Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-09 17:55:23    
Mazungumzo ya pande sita kuaanza tena baada ya kusimama kwa miezi 9

cri

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Qin Gang tarehe 8 alitangaza kuwa, kutokana na juhudi za pande zote mazungumzo ya pande sita kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea yamepata maendeleo muhimu. Ili kusukuma mbele mazungumzo hayo, pande sita zimeamua kufanya mkutano wa siku tatu wa viongozi wa ujumbe mjini Beijing kuanzia tarehe 10 Julai. Hayo ni mazungumzo ambayo yamerejeshwa tena baada ya kusimama kwa miezi 9.

Bw. Qin Gang alisema kwenye mkutano huo, pande sita zitajadili mpango wa utekelezaji wa kipindi cha pili na masuala mengine yanayofuatiliwa pamoja. Wakati wa mkutano huo Kikundi cha kuifanya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na nyuklia na Kikundi cha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kinishati pia vitajadili mpango wa utekelezaji wa kipindi cha pili. Bw. Qin Gang alisema, mkutano huo utafanyika kwa siku ngapi na utatoa taarifa au waraka wowote, hayo ni mambo yatakayoamuliwa kwa mujibu wa hali itakavyokuwa ya mkutano wenyewe. Kuhusu mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa pande sita, Bw. Qing Gang alisema hili ni suala ambalo pande sita zitajadiliana na kushauriana.

Viongozi wa ujumbe wa Marekani, Korea Kaskazini na Korea Kusini waliwasili Beijing tarehe 8. Kiongozi wa ujumbe wa Marekani Bw. Christopher Hill na kiongozi wa ujumbe wa Korea Kaskazini Bw. Kim Kye-gwan walifanya mazungumzo siku hiyo. Bw. Hill alisema ameafikiana na Bw. Kim Kye-gwan kuhusu lengo litakalofikiwa kwenye mazungumzo hayo. Zaidi ya hayo pande mbili zilijadili suala kuhusu Marekani kutoa msaada wa chakula kwa Korea Kaskazini na kuondoa uwezo wa majengo ya nyuklia ya Korea kaskazini.

Bw. Hill alisema lengo la mkutano wa viongozi wa ujumbe wa pande sita ni kuanzisha utaratibu wa kuthibitisha ripoti iliyotolewa na Korea Kaskazini kuhusu shughuli za nyuklia ili kumaliza mapema mazungumzo ya kipindi cha pili na kuweka lengo la mazungumzo ya kipindi cha tatu. Alisema, mambo yatakayokaguliwa na kuthibitishwa ni pamoja na ripoti iliyotolewa na Korea Kaskazini, kukagua majengo ya nyuklia na kuzungumza na wataalamu husika. Bw. Hill anaona kuwa Korea Kaskazini imeelewa vilivyo utaratibu huo.

Tarehe 3 Oktoba mwaka jana waraka uliopitishwa na pande sita wa "mpango wa utekelezaji wa kipindi cha pili" unasema Korea Kaskazini inapaswa kukamilisha kazi ya kuondoa kabisa uwezo wa majengo ya nyuklia huko Yongbyon kabla ya tarehe 31 Desemba na kutoa ripoti kamili ya kihalisi kuhusu mpango wa nyuklia. Na kwa mujibu wa vitendo vya Korea Kaskazini, Marekani itaiondoa Korea Kaskazini kutoka kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi na kusimamisha utekelezaji wa "Sheria ya Biashara kwa Nchi za Kiadui" kwa Korea Kaskazini, pande husika zitaipatia Korea ya Kaskazini misaada ya kiuchumi, nishati na kibinadamu.

Lakini kutokana na migongano kati ya Marekani na Korea Kaskazini kuhusu ripoti iliyotolewa na Korea kaskazini, waraka wa "mpango wa utekelezaji wa kipindi cha pili" uliahirishwa kutekelezwa kwa nusu mwaka. Tarehe 26 Juni Korea Kaskazini iliikabidhi rasmi China, nchi mwenyekiti wa mazungumzo ya pande sita, ripoti kuhusu mpango wa nyuklia, na siku hiyo Marekani ilitangaza kuanza kutekeleza utaratibu wa kufuta jina la Koreka Kaskazini kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi na kusimamisha utekelezaji wa "Sheria ya Biashara kwa Nchi za Kiadui". Tarehe 27 Juni Korea Kaskazini ililipua mnara wa kupoza zana za nyuklia uliopo Yongbyon.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Qin Gang alisema, China ina matumaini kwamba mkutano huo wa viongozi wa ujumbe wa pande sita utapata mafanikio na kusukuma mazungumzo ya pande sita kwenye kipindi kipya. Alisema pande zote sita zinafanya juhudi ili kuyahimiza mazungumzo yaelekee kwenye lengo la kutokuwa na nyuklia kwenye peninsula ya Korea na kuifanya peninsula hiyo na Asia ya Kaskazini Mashariki iwe na amani na utulivu.