Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-10 12:22:29    
Ndoto ya msichana wa China kuhusu michezo ya Olimpiki

cri

Wakati michezo ya Olimpiki ya Beijing inapokaribia, watu wa China wanazidi kuonesha uchangamfu mkubwa kuhusu michezo hiyo. Katika kipindi cha leo tutasikia maelezo ya msichana wa China akieleza ndoto yake kuhusu michezo ya Olimpiki.

"Hamjambo. Mimi ninaitwa Chen Yanhong, natoka shule ya sekondari ya Bayi ya Beijing. Nina umri wa miaka 14. Ninavutiwa na mambo mbalimbali, hivi sasa pia ninafanya utangazaji katika kipindi cha watoto cha kituo cha televisheni cha taifa la China, mimi ni mwandishi wa habari chipukizi. Ninaitakia mafanikio michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, napenda watu wengi zaidi wafuatilie michezo hiyo na kushiriki kwenye michezo hiyo, nina matumaini kuwa kila mtu atatoa mchango wake ili dunia yetu iwe nzuri zaidi."

Msichana Chen Yanhong ana vipaji vya aina mbalimbali. Akiwa mwandishi wa habari mdogo zaidi, aliwahi kukusanya habari za shughuli muhimu za kisiasa za China, aliwahi kufanya mahojiano na rais Hu Jintao wa China na kujenga urafiki na balozi wa Marekani nchini China kwenye mahojiano. Katika kipindi cha miaka 6 alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi, mbali na kumaliza masomo, alipata mafunzo kuhusu muziki, dansi na filamu. Yeye ni hodari katika kuimba, kucheza dansi, pia aliwahi kushiriki kwenye filamu na michezo ya kuigiza ya televisheni, na hivi sasa ni mtangazaji kwenye kituo cha televisheni. Pamoja na kupata mafanikio hayo yote, Chen Yanhong hana majivuno. Baba yake Bw. Chen Longshi alisema, yeye na mke wake wanapenda binti yao aweze kukua kwa afya njema kiroho na kimwili.

Alisema  "Tunazingatia kumtunza katika mambo matatu, la kwanza ni matendo yake, la pili ni uwezo wa kuwasiliana na wengine na la tatu ni uwezo wa kazi. Watoto wanapaswa kuelimishwa uwezo huo na jamii, shule na familia kwa pamoja, tunazingatia sana kumfundisha vitu visivyofundishwa shuleni. Tumemfanya apate mafunzo mbalimbali ya kuinua uwezo wake."

Hivi sasa katika kufanya mahojiano, Chen Yanhong anaonekana kuwa na uwezo wa uandishi wa habari, hata hivyo alisema alikuwa na wasiwasi mkubwa alipofanya uandishi wa habari kwa mara ya kwanza. Alikumbusha akisema  "Nilikuwa na wasiwasi sana, moyo ulidunda kwa haraka kama ngoma inavyopigwa. Lakini baada ya kuanza kazi, niliona kuwa watu waliohojiwa ni wapole sana kwani mimi ni mtoto, kwa hiyo hisia za woga zilitoweka. Mimi ni hodari katika matumizi ya lugha, kwa hiyo muda uliopangwa wa mahojiano ulikuwa dakika 15 tu, lakini tulikuwa tunazungumza kwa furaha na mahojiano yalifanyika kwa zaidi ya saa moja."

Baada ya kufanya mahojiano kwa mara nyingi, msichana huyo amepata uzoefu mwingi na kuzoea kufuatilia habari mbalimbali na matukio muhimu, ikiwemo michezo ya Olimpiki itakayofunguliwa hapa Bejing. Alieleza kuwa aliwahi kufanya mahojiano na Bw. Wang Sheng'an, ambaye alikuwa kwenye ujumbe wa Beijing wa kugombea nafasi ya kuandaa michezo ya Olimpiki. Msichana Chen Yanhong alisema "Ili kupata nafasi ya kuandaa michezo ya Olimpiki, Bw. Wang Sheng'an hakujali maslahi yake binafsi. Niliguswa sana hisia zangu. Kwenye mahojiano, aliponijibu maswali, alikuwa anaongea kwa uchangamfu, kiasi kwamba niliweza kuhisi kuwa ana nia kubwa ya kuchangia taifa na michezo ya Olimpiki."

Hapo baadaye msichana Chen Yanhong alianza kufuatilia ujuzi kuhusu michezo ya Olimpiki, na habari kuhusu maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing. Na ndoto moja ikamjia kwamba anataka kutoa mwaliko kwa walimwengu kwa niaba ya wanafunzi wa shule za sekondari wa China. Baada ya kufanya uchunguzi alifahamishwa kuwa, wachezaji 649 walipata medali za dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka 2004 iliyofanyika mjini Athens, Ugiriki. Kwa hiyo aliamua kutuma barua za mwaliko kwa mabalozi 54 wa nchi na sehemu hizo wanakotoka washindi wa medali za dhahabu, pamoja na wenyeviti watatu wa kamati ya Olimpiki ya kimataifa. Kutokana na msaada wa walimu na wazazi wake, baada ya maandalizi ya miezi miwili, barua hizo za mwaliko pamoja na matarajio ya msichana huyo kuhusu michezo ya Olimpiki zilitumwa kwa mabalozi mbalimbali.

Hadi sasa Chen Yanhong amepata barua za majibu kutoka kwa ubalozi wa nchi kadhaa zikiwemo Ujerumani na Kenya nchini China, pia ubalozi wa Ethiopia na Marekani uilimpigia simu kumjibu. Hivi sasa msichana huyo bado anaendelea kupokea salamu kutoka kwenye ubalozi wa nchi mbalimbali.

Kuhusu michezo ya Olimpiki itakayofunguliwa mwezi Agosti mwaka huu, alieleza matarajio yake, akisema  "Kila mtu anatakiwa kutoa mchango kwa michezo ya Olimpiki ya Beijing. Tuna dunia moja na ndoto moja. Naamini kuwa kuna shughuli nyingi ambazo tunaweza kuchangia. Kwa hiyo nakuomba utoe mchango kwa michezo ya Olimpiki kwa kutumia mikono yako, ili michezo hiyo ya mwaka 2008 ifanyike kwa mafanikio na dunia yetu iwe nzuri zaidi."

Idhaa ya kiswahili 2008-07-10