Shirika la Fedha la Kimataifa IMF tarehe mosi Julali kwenye makao makuu yake mjini Washington, lilitoa ripoti ya ufafanuzi kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta na chakula duniani. Ripoti hiyo inasema hivi sasa kazi za haraka zinazozikabili nchi zote ni kutatua tatizo la chakula na huku zikihakikisha utulivu wa uchumi duniani ambao haukupatikana kwa urahisi. Ripoti hiyo imefafanua hali ya nchi 150 kuhusu mapato na matumizi, bajeti na bei ya bidhaa kuanzia mwaka 2006 hadi sasa. Ripoti inasema hivi sasa uchumi duniani umekuwa katika kipindi cha kupanda kwa bei kwa haraka na kwa upana kabisa tokea miaka ya 70 mfumuko wa bei ulipotokea duniani. Bei ya mafuta sasa imepanda hadi zaidi ya dola za Marekani 140 kwa pipa kutoka dola za Marekani 30 mwaka 2003, ni ongezeko la 35% ikilinganishwa na bei ya mwaka 1979. Bei ya chakula imechelewa kidogo kuanza kupanda, tokea mwaka 2006 hadi sasa bei ya chakula bado haijapanda zaidi ya bei ilipokuwa katika miaka ya 70. Kati ya bidhaa za chakula bei ya nafaka na mafuta imepanda zaidi. Mkurugenzi wa IMF Bw. Dominique Strauss-Kahn alisema hivi sasa uchumi duniani unakumbwa na changamoto kubwa. Alisema
"Hii ni changamoto kubwa, ingawa hali ya kila nchi ni tofauti, lakini changamoto hiyo ni sawa kwa kila nchi, kazi ya haraka kwa sasa ni namna ya kutatua tatizo la chakula na kuhakikisha utulivu wa uchumi duniani na kujaribu kwa juhudi kupata uwiano kati ya mambo hayo mawili."
Naibu mkurugenzi wa kitengo cha utafiti wa sera za maendeleo katika IMF Bw. Particia Alonso-Gamo alisema nchi nyingi zimezama katika hali mbaya kutokana na kupanda kwa bei ya chakula na mafuta. Alisema,
"Nchi nyingi zinakumbwa na mashinikizo hayo mawili. Uchunguzi umegundua kwamba akiba za fedha za kigeni katika nchi 37 zenye mapato ya chini na nchi 25 zenye mapato kiasi zinaweza kutosheleza matumizi ya miezi mitatu tu, na kati ya nchi hizo, nyingi ni nchi zinazoingiza mafuta kutoka nje. Bei ya mafuta ina athari kubwa kuliko athari ya bei ya chakula katika matumizi na mapato duniani. Hii ni rahisi kuelewa kwamba kwa nchi zenye mapato ya chini, mafuta yanayoingizwa ni mara 2.5 kuliko chakula kinachoingizwa. Zaidi ya hayo athari ya kupanda kwa bei ya mafuta na chakula ni kubwa kwa mfumuko wa bei, na athari ya kupanda kwa bei ya chakula ni kubwa zaidi."
Bi. Sanjeev Gupta alisisitiza kwamba baadhi ya nchi zinashindwa kuhimili mashinikizo hayo mawili, lakini nchi nyingine kama vile nchi zinazouzwa mafuta nje zinapata faida kutokana na hali hiyo. Kupanda kwa bei ya mafuta na chakula kumeleta tishio kubwa katika juhudi za kuondoa umaskini, kuhakikisha usalama wa chakula na utulivu wa uchumi duniani. Bw. Sanjeev Gupta ni mtaalamu wa kitengo cha mambo ya fedha katika IMF alisema serikali za nchi mbalimbali zimechukua hatua za kupambana na hali mbaya kutokana na kupanda kwa bei. Alisema,
"Serikali za nchi mbalimbali zimechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na hali ya kupanda kwa bei ya chakula na mafuta, hatua hizo ni pamoja na kupunguza kodi ya mafuta na chakula, kuongeza marupurupu, mishahara na malipo ya uzeeni."
Bw. Sanjeev aliongeza kuwa nchi 150 zilizotajwa katika ripoti hiyo karibu nusu ya nchi hizo zinatumia 0.6% ya pato la taifa GDP kuanzia mwaka 2007 hadi 2008 kwa ajili ya kutekeleza hatua hizo, na 20% ya nchi hizo zimetumia 1% kwa ajili ya kutekeleza hatua hizo. Bei ya mafuta na chakula itakavyokuwa baadaye inafuatiliwa sana duniani. Mtaalamu wa IMF Bw. Thomas Helbling alisema kutokana na mambo mengi yasiyoweza kubainika, hali ya baadaye pia haitakuwa nzuri.
|