Mkutano wa "Wiki ya Maji ya Kimataifa" unaoendelea nchini Singapore umewapatia wajumbe wa nchi mbalimbali nafasi za kujadiliana kuhusu matatizo ya maliasili ya maji, kubadilishana uzoefu wa usimamizi na kuonesha teknolojia mpya zinazotumika katika nyanja ya maji.
Kwenye mkutano huo mwenyekiti wa Mfuko wa Taifa wa Taasisi ya Utafiti ya Singapor Dakt. Tony Tan Keng Yam alipozungumzia suala la maliasili ya maji alisema, huduma ya maji safi ni muhimu sana lakini huduma hiyo haitoshelezi kabisa. Alisema,
"Maji ya kunywa ni mahitaji ya lazima kwa maisha na maendeleo ya jamii yoyote. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, duniani kote maji baridi inachukua 1% tu ya maliasili ya maji, na moja kwa sita ya watu hawapati maji safi. Suala la uhaba wa maji safi litazidi kuwa zito kadiri idadi ya watu na shughuli za kiuchumi zinavyoongezeka, hali hiyo itakwamisha maendeleo ya miji mingi ".
Udhibiti unaofaa wa maliasili ya maji ni msingi wa maendeleo endelevu ya uchumi, na pia ni njia muhimu ya kuhakikisha usalama wa nishati na mazingira safi. Washiriki wa mkutano huo wanajadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya kupambana na uchafuzi wa maji, ushirikiano wa uwekezaji kwenye nyanja ya maji na usimamizi wa matumizi ya maji.
China ni nchi yenye uhaba wa maji, wastani wa umiliki wa maji wa kila Mchina unachukua robo tu ya ule wa kila mmoja duniani. Pamoja na hayo, baadhi ya maeneo uchafuzi wa maji yaliyo karibu na uso wa ardhi unaelekea kuwa mbaya zaidi, na 75% ya maziwa nchini China yamechafuka kwa viwango tofauti. Ili kuhifadhi mazingira ya maji, serikali ya China imechukua hatua nyingi na kutilia nguvu zaidi katika kupambana na uchafuzi wa maji. Naibu waziri wa maji wa China Bw. Hu Siyi alipoeleza uzoefu wa kushughulikia uchafuzi wa maji nchini China alisema,
"Kutokana na uchafuzi wa Ziwa Taihu, mwezi Mei mwaka 2007 msukosuko wa maji ulitokea na kuathiri wakazi milioni kadhaa wa mji wa Wuxi mkoani Jiangsu. Ingawa maeneo ya Ziwa Taihu yalianza mapema katika maendeleo ya uchumi nchini China, lakini hatua za kuzuia uchafuzi wa maji na mazingira haziendani na maendeleo yake ya uchumi.Ili kutatua tatizo la huduma ya maji, serikali ya China na idara husika zilichukua hatua za haraka na kulitatua suala hilo kwa wiki moja tu. Ili kutatua kabisa suala la uchafuzi wa Ziwa Taihu, idara husika zimeandaa "Mpango wa Kuhakikisha Mazingira Safi ya Maji kwenye Maeneo ya Ziwa Taihu" na mpango huo umeidhinishwa na serikali. Lengo la mpango huo ni kutatua kabisa suala la uchafuzi wa maji ya Ziwa Taihu katika muda kati ya miaka mitano na miaka kumi."
Kuhusu udhibiti wa matumizi ya maliasili ya maji, mwenyekiti wa Kundi la Shughuli za Maji la Marekani Bw. Tom Searle alisema,
"Naona kwamba viongozi sio tu wanatakiwa kushughulikia usafi wa maji, bali pia wanatakiwa kushughulika na udhibiti endelevu na wa kikamilifu wa maji, na kujenga miundombinu inayoweza kusaidia marudio ya matumizi ya maji. Kadhalika, kuhakikisha usafi wa maji, kuweka bei ya maji na kutunga sheria za matumizi ya maji, kueneza elimu ya kuthamini maji, n.k."
Benki ya Maendeleo ya Asia siku zote inatoa misaada ya kifedha na kiteknolojia kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya maji ya nchi zinazoendelea za Asia na Pasifiki na inajitahidi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo. Kuhusu usalama wa maji benki hiyo pia imetoa misaada. Meneja mkuu wa benki hiyo Bw. Haruhiko Kuroda alisema benki hiyo itaongeza mtaji wa dola za Marekani bilioni 20 kwa nchi mbalimbali kwenye sehemu za Asia na Pasifiki ili kuhakikisha usalama wa maji vijijini, mijini na kwenye mabonde ya mito.
|