Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-07 17:06:32    
Kutalii kwenye kijiji cha Shifo cha mji wa Zhengzhou

cri

Katika miji mingi mikubwa ya China kuna sehemu moja yenye wakazi wengi wasomi na wachoraji wa michoro ya sanaa. Kwa mfano kiwanda No. 958 cha Beijing na sehemu ya wasanii iliyoko kando ya mto Suzhou mjini Shanghai. Katika kipindi hiki cha leo, ninawafahamisha kuhusu "Jumuiya ya sanaa ya sanamu ya Buddha ya mawe ya Henan" iliyoko mjini Zhengzhou, mkoa wa Henan, sehemu ya kati ya China.

"Jumuiya ya sanaa ya sanamu ya Buddha ya mawe ya Henan" iko katika kijiji cha Shifo cha mji wa Zhengzhou, katika lugha ya Kichina, Shifo ni sanamu za mawe. Kijiji hicho kiko kwenye kiasi cha umbali wa kilomita 10 kaskazini magharibi mwa mji wa Zhengzhou. Kwenye upande wa kaskazini magharibi mwa kijiji hicho kuna hekalu moja la kale, kutokana na maelezo yaliyochongwa kwenye jiwe la kumbukumbu lililoko kwenye hekalu hilo, hekalu hilo lilijengwa katika mwaka wa kwanza wa enzi ya Tang ya karne ya 7. Ndani ya hekalu hilo kuna sanamu moja ya mawe ya Buddha yenye kimo cha zaidi ya mita 2, sanamu hiyo ilichongwa kwa ufundi mkubwa, na inaonekana kama Buddha hai, kwa hiyo hekalu hilo lilipewa jina la hekalu la sanamu ya Buddha ya mawe, na kijiji lilipo hekalu hilo kikaanza kuitwa kijiji cha sanamu ya Buddha ya mawe.

Mazingira ya Kijiji cha Shifo ni safi na utulivu. Mwezi Aprili mwaka 2006, mchoraji bingwa wa Marekani mwenye asili ya China, Bw. Huang Guorui alivutiwa na sehemu hiyo, akaanzisha studio katika kijiji hicho, na alipaka kuta za nyumba rangi ya manjano, na kujenga studio yeye mwenyewe kwenye ghorofa ya nyumba, studio ikawa mfano wa kuigwa, hapo baadaye wasanii wengine wakiwemo Bw. Wang Yiding na Bw. Su Xiaoshi pia walijenga studio zao kwenye ghorofa ya nyumba zao. Wasanii hao walianzisha "Jumuiya ya sanaa ya sanamu ya Buddha ya mawe ya Henan" tarehe 30 mwezi May mwaka huo. Baada ya hapo, wasanii wengi walihamia huko. Katika muda wa zaidi ya mwaka mmoja, studio zaidi ya 100 zilianzishwa katika kijiji hicho, na kijiji hicho kimekuwa kijiji cha kipekee mkoani Henan chenye wakazi wasanii wengi wa aina mbalimbali.

Mgeni akiingia kwenye kijiji hicho atavutiwa na umaalumu wa huko, michoro mingi ilichorowa kwenye kuta za nyumba zilizoko kwenye kando mbili za njia. Mchoraji wa Marekani mwenye asili ya China Bw. Huang Guorui alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, mwanzoni baada ya kurudi China, studio yake ilikuwa katika mji wa Beijing, muda si muda alichoshwa na adha bei kubwa za vitu pamoja na makelele ya mji mkubwa, hatimaye aliamua kurejea kwao, kijiji cha Shifo kilichoko mkoani Henan. Ikilinganishwa na studio za wasanii wengi wa Beijing na Shanghai, "Jumuiya ya sanaa ya sanamu ya Buddha ya mawe ya Henan" inawavutia wasanii wengi kutokana na mazingira safi na utulivu na bei rahisi za vitu. Bw. Huang Guorui alisema,

"'Jumuiya ya sanaa ya sanamu ya Buddha ya mawe' ilipoanzishwa ni mimi pekee yangu niliamua kujenga studio katika kijiji hicho, hapo baadaye studio zilizojengwa zilifikia 6, 7 hadi zaidi ya kumi, katika wakati wa kufanya maonesho kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa jumuiya yetu, maonesho yalishirikisha wasanii zaidi ya 30. Hivi sasa, wasanii zaidi ya 100 wa michoro ya rangi ya mafuta, michoro wa kichina, sanaa ya maandiko ya hati ya mkono, sanaa ya uchongaji wa sanamu, wapiga picha, sanaa ya ufinyanzi na waongozaji upigaji wa michezo ya sinema na kuigiza wamepanga nyumba katika kijiji hicho."

Katika muda wa zaidi ya mwaka mmoja tangu ianzishwe "Jumuiya ya sanaa ya sanamu ya Buddha ya mawe", jumuiya hiyo imefanya maonesho manne katika kijiji hicho. Mwanzoni mwa mwaka huu, jumuiya hiyo ilifanya maonesho kwenye ukumbi wa maonesho ya sanaa ya michoro wa SOHO 456 iliyoko mjini New York, Marekani, vitu vya sanaa vilivyooneshwa viliwapa watazamaji kumbukumbu nyingi. Bw. Huang Guorui alisema,

"Maonesho yetu yalifunguliwa tarehe 8 mwezi Januari katika sehemu ya Manhattan mjini New York, maonesho hayo yalifana kabisa na yaliwavutia wasanii wengi wa New York. Wasanii, wahakiki na wapanga mipango ya maonesho wa kawaida wanafahamu miji mikubwa ya Beijing na Shanghai, na hawafahamu mkoa wa Hehan. Kwa hiyo lengo la maonesho yetu hayo ni kuwafahamisha kuhusu wasanii wa sasa wa Henan, na sanaa ya kisasa ya kijiji cha Shifo. Baada ya kuangalia maonesho yetu, wanapenda sana kuangalia Henan, kuangalia mji wa Zhengzhou na kijiji cha shifo.

Kuingia kwa wasanii katika kijiji cha Shifo kunanufaisha pande zote mbili za wasanii na wakulima wa kijijini. Wasanii waliohamia kijijini walisaini makubaliano na wakulima wenyeji, wanajenga studio kwenye sehemu ya juu ya nyumba za wenyeji, wasanii wakijenga studio kwa fedha zao katika nyumba za wakulima, hawatozwi kodi ya nyumba kwa miaka kumi, na faida wanayopata wakulima ni kuwa baada ya miaka kumi, studio zilizojengwa zitakuwa mali ya wakulima. Ikiwa wasanii wataendelea kutumia studio zao baada ya miaka kumi, watapaswa kukodi studio kwa wakulima. Kodi ya studio moja kwa mwezi ni Yuan 50. "Jumuiya ya sanaa ya sanamu ya Buddha ya mawe" inaungwa mkono na serikali ya huko, serikali imegharimia fedha ya kujenga zana za miundo-mbinu za kijiji cha Shifo. Katika miaka 2 iliyopita, kadiri wasanii wengi walivyofika kwenye kijiji cha Shifo, ndivyo kijiji cha Shifo kilivyotokewa na mabadiliko makubwa. Bw. Huang Guorui alisema,

"Ninaona faida tunayowapatia wanakijiji ni kupanga nyumba zao. Hapo zamani hakukuwa na watu kupanga nyumba za wakulima. Baada ya wasanii kufika kwenye kijiji hicho, kijiji cha Shifo kimekuwa kijiji maarufu, watu wengi wanakwenda huko kupanga nyumba, pia biashara za mikahawa na supamaketi sasa imestawi. Hii ni hali ya juujuu tu, ninaona manufaa makubwa zaidi yanayoletwa kwa kijiji hicho ni mchango wa utamaduni na athari kwa watoto wa huko. Kwani kwa kawaida, muda wa makubaliano yaliyosainiwa na wasanii ni miaka 10, katika muda huo mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa shule ya msingi anafikia wakati wa kufanya mtihani mkuu wa kujiunga na chuo kikuu, katika kipindi hicho athari kwa mtoto pia ni kubwa, ikiwemo kuinuka kwa kiwango cha utamaduni na sanaa cha wanakijiji, ambayo ni muhimu zaidi kuliko faida ya nyumba zilizopangwa."

Idhaa ya kiswahili 2008-07-07