Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-07 15:36:22    
Wanawake wa kabila la Wali wanaopenda kufuma kitambaa cha Lijin

cri
Kabila la Wali ni kabila dogo lenye idadi kubwa zaidi ya watu mkoani Hainan kusini mwa China. Kama ilivyo kwa makabila mengine madogo madogo nchini China, kabila hilo lina desturi na utamaduni wake maalumu, na kitambaa cha Lijin ni kitu kizuri cha kisanaa kinachotengenezwa na wanawake wa kabila la Wali.

Kila wanapotembelewa na wageni muhimu, wanawake wa kabila la Wali wanawakaribisha kwa kuimba nyimbo nzuri wakiwa wamevaa sketi zilizotengenezwa kwa vitambaa vya Lijin. Kitambaa hicho kinafumwa kwa kusokota nyuzi za sufu maalumu zinazopatikana kutoka kwenye miti, ni kitambaa chenye historia ndefu zaidi nchini China, na kinasifiwa kama "Kisukuku Hai" katika historia ya utengenezaji nguo nchini China. Wanawake wa kabila la Wali wanafuma vitambaa vya Lijin vyenye rangi mbalimbali kwa kutumia vifaa rahisi.

Bibi Wang Xuebing mwenye umri wa miaka 32 anaishi kwenye kijiji cha Zana cha tarafa ya Chongshan ya mji wa Wuzhishan mkoani Hainan. Alianza kujifunza kufuma kitambaa cha Lijin wakati alipokuwa na umri wa miaka zaidi ya kumi, na sasa yeye ni mfumaji hodari wa kitambaa cha Lijin kwenye kijiji cha Zana. Bibi Wang Xuebing alisema,

"Nilipokuwa mtoto mwenye umri wa miaka kumi, niliwaona watu wakifuma kitambaa cha Lijin, nikawaomba wanifundishe. Nilifahamu ufundi wao baada ya wiki moja tu, kwa kuwa nilipenda sana kufanya kazi hiyo."

Ni watu wachache tu kama bibi Wang Xuebing aliyepata ufundi wa kufuma kitambaa cha Lijin kwa wiki moja, na kwa kawaida watajifunza kwa mwezi mmoja, halafu watakuwa na uwezo wa kufuma kitambaa hicho.

Kufuma kitambaa cha Lijin ni kazi ya kuchosha, kwa kuwa wafumaji wanakaa mbele ya vifaa vya kutengeneza kitambaa wakitokeza miguu na kukanyaga vifaa hivyo ili kukaza nyuzi za kitambaa. Lakini bibi Wang Xuebing alisema hachoki hata kama akifanya kazi hiyo kwa siku nzima. Alisema,

"Kila ninapoona mtindo mzuri wa ufumaji, ninataka kujifunza. Nikianza kufuma kitambaa, siwezi kuacha bila kujali uchovu au njaa."

Bibi Wang Xuebing alisema hivi sasa mradi wa ukarabati wa nyumba mbovu unafanywa vijijini na idara husika za serikali, nyumba yake aliyohamia hivi karibuni ni mpya. Alisema sasa anashughulikia kusafisha nyumba na kazi za mashambani, akiwa na nafasi, anafuma kitambaa cha Lijin.

Maisha ya wanawake wengine wa kabila la Wali ni kama ya bibi Wang Xuebing, baada ya kumaliza kazi za kilimo na kazi za nyumbani, wanafuma vitambaa vya Lijin, na hali hii inatokana na wao kupenda, pia ni kwa ajili ya kupata mapato. Wanatengeneza vitambaa kutokana na matakwa ya makampuni ya vitambaa vya Lijin, na wanaweza kufanya kazi hii nyumbani au kwenye karakana za makampuni hayo. Bibi Wang Binxue aliwahi kufanya kazi kwenye taasisi ya sanaa ya vitambaa vya makabila madogo madogo ya Hainan. Alisema,

"Kwenye taasisi hiyo, wafanyakazi wanafuma vitambaa vyenye umaalumu wa makabila tofauti, na vitambaa hivyo vinauzwa katika nchi za nje zikiwemo Marekani na Japan."

Bibi Wang Xuebing alijulisha kuwa sasa anafuma vitambaa baada ya kazi nyingine, anaweza kutengeneza vitambaa kati ya viwili hadi vitatu kwa mwezi, na kila kimoja kinauzwa kwa yuan mia kadha.

Kampuni ya Maendeleo ya Utamaduni wa Kitambaa cha Lijin ya Wuzhishan ni moja kati ya makampuni yanayonunua vitambaa kutoka wanawake wa kabila la Wali. Kampuni hiyo ilianzisha vituo kadhaa kwenye sehemu ya Wuzhishan, na kuwaajiri wanawake wengi wanaojua kufuma kitambaa cha Lijin. Meneja mmoja wa kampuni hiyo bibi Lu Shaosui alisema wanawake hao wanafanya kazi ya ufumaji kwa saa nne kila siku, na wanapata mapato ya yuan elfu moja kwa mwezi. Bibi Lu Shaosui alisema,

"Vitambaa hivyo vinauzwa kwenye mikoa mingine nchini China, vinachukuliwa kuwa zawadi kubwa kwa wageni muhimu. Kampuni yetu inashughulikia kuuza vitambaa hivyo, wakulima hawana wasiwasi wa kutoweza kuuza vitambaa vyao."

Bibi Li Chunying amefanya kazi kwenye kampuni hiyo kwa muda mrefu, na kila siku anafuma vitambaa kuanzia saa moja na nusu asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni. Alisema anapenda zaidi kufanya kazi pamoja na wanawake wenzake kwenye kampuni hiyo kuliko nyumbani, alisema,

"Tunafuma vitambaa vya Lijin kutokana na matakwa ya wateja. Wanawake wengi wanafanya kazi pamoja huku wakiimba nyimbo, na tunafurahi sana."

Imefahamika kuwa kutokana na watu wanaofahamu kutumia vifaa vya kufuma kitambaa cha Lijin kupungua siku hadi siku, uzalishaji wa vitambaa hivyo pia unapungua. Miaka miwili iliyopita, ufundi wa kutengeneza vitambaa vya jadi vya kabila la Wali uliwekwa kwenye orodha ya mabaki ya utamaduni ya China, na ufundi huo ukaanza kufuatiliwa zaidi na watu. Kwenye sehemu ya Wuzhishan, hata kina bibi wenye umri wa miaka zaidi ya 80 hawataki kuachana na ufundi huo, na wanafuma kitambaa kwa saa kadhaa kila siku, wakati huo huo mtu mdogo zaidi aliyefahamu ufundi huo ana umri wa miaka 6 tu.

Wakati ufundi wa kufuma kitambaa cha Lijin unaporithiwa, pia unawasaidia wakulima wa kabila la Wali kuondoa umaskini. Mkurugenzi wa idara ya kuwasaidia watu kuondokana na umaskini ya mji wa Wuzhishan bibi Huang Xuemei alisema, miaka minne iliyopita, serikali ya mji huo ilianza kuandaa mafunzo ya ajira kwa ajili ya wakulima, na ufundi wa kufuma kitambaa cha Lijin pia unafundishwa kwenye mafunzo hayo. Alisema,

"Kufundisha ufundi wa kufuma kitambaa cha Lijin ni kwa ajili ya kurithi utamaduni wa kabila la Wali, pia tunauchukua kuwa ni kazi ya kuwasaidia wakulima kuongeza mapato, na mafunzo hayo yamewanufaisha sana."

Bibi Huang Xuemei alisema serikali pia ilifanya uchunguzi wa soko, na kuwaalika wataalamu kuboresha mbinu za kufuma kitambaa cha Lijin, ili kuongeza ufanisi wa kutengeneza kitambaa hicho. Wanawake wengi wa kabila la Wali walieleza matarajio yao kuwa, ufundi wa kufuma kitambaa cha Lijin utarithiwa kizazi baada ya kizazi, na kuwa mali ya utamaduni ya China.

Idhaa ya kiswahili 2008-07-07