi wa Utamaduni wa China, Beijing itafanya "shughuli za kuupamba mji wa Beijing kwa taa za rangi kusherehekea michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008", sehemu zote za umma zitapambwa kwa taa za aina ya jadi ya China. Tokea tarehe 8 Juni hadi tarehe mosi Septemba makundi ya wasanii kutoka sehemu mbalimbali nchini China yataonesha aina zaidi ya kumi za michezo ya opera za jadi, watazamaji pia wataweza kufurahia ufundi wa sanaa za jadi za mikono. Katika jumba la makumbusho la Beijing na bustani za umma wataalamu wa vitu na utamaduni wa kale watafanya mihadhara. Hivi karibuni serikali ya China itatangaza makundi ya pili ya utamaduni usioonekana zaidi ya aina 600, kwa kufanya hivyo mfumo wa hifadhi ya urithi wa utamaduni utakamilishwa zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2008-06-19