Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-11 14:51:19    
Uzuri na ugumu wa kazi ya kulinda amani nchini Sudan

cri

Kikosi cha tatu cha askari wa China kilichotumwa kwenda kutekeleza jukumu la kulinda amani huko Wau nchini Sudan kwa miezi 9, hivi karibuni kilimaliza kipindi chake na kurudi nyumbani China. Katika siku zaidi ya 200 walizokuwepo huko, zilijaa mazuri na mabaya.

Kila asubuhi tarumbeta ya kuwaamsha ilipigwa huku milio ya mbwa ikisikika. Hiyo ni sehemu wanapoishi askari, sehemu ambayo imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi kusini mwa Sudan, ambapo askari wanaeleza kuwa "vumbi la udongo mwekundu linapeperuka, magugu ni marefu kuliko kimo cha watu, nyoka na nge waonekana kila mahali, mbu na wadudu wametapakaa na kuna magonjwa ya kuambukiza." Lakini hapo ndipo mahali walipo askari 435 wa China wakiwa ni pamoja na askari wa uhandisi, uchukuzi na matibabu walijipatia sifa mbalimbali. Kamanda wa kikosi hicho Bw. Zhang Yong alisema,

"Kikosi chetu kilisifiwa na kundi la jeshi lililotumwa na Umoja wa Mataifa kutokana na kuwepo huko kwa muda mrefu zaidi, na askari waliosifiwa walikuwa wengi zaidi. Ni kikosi pekee kilichosifiwa katika Siku ya wauguzi duniani, na ni kikosi kilichosifiwa kwa kushinda hali ngumu ya uhaba wa chakula na matukio mengi ya ghafla."

Katika siku za kulinda amani huko Wau kila askari ana jambo ambalo hawezi kusahau. Jambo ambalo mkuu wa kikundi cha uchukuzi Bw. Zhang Lizhong hawezi kusahau, ni kutaja majina ya askari wake. Jambo hilo lilitokea katika safari ndefu ya kusafirisha mizigo. Kwa mujibu wa video iliyopigwa, tumeweza kupata rekodi ya sauti.

"Wu Zhicai. Ndio! Han Wei. Ndio! Qin Lizhong. Ndio!...."

Majina hayo yalitajwa kwa simu ya upepo, kwenye sehemu isiyo uwanja wa kufanyia mazoezi ya kijeshi bali ni ndani ya gari la Benz. Majina hayo yaliitwa mara moja kila baada ya robo saa. Je ni kwa sababu gani? Bw. Zhang Lizhong alisema,

"Asilimia 85% ya njia ilikuwa ni mashimo na matope, upana wa njia ulikuwa wa mita 3 tu na njiani kuna mabomu yaliyotegwa ardhini, na watu wenye silaha wasiofahamika walikuwa wanapita mara kwa mara. Safari ilikuwa ya hatari kwa kila hatua."

Kutokana na miaka mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, miundo mbinu iliharibiwa vibaya sana huko Wau kusini mwa Sudan, hali ya usalama ni mbaya sana. Kusafiri katika barabara mbaya kama hiyo kwa muda mrefu kunachosha sana, dereva anapotajwa jina lake anazinduka. Lakini si kila siku walipokuwa huko zilikuwa za hatari, kwani vilevile kulikuwa na siku za furaha. Wakati wa mapumziko, maisha ya askari wa China yalikuwa na burudani za aina nyingi. Kuwa na furaha katika hali ngumu ni tabia ya askari hao.

Hii ni sauti ya ngoma ya kiunoni walipokuwa wakishindana.

Hii ni sauti waliposhindana kuimba mashairi.

Kamanda mkuu wa kundi la jeshi lililotumwa na Umoja wa Mataifa Bw. Jasbir Singh Lidder alivutiwa sana na tabia ya askari hao ambayo wakati wa kazi ni kazi na wakati wa furaha ni furaha. Kabla ya kuondoka kazini na kurudi nyumbani alikwenda kuagana na askari hao. Alisema,

"Naona furaha kuwahudumia askari wa China kwa sababu wanaheshimu sana majukumu yao. Askari wa uhandisi na matibabu wamefanikiwa sana katika kazi zao."

Askari Feng Bing aliyekuwa huko kwa vipindi viwili alisema,

"Ni kikosi cha askari wa kulinda amani kilinishupaza na kiliniimarisha, ni kikosi hicho kilichonifundisha namna ya kupambana na matatizo. Nina bahati sana kuwepo hapa kwa vipindi viwili, naona fahari."

Katika Siku ya kina mama Duniani, mwuguzi Bi. Wang Xia alipata simu ya pongezi kutoka kwa binti yake aliyekuwa nchini China. Kwenye simu hakusahau kumwambia binti yake mambo aliyojifunza nchini Sudan.

Binti: Mama, leo ni siku ya kina mama duniani, kwa sababu haupo nyumbani siwezi kukufanyia lolote ila nakupongeza kwa kuadhimisha siku hiyo.

Mama: Nashukuru binti yangu, nafurahi, niko salama. Nimeona watoto wengi hapa wanashindwa kwenda shule, unatakiwa uthamini mazingira yako kusoma.

Binti: Ndio.

Mtu aliyeshuhudia ukatili wa vita ndiye anayethamini sana hali ya usalama. Kikosi cha nne cha askari wa kulinda amani kitafunga safari ya kwenda huko Wau. Mambo yote waliyopata askari hao yatakuwa mapya kwa askari wa kikosi cha nne ikiwa pamoja na sauti ya tarumbeta ya kuamka na milio ya mbwa.

Idhaa ya kiswahili 2008-07-11