Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-24 18:33:02    
Chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Mkoa wa Guangxi(5)Mji mdogo wa kale wa Huangyao na Mlima Gupo unaowavutia watalii

cri

Kabla ya kuwasomea makala hii, kwanza tunatoa maswali mawili. 1, Mji mdogo wa kale wa Huangyao umekuwa na historia ya miaka mingapi? 2. Kwenye eneo la Mlima Gupo kuna vilele vingapi vya mlima? Tafadhali sikilizeni kwa makini ili muweze kujibu vizuri maswali hayo.

Mji mdogo wa kale wa Huangyao uko kwenye sehemu ya chini ya mtiririko wa Mto Lijiang iliyoko Mjini Hezhou, mashariki mwa mkoa wa Guangxi, na uko kwenye umbali wa kilomita 200 kutoka Mji wa Guilin. Mji wa kale wa Wilaya ya Huangyao umekuwa na historia ya miaka 1036, mji huo kweli umekuwa ni mji wa kale. Mfanyakazi wa Kampuni ya utalii ya Mji wa kale wa Huangyao Bw. Zhu Xianggui alisema, mpangilio mzima wa mji huo unatokana na elimu ya jadi ya China kuhusu mazingira. Alisema:

"Ukiingia kwenye mji huo wa kale, utaona barabara moja kuu, kwenye kando ya barabara hiyo kuna njia nane zilizopindapinda, mji huo wa kale unaonekana kama dragon anayeruka".

Katika zama za kale, Mji wa kale wa Huangyao ulikuwa mji unaojulikana kutokana na shughuli zake za biashara, kwani watu wa familia nyingi kwenye mji huo walishughulikia biashara, na maisha yao yalikuwa mazuri. Ndiyo maana, maduka na nyumba za kila familia pamoja na mahekalu na majengo mengine mbalimbali mjini humo yote yalijengwa vizuri na yalikuwa na mapambo yanayowavutia watu. Majengo hayo yenye historia ya miaka mia kadhaa yamekuwa vivutio vinavyoonesha historia na utamaduni wa mji huo mdogo wa kale. Bw. Zhu Xianggui alisema:

"Katika mji huo mdogo wa kale kuna vivutio vinne vnavyowavutia zaidi watu: Miti ya kale ya banyan; Mto Yaojiang unaopita katikati ya mji; njia zilizotandikwa kwa mawe yenye unene yanayoonekana laini sana, njia hizo zilibaki tangu zamani za kale; na mabanda mengi yenye kumbukumbu nyingi za maandishi".

Mji huo wa kale wa Huangyao uko kwenye sehemu ya kijiolojia yenye chokaa, pembezoni mwa mji huo vimesimama vilele vingi vya milima vyenye maumbo ya ajabu, na mito mitatu ya Yaojiang, Zhujiang na Xingning inazunguka mji huo wa kale, na kuumba mandhari nzuri ya mji huo wa kale.

Mji mdogo wa kale wa Huangyao ni sehemu ambayo watu wa makabila mbalimbali yenye mila na desturi tofauti wanaishi pamoja katika hali ya masikilizano, na kila kabila linaonesha mvuto wake pekee wa utamaduni. Wanawake wa kabila la watuyao na la wapanyao ambayo ni matawi ya kabila la wayao, wanapenda kuvaa mapambo mazuri yanyong'aa vichwani mwao; meza ya kunywea pombe ya watuyao ina urefu wa mita mia moja hivi, ambayo watu mia kadhaa wanaweza kukaa pamoja kunywa pombe kwenye meza ya aina hiyo; wapanyao wana mila na desturi zao za ndoa zinazowafurahisha watu; na watu wa kabila la wazhuang wa kijiji cha Nanxiang wanaoishi huko wanajua sana kuimba, ambao wanapenda kuimba nyimbo na kucheza ngoma usiku.

Wakazi wa mji huo mdogo wa kale wameishi huko kizazi baada ya kizazi tangu zama za kale, ambapo hali halisi ya awali inaonekana popote pale katika mji huo mdogo wa kale, tunaweza kuona wazee wanaowavuta ng'ombe kusaga mchele; tunaweza kuona watu wanaokanyaga kwa miguu chombo cha kuchukulia maji kutoka mtoni; pia tunaweza kuona majengo ya kale ya kutengeneza pombe na kusaga nafaka, ambapo watalii wanaweza kufanya majaribio ya kazi ya jadi kwenye majengo hayo ya kale. Na kisima cha kale cha malaika kilichoko kwenye pembe ya kusini mashariki mwa mji huo wa kale pia ni kivutio kwa watalii.

Kihalisi, Kisima cha kale cha malaika ni safu moja yenye mashimo matano ya visima vya chemichemi, kila shimo la kisima lina upana wa mita 3, na kimo chake ni mita moja hivi, shimo ambalo lilijengwa kwa mawe. Maji ya chemichemi yanabubujika kutoka kwenye mabomba chini ya ardhi, yakiingia kwenye shimo la kwanza la kisima, halafu yanaingia kwa utaratibu kwenye mashimo mengine ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano. Lakini matumizi ya maji ya kila shimo la kisima yanadhibitiwa kwa makini sana. Mkazi wa mji huo mdogo wa kale Bw. Liang Hua alituambia:

"Kisima hiki cha mjini kwetu kinaitwa "Kisima cha kale cha malaika" kimepangwa kwa makini, maji ya shimo la kwanza la kisima ni maji kwa ajili ya kunywa, watu hawaruhusiwi kuyatumia kwa kunawa mikono; maji ya shimo la pili la kisima ni maji kwa ajili ya kusafisha mboga, watu pia hawaruhusiwi kuyatumia kwa kunawa mikono; na maji ya mashimo ya tatu, ya nne na ya tano yanatumika kwa ajili ya kufua nguo. Kufanya hivyo, maji ya kila shimo la kisima yanaweza kutumiwa kwa marudio, na maliasili ya maji inaweza kuhifadhiwa".

Kugawa matumizi ya maji ya kisima kumeonesha busara walizonazo wachina wa zama za kale. Na sehemu iliyoko karibu na kisima ni kama kituo cha upashanaji wa habari, ambapo wanawake wengi wanakusanyika huko kufua nguo na kusafisha mboga, huku wakipiga soga na kupashana habari mbalimbali za mjini, hali ya furaha hujaa huko.

Watu walisema kuwa Mji mdogo wa kale wa Huangyao ni kama kitabu kilichoandikwa historia ya miaka elfu moja, ambacho kilisahauliwa kwenye rafu ndani ya maktaba, na hivi sasa mji huo unafungua ukurasa wake unaong'ara na kuonesha hali yake asili yenye mvuto kwa walimwengu. Bw. Zhu Xianggui alisema:

"Tunawakaribisha marafiki wa nchi mbalimbali waje kwenye Mji wa kale wa Huangyao kutalii, wakazi wa mjini kwetu wanafuata desturi za zama za kale, mjini kwetu kuna mito na milima yenye mandhari nzuri, na vivutio vinavyoonesha historia na utamaduni wa miaka mingi, hakika watalii watafurahia sana".

Katika sehemu iliyoko karibu na Mji mdogo wa kale wa Huangyao kuna Hifadhi ya misitu ya taifa ya Mlima Gupo, hifadhi hiyo ni kivutio cha hali ya maumbile ya dunia.

Hifadhi hiyo ya misitu iko kwenye sehemu inayopakana na mikoa mitatu ya Guangxi, Hunan na Guangdong, eneo lake la jumla ni hekta 8000, kwenye hifadhi hiyo kuna vilele virefu na mabonde ya kina kirefu na mlima mrefu unaotambaa kwenye mazingira mazuri ya utulivu, na hali asili ya miti na majani kwenye hifadhi hiyo inahifadhiwa vizuri, ambapo kuna vilele 25 vya milima vilivyoko kwenye mwinuko wa zaidi ya mita 1000, kati ya vilele hivyo, Kilele cha Tiantangding kiko kwenye mwinuko wa zaidi ya mita 1800 kutoka kwenye usawa wa bahari; kwenye hifadhi hiyo ya misitu pia kuna maporomoko yenye sura ya aina tofauti, baadhi yao yanaonekana kama ni malaika anayeruka mbinguni, mengine yanaonekana kama Buddha aliyekaa, na mengine yana sura nyingine tofauti.

Kwa kuwa misituni kuna miti mingi na maporomoko mengi, hivyo mazingira ya hewa ya Mlima Gupo ni safi sana, sehemu hiyo inasifiwa kuwa ni sehemu yenye negative oxygen ions zaidi kuliko sehemu nyingine kwenye sehemu ya kusini mwa China, na sehemu ya Mlima Gupo ina hali ya hewa nzuri, katika majira ya baridi, sehemu hiyo siyo baridi sana, na katika majira ya joto, sehemu hiyo siyo joto sana, kweli ni sehemu nzuri kwa watu kupumzika na kujiburudisha kwa raha mustarehe. Ofisa mhusika wa sehemu ya vivutio vya Mlima Gupo Bw. Deng Chonglang alisema:

"Wataalamu wa Taasisi ya sayansi ya misitu ya Zhongnan waliwahi kuja kwenye bustani yetu kupima kiasi cha negative oxygen ions, walisema wastani wa ujazo wa negative oxygen ions ni zaidi ya elfu 10 kwa kila sentimita ya ujazo, ujazo huo ni kati ya mara 200 na 300 kuliko ule wa mjini.

Kutokana na mazingira mazuri ya asili, sehemu ya Mlima Gupo pia imekuwa mahali pa kupigia filamu, michezo mingi ya filamu imepigwa kwenye sehemu hiyo, ndiyo maana sehemu hiyo inajulikana zaidi. Hivi sasa sehemu ya Mlima Gupo kila mwaka inawapokea watalii zaidi ya elfu 50 kutoka nchini na nje, mbali na Guilin, sehemu hiyo ni ya pili mkoani Guangxi inayowapokea watalii kwa wingi zaidi. Watalii kutoka nchi mbalimbali duniani wanapenda sana mazingira ya sehemu hiyo, mtalii kutoka Malaysia Bw. Zhang Shengfeng alisema:

"Mimi natoka Malaysia, nilipotazama filamu ya televisheni iliyopigwa na Hong Kong niliona sehemu hiyo ya Mlima Gupo ni yenye mandhari nzuri na hewa safi, tena hali ya hewa siyo joto na siyo baridi, nimekuja kujionea mwenyewe, kweli ni sehemu nzuri, nitawashauri marafiki zangu waje kutembelea".

Mlima Gupo ni sehemu yenye wanyama pori wengi na mimea pori mingi, ukitembea mlimani unaweza kusikia milio ya ndege wa aina mbalimbali pamoja na sauti ya mtiririko wa maji, utajihisi raha mustarehe na kujiona kama umekaa sehemu ya peponi. Tausi wa rangi buluu wanarukaruka kwenye kiwanja cha majani, na kima wadogo wanaocheza mlimani wanapitapita huko.

Idhaa ya kiswahili 2008-06-24