Viongozi wa kundi la nchi 8 zinazoendelea D-8 tarehe 8 wanafanya mkutano huko Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia, ambapo wanajadili kwa kina masuala ya uchumi yanayokumba nchi hizo. Mkuktano wa viongozi wa D-8 unafanyika kila baada ya miaka miwili. Mada ya mkutano huo ni "kufanya ushirikiano mpya kwa ajili ya kukabiliana pamoja na changamoto". Washiriki wa mkutano huo watajadili maendeleo ya kundi lenyewe, kuandaa mpango wa ushirikiano wa kiuchumi na kuanzisha ofisi ya sekretarieti na kujadili suala la kupanda kwa bei ya mafuta na chakula duniani.
Mkutano huo utajitahidi kuyafanya makubaliano ya ushuru nafuu wa forodha kati ya nchi 8 zinazoendelea yapitishwe na kutekelezwa. Waziri wa mambo ya nje wa Malaysia Bw. Rais Yatim tarehe 6 kwenye ufunguzi wa mkutano huo alisema, washiriki wa mkutano huo watajadili njia mpya ili kufikia makubaliano yenye mafanikio. Mwaka 2006 nchi wanachama wa D-8 zilimaliza mazungumzo kuhusu makubaliano ya ushuru nafuu wa forodha, lakini kutokana na maoni tofauti juu ya vifungu kwenye "kanuni kuhusu bidhaa zilizotengenezwa kwa malighafi za nchi zenyewe" makubaliano hayo hayakutekelezwa kwa sababu hayakukubaliwa zaidi na nchi nne, nchi zilizoidhinisha makubaliano hayo ni Malaysia na Iran tu. Hivi sasa maofisa wa ngazi ya juu wa biashara wamemaliza mazungumzo kuhusu bidhaa zilizotengenezwa kwa malighafi za nchi za kundi hilo na orodha ya bidhaa zenyewe, washiriki wa mkutano huo wana matumaini kuwa watakubaliana na kupitisha na kutekeleza makubaliano ili kustawisha biashara kati ya nchi hizo nane.
Aidha, mkutano huo utaandaa mpango mpya wa ushirikiano wa kuendeleza uchumi wa kila nchi mwanachama. Hivi sasa thamani ya biashara kati ya nchi hizo imeongezeka hadi kufikia dola za Marekani bilioni 49 kutoka dola za Marekani bilioni 14.5 mwaka 1999. Katika mpango wa pili wa ushirikiano wa miaka 10 utakaotangazwa thamani ya biashara itaongeza kwa 15% hadi 20% kutoka ongezeko la sasa la 5% ili kuinua maisha ya wananchi wa kila nchi mwanachama.
Mkutano huo pia utajadili namna ya kuimarisha ushirikiano ili kukabiliana kwa pamoja na changamoto inayosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta na chakula. Katika miaka ya hivi karibuni kupanda kwa bei ya mafuta na chakula kumekuwa shinikizo kubwa kwa nchi zote wanachama na kumekuwa tatizo linalotakiwa kutatuliwa haraka. Nchini Malaysia bei ya petroli na dizeli imepanda kwa 41% na 63.3%, na tarehe 25 Juni kulikuwa na maandamano makubwa kote nchini kutokana na kupanda kwa bei. Tarehe 24 Mei serikali ya Indonesia ilitangaza kupandisha bei ya mafuta, kwa wastani imepanda kwa 28.7% na kusababisha malalamiko mengi. Licha ya kupanda kwa bei ya mafuta, matatizo ya bei ya chakula na uhaba wa chakula pia yamekuwa mazito siku hadi siku. Nchi wanachama Indonesia, Bangladesh, Pakistan ambazo ni nchi zinazozalisha nafaka kwa wingi, katika miaka ya hivi karibuni zilikumbwa na maafa ya kimaumbile na ya kibinadamu, kwa kiasi kikubwa maafa hayo yameathiri uzalishaji. Kadhalika bei kubwa ya mafuta na chakula imechangia kuwepo kwa mfumuko wa bei kwa kila nchi mwanachama.
Zaidi ya hayo kwenye mkutano huo washiriki watajadili namna ya kuendeleza nishati endelevu ili kuhakikisha usalama wa nishati na namna ya kustawisha viwanda vya uzalishaji vya nchi za Kiislamu. Kwa mujibu wa maelezo, bidhaa za Kiislamu na biashara ya huduma zina mustakbali mzuri katika soko la dunia, thamani yao inatazamiwa kufikia dola za Marekani bilioni 4.23.
Kundi la Nchi 8 Zinazoendelea D-8 lilianzishwa mwaka 1997, ni jumuyia ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Bangladesh, Misri, Iran, Malaysia, Nigeria, Pakistan, India na Uturuki, lengo la kuanzishwa kwa jumuyia hiyo ni kuhimiza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Kiislamu na kuimarisha mashauriano na ushirikiano kati ya nchi wanachama kwenye mikutano ya kimataifa na kuimarisha ushirikiano katika mambo ya fedha, utalii, nishati, biashara, afya na hifadhi ya mazingira.
|