Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-23 21:26:27    
Kiongozi wa chama cha upinzani atangaza kujitoa kwenye duru la pili la uchaguzi nchini Zimbabwe

cri

Kiongozi wa chama cha upinzani Movement for Democratic Changge MDC Bw. Morgan Tsvangirai tarehe 22 alitangaza kujitoa kwenye duru la pili la uchaguzi utakaofanyika tarehe 27 mwezi huu. Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Zimbabwe, kama mgombea mmoja akijitoa kwenye uchaguzi, mgombea mwingine anakuwa rais bila kupigiwa kura. Hii inamaanisha kuwa mgombea wa chama tawala cha ZANU-PF rais wa sasa Robert Mugabe ataendelea kuwa rais katika kipindi kijacho.

Wakati duru la pili la uchaguzi lilipokaribia, viongozi wakubwa wa chama cha MDC tarehe 22 walifanya mkutano huko Harare kujadili kama chama hicho kitashiriki kwenye uchaguzi huo katika hali ya hivi sasa au la. Alasiri ya siku hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari Bw. Morgan Tsvagirai alitangaza uamuzi wa kujitoa kwenye uchaguzi huo, alisema katika hali ambayo matukio ya kimabavu yanatokea mara kwa mara, uchaguzi utakaofanyika hauwezi kuwa huru na wa haki, kura haziwezi kuonesha nia yao halisi, na yeye mwenyewe hatashiriki kwenye uchaguzi huo utakaojaa "hali ya mabavu". Bw. Moragan Tsvangirai aliutaka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuyia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika zifuatilie hali ya Zimbabwe na kuzuia kutokea kwa matukio ya kimabavu. Pia alisema tarehe 25 mwezi huu kama hali ya matumizi ya mabavu ikipungua pengine atabadilisha uamuzi wake na kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Baada ya kupata habari kuwa Bw. Morgan Tsvangirai amejitoa kwenye uchaguzi, msemaji wa chama tawala ZANU-PF Partick Chinamasa alisema sababu ya Morgan Tsvangirai kujitoa kwenye uchaguzi ni kukwepa "kushindwa vibaya". Jumuyia ya kimataifa inafuatilia sana suala hilo. Msuluhishi aliyeteuliwa na Jumuyia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ambaye pia ni rais wa Afrika Kusini Bw. Thabo Mbeki alisema, Afrika Kusini itawahimiza viongozi wa pande mbili wafanye juhudi za kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Tokea mwezi uliopita matokeo ya duru la kwanza la uchaguzi yalipotangazwa na duru la pili la uchaguzi kutangazwa kufanyika tarehe 27 mwezi huu, hali ya Zimbabwe inakuwa mbaya kila kukicha. Chama cha upinzani MDC na chama tawala ZANU-PF vinashutumiana na kupambana na kusababisha vifo vya watu. Kwa mujibu wa maelezo ya MDC, tokea uchaguzi wa duru la kwanza ulipomalizika, watu zaidi ya 70 wanaounga mkono chama hicho wameuawa. Chama tawala pia kimesema, baadhi ya watu wanaounga mkono chama hicho wameuawa.

Matukio ya matumizi ya mabavu yaliyotokea baada ya uchaguzi wa duru la kwanza kati ya vyama hivyo viwili yanafuatiliwa sana na jumuyia ya kimataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon alituma mjumbe wake nchini Zimbabwe kufahamishwa na kuchunguza hatua zilizochukuliwa na serikali ya Zimbabwe katika juhudi za kutuliza hali ya vurugu. Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini alikwenda nchini Zimbabwe, na kwa nyakati tofauti alikutana na rais Robert Mugabe na kiongozi wa chama cha upinzani Bw. Morgan Tsvangirai ili kufanya usuluhisho na kuzitaka pande mbili zifikie maafikiano, kusimamisha shughuli za kimabavu na kuanzisha serikali ya mseto. Lakini hali ya sasa inaonesha kuwa chama tawala na chama cha upinzaji vyote havikubaliani, uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya mseto ni mdogo sana.

Tarehe 29 mwezi Machi mwaka huu uchaguzi mkuu, uchaguzi wa bunge na uchaguzi wa madiwani ulifanyika kwa mara ya kwanza kwa pamoja tokea Zimbabwe ipate uhuru, lakini kutokana na kuwa hakukuwa na mgombea urais aliyepata zaidi ya nusu ya kura, tarehe pili Mei tume ya uchaguzi ilitangaza kwamba waliopata kura nyingi zaidi yaani rais wa sasa Robert Mugabe na kiongozi wa chama cha upinzani Bw. Morgan Tsvangirai watagombea urais katika duru la pili la uchaguzi.