Maofisa wa ngazi ya juu pamoja na watafiti wa baadhi ya jumuiya za kimataifa wapatao zaidi ya 200, walikuwa na kongamano tarehe 2 huko Washington kujadili namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na kupanda kwa bei za nafaka duniani kwa hivi sasa. Washiriki wanaona kuwa mgogoro wa nafaka wa hivi sasa umevuka masuala ya nafaka na kilimo, hivyo jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuutatua mgogoro huo kwa njia ya ushirikiano. Mkurugenzi wa Benki ya dunia Bw Robert Zoelick alisema,
"Ninaona, kuna upungufu wa mazao ya kilimo na chakula kwenye soko la kimataifa, sasa nchi nyingi zimechukua hatua za kutuliza bei kutokana na shinikizo, nchi hizo licha ya kudhibiti usafirishaji nafaka kwa nje, pia zimebatilisha makubaliano mengi. Hali hii inadhihirisha kuwa akiba ya nafaka imepungua sana. Nchi zenye pato dogo, sasa zinatatizwa na kupanda kwa bei za chakula na mafuta ya petroli. Utafiti mwingi uliofanywa na jumuiya husika katika miezi michache iliyopita ni kuhusu kupanda kwa bei za chakula. Kutokana na hali ilivyo ya hivi sasa, ninaona kupanda kwa bei za chakula kunahisiana sana na kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli."
Bw Robert B. Zoellick aliyasema hayo kwenye kongamano lililoandaliwa na taasisi moja ya utafiti ya Marekani. Mtafiti wa taasisi hiyo ya Marekani, Bw. Mauro De Lorenzo anakubaliana na maoni ya Bw. Zoellick, akiona kuwa mgogoro wa nafaka wa hivi sasa umekuwa ni zaidi ya nafaka na kilimo, na umeingiliana na mambo mbalimbali ya maeneo mengine, hivyo hali ya sasa ni yenye matatizo mengi. Alisema,
"Mgogoro wa nafaka wa hivi sasa ni tofauti na ule wa zamani, na umekuwa ni moja ya masuala muhimu yanayofuatiliwa sana duniani. Chanzo na matokeo yake yamefikia hata kwenye utoaji wa misaada ya kibinadamu, na yameingia katika maeneo mengine, ambayo hapo zamani hayakuwa na uhusiano mkubwa na chakula na kilimo."
Kutokana na dunia kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa nafaka, mkuu wa Benki ya Dunia, Bw. Zoelick alisema, kutokana na mabadiliko ya hali ya idadi ya watu, muundo wa chakula wa watu, mwelekeo wa bei za nishati, maendeleo ya nishati ya ikolojia na mabadiliko ya hali ya hewa, kupanda kwa kiwango kikubwa kwa bei za nafaka na hali ya msukosuko bado vitaendelea kwa muda fulani. Na ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoletwa na mgogoro wa nafaka, majukumu ya Benki ya Dunia pia yanabadilika. Bw. Zoellick alisema,
"Mabadiliko ya majukumu ya Benki ya Dunia ni kwamba tunatumia chombo cha mambo ya fedha kwa unyumbufu mkubwa zaidi, na kuchukua hatua kwa haraka. Kuna mabadiliko mengine ni kwamba Benki ya Dunia inabadilika kuwa shirika la kutatua matatizo kutoka taasisi ya kufanya utafiti na kutoa ripoti."
Kuendeleza matumizi ya nishati ya ikolojia ni moja ya masuala muhimu yaliyofuatiliwa kwenye kangamano hilo. Naibu mkurugenzi mkuu wa kwanza wa zamani wa shirika la mfuko wa sarafu wa duniani, ambaye mtafiti maarufu wa chuo kikuu cha Johns Hopkins, Bi. Anne Krueger alisema, katika muda mfupi wa baadaye, kubadilisha sera za nishati ya ikolojia kunaweza kupunguza mgogoro wa nafaka. Mbunge wa taifa wa jimbo la Indiana, ambalo linazalisha mazao ya kilimo kwa wingi nchini Marekani, Bw. Richard Lugar alisema, ili kukabiliana na mgogoro wa nafaka wa hivi sasa, tunapaswa kuchukua hatua za dharura, vilevile tunatakiwa kujenga msingi madhubuti wa usalama wa chakula wa dunia. Washiriki wote wanasema, kukabiliana na mgogoro wa nafaka kunahitaji ushirikiano mkubwa wa jumuiya ya kimataifa.
|