Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-20 20:22:07    
Chuo kikuu cha Suzhou chatoa mchango kwa ushirikiano na mawasiliano kati ya China na Afrika

cri

China siku zote inatilia maanani kuendeleza mawasiliano na ushirikiano kati yake na nchi za Afrika katika sekta mbalimbali. Tangu kuanzishwa kwa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika mwaka 2000, serikali ya China iliimarisha zaidi ushirikiano kati yake na nchi za Afrika katika sekta ya elimu, vyuo vikuu vingi vya China vilibeba jukumu la kuzisaidia nchi za Afrika kuwaandaa watu wenye ujuzi, kikiwemo chuo kikuu cha Suzhou.

Kutokana na kukabidhiwa jukumu na wizara ya elimu ya China, mwezi Septemba mwaka 2005 na mwezi Septemba mwaka 2006 chuo kikuu cha Suzhou kiliandaa semina mbili za kutoa mafunzo ya kuisaidia Afrika kuhusu "kupunguza umaskini na maendeleo ya uchumi", na "kupunguza umaskini na maendeleo ya elimu". Wanafunzi karibu 40 kutoka nchi zaidi ya kumi za Afrika walishiriki kwenye semina hizo. Mkurugenzi wa idara ya ushirikiano wa elimu ya chuo kikuu cha Suzhou Bw. Huang Xing alieleza kuwa, viongozi wa chuo hicho walitilia maanani semina hizo mbili za kutoa mafunzo ya kusaidia Afrika, waalimu walioteuliwa kutoa mafunzo wote ni madaktari na wataalamu na waalimu wazuri wanaoweza kutoa mafunzo kwa kiingereza moja kwa moja. Bw. Huang alisema: 

"kwa kupitia semina hizo, wanafunzi hao wa Afrika waliweza kufahamu hali ya maendeleo ya jamii na uchumi wa China, uzoefu na mafunzo iliyopata China katika kupunguza umaskini na kuendeleza mambo ya elimu, na pia wanafunzi hao wa Afrika wanaweza kuunganisha ujuzi waliopata na hali halisi ya nchi zao, na kujadili njia ya kuondoa umaskini na maendeleo ya elimu ya nchi za Afrika."

Aidha, chuo kikuu hiki kilitoa huduma nzuri kwa wanafunzi hao na kuwasaidia kutatua matatizo mbalimbali yaliyowakabili wakati walipoishi nchini China. Mwanafunzi mmoja kutoka Sudan aliwahi kuvunjika shingo kwenye ajali ya gari, na baada ya kuja China aliona maumivu na hakuweza kujifunza vizuri. Baada ya mwalimu wa chuo hicho kuambiwa hali hiyo, alimpeleka kwa daktari hodari wa kichina mjini Suzhou ili atibiwe, na kumsaidia kupunguza maumivu.

Semina hizo zilisifiwa sana na wanafunzi wa Afrika. Baada ya kumalizika kwa semina hizo, chuo kikuu cha Suzhou kilipata barua iliyoandikwa na naibu katibu wa chama cha MMD cha Zambia, kwenye barua hiyo alimsifu Bibi Frideswide Chanda Chapewa Tute wa Zambia aliyewahi kushiriki kwenye semina ya chuo kikuu cha Suzhou, ambaye anatoa huduma kwa jamii baada ya kurudi nchini Zambia, na wazo la mwanafunzi huyo kuhusu kuendeleza elimu na teknolojia ili kupunguza umaskini na kutoa huduma katika siku za baadaye kutokana na elimu na teknolojia limewapa mwanga wenzake wengi nchini Zambia.

Baada ya kurudi nchini Zambia Bibi Tute alianzisha kundi moja la vijana na kuwashirikisha vijana wanaowajibika kwa jamii na wenye ujuzi na maarifa ya taaluma. Kundi hilo lilipanga kufanya shughuli mbalimbali ili kuimarisha mawasiliano kati ya vijana wa sehemu mbalimbali. Hasa lilipanga kusaidia wanawake na watoto mijini na vijijini kuondokana na umaskini na ubaguzi kwa kupitia shughuli za kueneza elimu. Serikali ya Zambia iliunga mkono mpango huo na kutenga shilingi bilioni 4 za nchi hiyo kwa ajili ya kundi hilo.

Habari zinasema katika mwaka 2007, idadi ya wanafunzi wa Afrika waliokuja kusoma nchini China ilifikia 5,915, ambayo iliongezeka kwa asilimia 58.28 kuliko mwaka 2006. Chuo kikuu cha Suzhou kilianza kuwapokea wanafunzi kutoka Afrika mwaka 2007 kwenye msingi wa kupata uzoefu wa kuandaa semina.

Kijana Tinarwo kutoka Zimbabwe alikuja China mwezi Machi mwaka huu, yeye atajifunza lugha ya kichina kwenye chuo kikuu cha Suzhou, na baadaye ataendelea kusomea kozi ya matibabu kwenye kitivo cha matibabu cha chuo kikuu cha Suzhou. Alisema anaipenda sana China na anataka kuufahamu utamaduni wa China. Baada ya kuja Suzhou alipata marafiki wengi wa China ambao walimsaidia sana. Alisema kwa furaha kuwa ingawa alikuja China muda si mrefu uliopita, lakini anaweza kutumia lugha ya kichina isiyo sanifu kwenda dukani kununua vitu. Akisema: "kujifunza lugha mpya ni jambo gumu sana, lakini sasa ninaweza kuongea kidogo lugha ya kichina, kama nikienda kununua chakula kwenye mkahawa wa McDonald's, naweza kuuliza kwa lugha ya kichina: Coca-Cola ni bei gani?"

Mwanafunzi mwingine kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Kahindo Katsuva Jules alikuja China nusu ya mwaka uliopita, lakini anajua kuzungumza na mwandishi wetu wa habari kwa lugha ya kichina bila matatizo. Akisema: "ninaona kujifunza lugha ya kichina ni vigumu sana, kwa sababu kabla ya kuja China, sikujifunza lugha ya kichina, hivyo ninaona kuandika kichina na kuongea ni vigumu sana. Hivi sasa naweza kuongea na kuandika kidogo lugha ya kichina. Kwenye chuo kikuu cha Suzhou kuna mwalimu anayenifundisha lugha ya kichina, na pia marafiki zangu wananisaidia kuongea kwa kichina na kujifunza kuandika kwa kichina."

Bw. Jules anafurahia maisha yake huko Suzhou, akisema: "ninasoma mjini Suzhou, nimepata marafiki wengi kutoka Japan, Korea Kusini na India, tunafundishana na kusaidiana, hivyo sina tatizo lolote."

Wanafunzi wa kigeni kwenye chuo kikuu cha Suzhou wanapenda mji huo wenye vivutio vingi na wanakipenda chuo kikuu cha Suzhou, Bw. Tinarwo wa Zimbabwe alisema angependa wanafunzi wengi zaidi wa Afrika waende kusoma kwenye chuo hicho. Alisema: "nafurahi sana kusoma nchini China, utamaduni na lugha ya kichina vinanivutia sana, mngekuja kuitembelea China, wachina ni marafiki wazuri na piamtapata kutembelea sehemu nyingi zenye vivutio."