Ofisa mmoja wa Umoja wa Ulaya ambaye hakutaka kutaja jina lake tarehe 23 alidokeza kwamba mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya umekubali kuiwekea Iran vikwazo vipya ikiwa ni pamoja na kuzuia mali za Benki ya Taifa ya Iran na kupiga marufuku watu wanaohusika na mpango wa nyuklia wa Iran kuingia kwenye nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya au kufanya biashara katika nchi hizo.
Ofisa huyo alisema vikwazo vipya vitasimamisha shughuli za benki tanzu za Benki ya Taifa ya Iran katika miji ya London, Hamburg na Paris na kuwapiga marufuku maofisa 20 wa Iran wanaohusika na mpango wa nyuklia kuingia kwenye nchi za Umoja wa Ulaya, kukwamisha mali za mashirika 15 yanayohusika na mpango wa nyuklia, mashirika na watu wa mashirika hayo yatatangazwa tarehe 24, siku ya kuanza kutekeleza vikwazo vipya. Kadhalika ofisa huyo pia alisema kwa sababu vikwazo hivyo vipya vilikuwa vimeamuliwa kwenye mkutano mkuu wa Ulaya na Marekani uliofanyika hivi karibuni nchini Slovenia, vikwazo hivyo vilipitishwa moja kwa moja bila mjadala kwenye mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya. Alisisitiza kwamba mlango wa mazungumzo na Iran bado uko wazi.
Vikwazo hivyo havikutolewa kwa ghafla. Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Rais George Bush wa Marekani kwenye mkutano wa Ulaya na Marekani waliamua kuichukulia Iran hatua kali za kifedha kama Iran haitasimamisha shughuli za mpango wa nyuklia. Hata hivyo, Umoja wa Ulaya unaendelea kufanya juhudi za kidiplomasia ambazo zimefanywa kwa miaka mitatu sasa na kuwa na matumaini ya kutatua suala la nyuklia kwa njia ya amani. Bw. Javier Solana anayeshughulikia mambo ya nje na sera za usalama katika Umoja wa Ulaya tarehe 14 aliwasilisha mpango mpya wa kurudisha mazungumzo na Iran, huu ni mpango uliotolewa na Marekani, Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Mpango huo umeingiza hatua za kunufaisha Iran, lakini kwa uwazi unaitaka Iran kusimamisha kwa muda shughuli za kusafisha uranium.
Vyombo vya habari vimegundua kwamba kuna kutokukubaliana kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuhusu azimio la kuichukulia vikwazo Iran, nchi kadhaa zinataka Marekani ibadili msimamo wake na kuwasiliana na Iran moja kwa moja. Muda si mrefu uliopita rais George Bush wa Marekani alipofanya ziara ya kuaga barani Ulaya, suala la nyuklia la Irani lilizungumzwa mara kwa mara kwenye mazungumzo yake. Lakini ni waziri mkuu wa Uingereza tu ndiye aliyekidhi matakwa ya Marekani kwamba itazuia benki ya Iran nchini Uingereza, na nchi nyingi za Ulaya zilikuwa kimya.
Sambamba na hayo mbele ya juhudi mpya za kidiplomasia za Umoja wa Ulaya katibu wa Kamati ya Usalama ya Iran ambaye pia ni mjumbe wa kwanza wa mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran Bw. Saeed Jalili tarehe 21 alitangaza kuwa Iran inakubali kufanya mazungumzo na nchi husika kuhusu suala la nyuklia la Iran juu ya kanuni za kunufaishana. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Ali Hoseini tarehe 23 huko Teheran kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, Iran iko tayari kufanya mazungumzo, na mazungumzo hayo yatatoa nafasi za kutatua suala la nyuklia kwa ushirikiano kati ya Iran na nchi sita, lakini Iran inatumai kuwa nchi hizo sita zitachukua msimamo huo huo kuhusu pendekezo lililotolewa na Iran. Zaidi ya hayo, kwa mara nyingi Iran ilitangaza kuwa mazungumzo hayatahusika na kusimamisha shughuli zake za kusafisha uranium kwa muda. Kwa hivyo vyombo vya habari vinaona kuwa hata mazungumzo yakirejeshwa hayataziridhisha nchi za magharibi, na kinyume chake, pengine Iran itapata nafasi nyingi zaidi kuendeleza teknolojia yake ya nyuklia.
Wachambuzi wanaona kuwa vikwazo vipya dhidi ya Iran kuweza au kutoweza kuleta matokeo bado ni kitandawili, kwani gazeti moja la Iran liliwahi kutoa ripoti ikisema kwamba sehemu fulani ya mali za Iran kwenye benki barani Ulaya zimebadilishwa kuwa dhahabu na hisa, na sehemu nyingine zimehamishwa kwenye benki za barani Asia. Kama habari hiyo ni ya kweli basi vikwazo havitakuwa na maana yoyote.
|