Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-06-27 19:03:29    
Mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea yatazamiwa kuingia katika kipindi kipya

cri

Tarehe 26 Mei Korea ya kaskazini ilikabidhi mpango wake wa nyuklia kwa China ambayo ni nchi mwenyekiti wa mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea. Rais Bush wa Marekani siku hiyo alitangaza kuwa Marekani inataka kufuta jina la Korea ya kaskazini kutoka kwenye "orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi" na kusimamisha vikwazo vyake dhidi ya nchi hiyo.

Pande nyingine zinazohusika na mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea na jumuia ya Kimataifa tarehe 26 zilisifu vitendo vya siku hiyo vya Korea ya kaskazini na Marekani. Waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya kusini Bw. Yu Myung hwan alisema huko Seour kuwa, kitendo cha Korea ya kaskazini ni mwanzo muhimu wa kupata maendeleo halisi katika mchakato wa kuifanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na nyuklia, na kuweka msingi kwa ajili ya hatua ya kuacha nyuklia kwenye kipindi kijacho. Wizara ya mambo ya nje ya Russia ilitoa taarifa ikieleza kufurahishwa na Korea ya kaskazini kukabidhi mpango wake wa nyuklia. Ofisa wa serikali ya Japan alisema, Japan ikiwa upande mmoja unaowajibika wa mazungumzo ya pande 6, itashirika kwa makini kazi ya kuthibitisha mpango huo wa nyuklia. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-mon alitoa taarifa akisema kuwa, Korea ya kaskazini kukabidhi mpango wake wa nyuklia na Marekani kueleza kufurahishwa na hatua hiyo ya Korea ya kaskazini, hii ni hatua kubwa ya kusonga mbele kwa mazungumzo ya pande 6 ili kuifanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na nyuklia.

Kutokana na maendeleo ya vitendo vya kipindi cha pili vya Taarifa ya pamoja ya mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea, kurudisha mazungumzo hayo kumewekwa kwenye ajenda. Vyombo vya habari vya Korea ya kusini tarehe 26 vilisema kuwa, mazungumzo hayo huenda yatarudishwa mwanzoni mwa mwezi Julai, na pande mbalimbali zitajadili kazi ya kuthibitisha mpango wa nyuklia uliokabidhiwa na Korea ya kaskazini, pia zitajadili mpango wa utekelezaji wa kipindi kijacho, huenda ni pamoja na namna ya "kuacha nyuklia", kutoa gharama kiasi gani, namna ya kuufanya uhusiano kati ya Korea ya kaskazini na Marekani uwe wa kawaida, namna ya kupata maendeleo zaidi katika uhusiano kati ya Korea ya kaskazini na Japan ambao umelegea kwa kiasi fulani hivi sasa, na kwa msingi huu namna ya kuanzisha utaratibu wa usalama wa sehemu ya Asia ya kaskazini ya mashariki.

Lakini vyombo vya habari vinaona kuwa, ingawa Korea ya kaskazini na Marekani tarehe 26 zilionesha juhudi zao kwa ajili ya kutatua matatizo, lakini hali hii haimaanishi kuwa utatuzi wa suala la nyuklia la peninsula ya Korea utaendelea bila matatizo katika siku zijazo. Hivi sasa tatizo gumu la kwanza ni kuthibitisha mpango wa nyuklia uliokabidhiwa na Korea ya kaskazini. Ofisa mmoja wa Korea ya kusini alidokeza kuwa, mpango huo uliotolewa na Korea ya kaskazini unaohusu orodha ya majengo ya nyuklia, rikodi kuhusu kiasi cha utengenezaji wa plutonium, kiasi cha upatikanaji wa plutonium na matumizi yake, na akiba ya uranium. Kwa upande wake Marekani tarehe 26 ilitangaza kuwa unataka kufuta vikwazo vikubwa dhidi ya Korea ya kaskazini ndani ya siku 45. Katika kipindi hiki, Marekani itathibitisha usahihi wa mpango wa nyuklia uliokabidhiwa na Korea ya kaskazini, na Korea ya kaskazini inapaswa kufanya ushirikiano wa kutosha, ama sivyo Marekani itachukua hatua husika. Serikali ya Japan pia ilieleza matumaini yake kuwa, katika muda wa kipindi hiki, Korea ya kaskazini ingeonesha udhati wake wa kuufanya utatuzi wa suala la mateka upate maendeleo. Aidha, vyombo vya habari vya Korea ya kusini vilisema kuwa, katika mpango huo wa nyuklia uliotolewa na Korea ya kaskazini, hakuna orodha kuhusu idadi ya silaha za nyuklia na ufafanuzi wa Korea ya kaskazini kuhusu mpango wake wa uranium nzito na suala la uenezaji wa nyuklia, hivyo serikali ya Korea ya kusini imesikitishwa na mpango huo uliotolewa na Korea ya kaskazini.

Hivi sasa vitendo vya utekelezaji vya kipindi cha pili vya mazungumzo ya pande sita bado vinatakiwa kukamilishwa. Vyombo vya habari vimedhihirisha kuwa, pande mbalimbali zinapaswa kushika fursa nzuri, kuongeza zaidi hali ya kuaminiana na kuwasiliana ili kuhimiza mazungumzo ya pande 6 yapate maendeleo siku hadi siku.