Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-26 18:27:41    
China ni maskani yangu ya pili

cri

Bw. Abdul Latif Khan alikuja hapa China mwaka 2005, na ameajiriwa na kampuni ya kutengeneza mazulia ya sufi ya kitibet ya Qinghai. Mwaka 2007 kutokana na mchango mkubwa aliotoa katika kuboresha utengenezaji wa mazulia wa China, Bw. Khan alipata tuzo ya urafiki, ambayo ni tuzo ya ngazi ya juu kabisa inayotolewa na serikali ya China kwa wataalam wa kigeni wanaofanya kazi nchini China. Kila mwaka tarehe 1 mwezi Oktoba, yaani sikukuu ya taifa la China, wataalam wanaopata tuzo hiyo hualikwa kuja Beijing, mji mkuu wa China kushiriki sherehe ya kupewa tuzo hiyo, na kukutana na viongozi wa China. Sasa ni miezi kadhaa imepita, lakini Bw. Khan akitaja jambo hilo, bado anakuwa na furaha kubwa. Alisema,

"Jamaa zangu na watu wa maskani yangu wote walifurahi kuambiwa kuwa nimepata tuzo hiyo. Pakistan na China ni nchi marafiki wakubwa. Naona kuwa kupata tuzo hiyo sio tu ni heshima kwangu, watu wengi pamoja na wenzangu walinisaidia, ndio nikaweza kupata tuzo hiyo. Tuzo hiyo ni ya watu wote."

Wafanyakazi wenzake wachina wanamsifu Bw. Khan kwa moyo wake wa kuchapa kazi. Mfanyakazi mwenzake Bw. Xing Kerong alisema, kampuni ilipokuwa inatafiti na kutengeneza bidhaa mpya, Bw. Khan alikuwa anashiriki karibu katika kila mchakato, na kuwafundisha wenzake teknolojia na uzoefu kwa makini. Alisema

"Yeye anachapa kazi kwa bidii, na anawafundisha mafundi wetu wa China bila kuficha. Anachojua anapenda kuwafundisha wengine. Anawafundisha mafundi wengi, na kutusaidia kukabiliana na matatizo mengi ya kiufundi."

Chini ya uongozi wa Bw. Khan, hadi sasa, kampuni ya mazulia ya sufi ya kitibet ya Qinghai imepata hataza 6 za kitaifa katika ufumaji na ufundi wa mazulia, kati ya hataza hizo, moja ilipata tuzo ya kwanza ya "tuzo ya uvumbuzi" ya hataza ya kitaifa na tuzo ya pili ya mafanikio ya sayansi na teknolojia ya taifa la China. Akizungumzia maisha yake nchini China, Bw. Khan alisema, mkoa wa Qinghai ni mkoa wa uwanda wa juu, mwanzoni alipofika huko alikuwa hawezi kuzoea hali ya huko kwa haraka, lakini baadaye alizoea maisha ya huko, na kupenda mkoa huo. Alisema

"Nilizoea maisha ya hapa kwa haraka. Katika wiki mbili za kwanza, nilisikia maumivu kidogo ya kichwa, kwa kuwa mkoa wa Qinghai uko kwenye sehemu yenye mwinuko wa juu kutoka kwenye usawa wa bahari, na hali kwenye maskani yangu ni tofauti kubwa. Lakini baada ya wiki mbili Nilizoea hali ya hapa. Sasa nimeishi hapa Qinghai kwa miaka mitatu, na naipenda hali ya hewa ya hapa."

Bw. Khan alisema ametembelea sehemu nyingi zenye mandhari nzuri mkoani Qinghai ikiwemo ziwa Qinghai, na anazipenda sana sehemu hizo. Hasa mandhari nzuri ya ziwa Qinghai ni kama iliyochorwa kwenye picha. Mbali na kuvutia mandhari nzuri ya sehemu hiyo, anawapenda zaidi marafiki wa China. Bw. Khan alisema, kufanya kazi nchini China ni chaguo la busara katika maisha yake. Alisema,

"Kwa ujumla nilitembelea nchi 7, hii pia ni sehemu ya kazi yangu. Mwishoni nilikuja hapa China, kwani Wachina ni watu wenye urafiki na uchangamfu zaidi, na wanapenda kuwasaidia watu wengine. Kwa kiasi fulani, kuishi nchini China ni kama kuishi katika maskani yangu. Wachina ni wazuri, hasa watu wa mkoa wa Qinghai, unaponunua vitu au kula mkahawani, wanawasiliana nawe kwa urafiki. Watu wa hapa ni wazuri sana, hizi ni hisia zangu kuhusu wachina."

Katika miaka mitatu iliyopita, Bw. Khan ameshuhudia maendeleo kasi ya nchini China, alisema,  

"Nilipofika nchini China mwaka 2005, wakati huo uwanja wa ndege wa Xining ulikuwa mdogo, hata hakukuwa na lifti. Lakini sasa uwanja wa ndege wa Xining unapendeza sana. Vilevile ukilinganisha hali ya mkoa wa Qinghai kwa sasa na ile ya miaka mitatu iliyopita, mkoa huo umebadilika sana, mambo yote yanabadilika na yanabadilika kwa kasi. Mtazamo wa watu wa mkoa wa Qinghai pia unabadilika na kuwa wa wazi zaidi."

Lakini kama ilivyo kwa wageni wengi wanaofanya kazi nchini China, Bw. Khan pia anaona upweke. Ingawa maisha yake nchini China ni ya starehe, na marafiki wa China ni wakarimu, lakini moyoni mwake anakumbuka jamaa zake. Bw. Khan alisema mke wake ni mrembo, na wana watoto wanne wazuri, na waliwahi kuja kumtembelea nchini China mwezi Oktoba mwaka 2007 alipopata tuzo. Alisema:

"Baba yangu ana umri wa miaka 102, anaishi nchini Pakistan, na mke wangu na watoto wangu pia wanaishi huko. Wakati fulani ninawakumbuka sana baba yangu, mke wangu na watoto wangu. Lakini pia napenda kufanya kazi nchini China. Kama ikiwezekana, katika siku za usoni nitawaalika na tuishi pamoja nchini China."

Idhaa ya kiswahili 2008-06-26