Mkutano wa 11 wa wakuu wa Umoja wa Afrika unafanyika tarehe 30 Juni na tarehe 1 Julai huko Sharm el Sheikh, nchini Misri. Masuala yanayofuatiliwa zaidi kwenye mkutano huo ni suala la maji na afya, msukosuko wa chakula na hali ya kisiasa nchini Zimbabwe.
Ajenda kuu ya mkutano huo ni jinsi ya kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia yanayaohusu maji na afya. Kwa mujibu wa malengo ya maendeleo ya milenia yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa, idadi ya watu wasioweza kupata huduma za maji safi ya kunywa na huduma za kimsingi za afya itapungua kwa nusu kabla ya mwaka 2015. Katika miaka ya hivi karibuni Afrika imepata maendeleo kiasi katika kuboresha usalama wa maji ya kunywa na hali ya afya, hata hivyo maendeleo hayo hayana uwiano na ongezeko la idadi ya watu barani Afrika. Takwimu zinaonesha kuwa, kati ya mwaka 1990 na 2006 idadi ya waafrika waliokosa maji safi ya kunywa iliongezeka hadi kufikia watu milioni 340 kutoka milioni 280 na idadi ya waafrika wasio na huduma za kimsingi ya afya iliongezeka hadi kufikia watu milioni 580 kutoka milioni 430. Ukosefu wa maji safi ya kunywa na huduma za afya si kama tu umesababisha kutokea kwa maradhi mbalimbali, bali pia umeathiri vibaya maendeleo ya uchumi wa Afrika. Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa mwezi Aprili mwaka jana inasema, katika baadhi ya nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Sahara, matatizo yanayotokana na ukosefu wa maji na afya yalikuwa yanagharimu asilimia 5 ya mapato ya nchi hizo, na kiasi hicho ni kikubwa zaidi kuliko misaada ya maendeleo iliyopokelewa na nchi hizo.
Hivi sasa ni miaka saba tu imebaki kabla ya kutimiza malengo ya maendeleo ya milemia yanayohusu huduma za maji na afya. Kwa hiyo mkutano huo wa wakuu wa Umoja wa Afrika utajadili masuala yanayokwamisha kutimizwa kwa malengo hayo na kutafuta ufumbuzi wa masuala hayo. Imefahamika kuwa mkutano huo utatoa taarifa kuhusu suala hilo.
Msukosuko wa chakula ni suala lingine linalofuatiliwa kwenye mkutano huo. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, bei ya chakula duniani imekuwa ikipanda kwa kasi. Takwimu mpya zilizotolewa na Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, kati ya nchi 37 duniani zinazosumbuliwa zaidi na tatizo la kupanda kwa bei ya chakula, nchi 21 ziko barani Afrika. Huu ni Mkutano mkubwa wa kwanza kwa viongozi wa nchi za Afrika tangu kuibuka kwa msukosuko wa chakula duniani. Inatarajiwa kuwa viongozi hao watabadilishana uzoefu wa kukabiliana na msukosuko huo, kujadiliana jinsi nchi za Afrika zinavyoshikamana na kushirikiana katika kukabiliana na msukosuko wa chakula, na kutoa hatua halisi.
Mkutano huo pia utazungumzia hali ya Zimbabwe. Tarehe 27 Juni kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, mwenyekiti wa kamati ya umoja huo Bw. Jean Ping alieleza kuwa, kwenye mkutano wa wakuu, viongozi wa Afrika watatoa tathmini kuhusu hali ya Zimbabwe na kutoa taarifa ya pamoja.
Tokea kampeni ya uchaguzi mkuu ilipoanza nchini Zimbabwe, matukio ya kimabavu yamekuwa yakiendelea kutokea kati ya wafuasi wa chama tawala na chama cha upinzani. Hivi karibuni nchi za magharibi zikiwemo Uingereza na Marekani zimekuwa zikiendelea kuiwekea shinikizo serikali ya Zimbabwe, lakini nchi nyingi wanachama wa Jumuiya ya SADC na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika bado hazijatoa maoni wazi. Ndiyo maana kuhusu hali ya Zimbabwe, kama nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zitaweza kuwa na msimamo mmoja na kutoa mbinu za kutatua msukosuko nchini Zimbabwe ni suala linalofuatiliwa sana kwenye mkutano huo.
|