Mkutano wa siku 5 wa wakurugenzi wa idara za hakimiliki ya ubunifu za China na nchi za Afrika umefungwa Tarehe 20 Juni hapa Beijing. Maofisa wa nchi za Afrika waliohudhuria mkutano huo wameeleza matumaini ya kuimarisha ushirikiano na China katika kazi ya kulinda hakimiliki ya ubunifu kwenye sekta ya utamaduni wa jadi, matibabu na dawa. Ofisa mhusika wa China ameahidi kuchukua hatua mbalimbali za kuhimiza ushirikiano wa kina kati ya China na Afrika kwenye sekta hiyo.
Kwenye Mkutano huo wajumbe kutoka nchi 16 za Afrika zikiwemo nchi za na Zimbabwe, Somalia na Sudan pamoja na maofisa wa China wanaoshughulikia kazi ya hakimiliki ya ubunifu walijadili masuala mengi kuhusu utungaji wa sera ya hakimiliki ya ubunifu, hataza, nembo za biashara na kazi ya kuwaandaa watu wenye ujuzi, wajumbe wa nchi za Afrika walitembelea idara kuu ya hakimiliki ya ubunifu ya China. Mkurugenzi wa idara hiyo ya China Bw. Tian Lipu alisema, mkutano huo ni ushirikiano halisi wa mara ya kwanza kati ya China na idara za hakimiliki ya ubunifu za Afrika. Alisema:
"Idadi ya watu wa China na wa nchi za Afrika kwa jumla inachukua zaidi ya theluthi moja ya ile ya jumla ya dunia nzima, kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta ya hakimiliki ya ubunifu kunasaidia pande hizo mbili zinufaike na uzoefu wa kutekeleza utaratibu wa hakimiliki ya ubunifu, na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa kila nchi, kufanya hivyo si kama tu kutaleta manufaa kwa wananchi wa China na nchi za Afrika, bali pia kutahimiza ustawi na maendeleo ya dunia".
Mkurugenzi mkuu wa Jumuiya ya hakimiliki ya ubunifu ya Afrika Bw. Gift Sibanda aliwataka wajumbe wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo waliohudhuria Mkutano huo waweze kujifunza kutoka China kuhusu hatua nyingi zaidi za kulinda hakimiliki ya ubunifu. Bw. Sibanda alisema, ameona mafanikio yaliyopatikana China katika kazi ya kulinda hakimiliki ya ubunifu. Alisema:
"China imepata maendeleo katika kazi nyingi zinazohusu hakimiliki ya ubunifu, pia imejenga maktaba kubwa ya data. Nchi za Afrika pia zinataka kujenga maktaba zao kamili za data zinazohusu sekta ya hakimiliki ya ubunifu".
Kwa kweli, China imeanzisha kazi ya kulinda hakimiliki ya ubunifu karibu kwa miaka 30 tu. Katika muda huo wa miaka 30, China imetunga sheria na kanuni zilizo za kamili kuhusu hakimiliki ya ubunifu, ambapo kiasi cha umiliki wa hakimiliki ya ubunifu kinaongezeka kwa kasi, uwezo wa usimamizi na ushindani wa makampuni kuhusu hakimiliki ya ubunifu pia unaimarishwa siku hadi siku, hasa watu wa jamii nzima wameongeza zaidi ufahamu wa kulinda hakimiliki ya ubunifu.
Katika historia, China na Afrika zote ni chimbuko la ustaarabu wa binadamu, na zote zina mali nyingi za urithi wa utamaduni wa binadamu. Kwa mfano watu wa Afrika wanatumia magamba na majani ya miti, mizizi na maua kutengeneza dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa ya binadamu na mifugo, ufanisi wa dawa hizo ni wa dhahiri, na dawa hizo zinafanana sana na dawa za mitishamba za China. Katika miaka ya hivi karibuni, nchini China shughuli za dawa za mitishamba za China zinaendelezwa kwa kasi, ambapo maombi ya kupata hataza kuhusu dawa yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Ofisa wa Sierra Leone anayeshughulikia kazi ya hakimiliki ya ubunifu Bibi Mariana Seray Kallay alimwambia mwandishi wetu habari kuwa anataka kupata maarifa ya China kuhusu kazi hizo. Alisema:
"Kwa sasa ni muhimu sana kwa nchi za Afrika, kufahamu namna ya kuhifadhi matibabu na dawa za jadi na kuhifadhi ujuzi wa mambo ya jadi".
Kutokana na "Waraka wa sera za China kwa Afrika" uliotolewa na serikali ya China mwaka 2006, China na Afrika zitajenga uhusiano wa aina mpya wa kimkakati na kiwenzi ambao pande mbili ziwe na usawa na kuaminiana kwenye mambo ya siasa, zifanye ushirikiano wa kunufaishana katika mambo ya uchumi, na zibadilishane maoni na kufundishana katika mambo ya utamaduni. Na mwaka jana pande hizo mbili zilisaini makubaliano ya ushirikiano kwenye sekta ya hakimiliki ya ubunifu. Mkutano uliofanyika ni hatua moja ya kutekeleza makubaliano hayo, katika siku zijazo mawasiliano na ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta hiyo vitafanyika kwa kufuata hali halisi zaidi.
|