Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-01 15:53:31    
Mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika wajadili masuala ya maji na usafi

cri

Mkutano wa 11 wa wakuu wa Umoja wa Afrika ulifunguliwa tarehe 30 Juni huko Sharm el Sheikh, nchini Misri.   Rais Hosni Mubarak wa Misri, ambayo ni nchi mwenyeji wa mkutano huo, akihutubia ufunguzi wa mkutano huo, alisema "Hivi sasa dunia nzima inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo msukosuko wa chakula, kupanda kwa bei ya nishati, pamoja na athari za nishati ya kiviumbe na mabadiliko ya hali ya hewa. Jumuiya ya kimataifa inapaswa kubeba wajibu, kufanya mazungumzo yanayosaidia kwa dhati juu ya masuala hayo, na kuchukua hatua kwa pamoja ili kuondoa misukosuko hiyo."

Rais Mubarak alisema, ajenda muhimu ya mkutano huo ni kusawazisha msimamo wa nchi za Afrika katika kukabiliana na misukosuko hiyo. Alisema  "Afrika ni sehemu inayoathiriwa vibaya zaidi na misukosuko hiyo duniani. Masuala hayo yote yana uhusiano wa karibu na maendeleo ya kilimo. Afrika inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Katika mkutano huo, nchi za Afrika zitasawazisha msimamo na kuionesha jumuiya ya kimataifa msimamo mmoja wa Afrika kuhusu masuala hayo."

Ajenda kuu ya mkutano huo ni jinsi ya kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia yanayohusu maji na afya. Kwa mujibu wa malengo ya maendeleo ya milenia yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa, idadi ya watu wasioweza kupata huduma ya maji safi ya kunywa na usafi wa mazingira wa kimsingi itapungua kwa nusu kabla ya mwaka 2015. Kuhusu ajenda hiyo kuu mtaalamu wa Taasisi ya sayansi ya kijamii ya China Bw. Zhang Yongpeng alisema  "Hadi sasa mchakato wa maendeleo ya Afrika unaonesha kuwa, maji na afya ni masuala yenye uhusiano wa karibu. Zamani kutokana na migogoro ya kikanda, idadi ya watu barani Afrika ilipungua sana, na hivi sasa migogoro mbalimbali imetulizwa, na upatikanaji wa maji safi ya kunywa una uhusiano wa karibu na afya ya watu wa Afrika. Kwa hiyo katika kujadili maendeleo ya Afrika, suala la maliasili ya maji ni suala la kimkakati linalotakiwa kuzungumzwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika."

Katika juhudi za nchi za Afrika kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia, pamoja na jitihada za nchi hizo zenyewe, vile vile inapaswa kupata msaada na uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa. Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Asha Rose Migiro aliyehudhuria ufunguzi wa mkutano huo, alitoa hotuba akisema kuwa Umoja wa Mataifa unaunga mkono Umoja wa Afrika uendelee kupata maendeleo katika juhudi za kuleta amani na ustawi barani Afrika. Alisema (sauti 5) "Umoja wa Mataifa unaahidi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Umoja wa Afrika katika kuleta amani na ustawi barani Afrika. Tukishirikiana tutachangia ujenzi wa Afrika yenye mustakabali mzuri zaidi. Afrika itaweza kutumia ipasavyo nguvu yake kubwa kama itazingatia ufuatiliaji na matakwa ya nchi za Afrika."