Umoja wa Mediterranean umeanzishwa kwenye mkutano wa wakuu wa kanda ya bahari ya Mediterranean uliofanyika tarehe 13 huko Paris. Wachambuzi wanaona kuwa, umoja huo umeanzishwa baada ya pande mbalimbali kufanya mazungumzo kwa muda mrefu na kutoa maamuzi ya kurudi nyuma, lakini umoja huo bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na hali ya utatanishi katika kanda ya bahari ya Mediterranean.
Kanda hiyo ni chimbuko la dini ya Kikristo na dini ya Kiislamu. Umoja wa Ulaya na baadhi ya nchi za bahari ya Mediterranean zina maoni tofauti kubwa katika mambo ya siasa, uchumi, utamaduni, itifaki na dini, aidha nchi mbalimbali zina maslahi tofauti na zinafuatilia masuala tofauti. Kwa mfano nchi za Umoja wa Ulaya zinafuatilia zaidi mapambano dhidi ya ugaidi na suala la wahamiaji haramu, huku nchi zilizoko kando ya kusini ya bahari ya Mediterranean ambazo ziko nyuma kimaendeleo kuliko nchi za Ulaya, zinafuatilia zaidi namna ya kupata maendeleo ya kiuchumi kwa kutumia nguvu ya umoja huo.
Pamoja na kuhimiza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za kanda ya bahari ya Mediterranean, rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa pia ameeleza nia ya kuhimiza mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati kwa kupitia Umoja wa Mediterranean, ili Ufaransa na Umoja wa Ulaya ziweze kuchukua sehemu ya kazi za Marekani katika kutatua suala la Mashariki ya Kati, hatua ambayo pia itaweza kuinua sifa ya Ufaransa ulimwenguni ambayo sasa inashuka siku hadi siku. Rais Sarkozy alipohutubia mkutano wa Umoja wa Ulaya, alisema hadi hivi sasa Umoja wa Ulaya ulikuwa umetoa misaada mingi ya kiuchumi kwa ajili ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, lakini umoja huo haujaweza kupata umuhimu mkubwa wa kisiasa unaolingana na ule wa Marekani. Ndiyo maana rais Sarkozy akitumia fursa ya mkutano huo wa wakuu wa nchi za kanda ya bahari ya Mediterranean, alikutana na watu kadhaa muhimu wanaoweza kutoa mchango mkubwa ili kusukuma mbele utatuzi wa suala la Mashariki ya Kati. Hata hivyo wachambuzi wameeleza kuwa, haiwezekani kwa Umoja wa Mediterranean kuonesha nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya muda mfupi katika mchakato wa mazungumzo kati ya Palestina na Israel.
Mbali na hayo Algeria, Libya, Sudan na sehemu ya Ghuba ya Guinea ni sehemu muhimu zinazozalisha mafuta duniani. Katika miaka ya hivi karibuni, nchi kubwa zikiwemo Marekani na Russia zimekuwa zikitumia mbinu mbalimbali ili kuimarisha nguvu za ushawishi katika sehemu hizo. Ndiyo maana kuanzishwa kwa Umoja wa Mediterranean hakika kutaleta ushindani mkali zaidi kati ya pande mbalimbali katika kanda hiyo.
Aidha baadhi ya nchi zilizoko kando ya kusini ya bahari ya Mediterranean zinaona kuwa umoja huo ulianzishwa kwa ajili ya maslahi ya Ufaransa, ambayo inalenga kuimarisha nguvu yake ya ushawishi katika kanda ya Afrika Kaskazini na kutumia umoja huo ili kupata nguvu kubwa zaidi katika mambo ya kimataifa.
Zaidi ya hayo mpango wa kuanzisha Umoja wa Mediterranean ulipingwa na nchi mbalimbali, ambapo Ujerumani ilikuwa ni mpinzani mkubwa zaidi, kwani kutokana na mpango wa awali wa rais Sarkozy, Umoja wa Mediterranean utawashirikisha nchi wanachama kutoka nchi zilizoko kando za bahari ya Mediterranean tu, hii ilionesha kuwa nchi muhimu za Umoja wa Ulaya, ikiwemo Ujerumani hazitaweza kuwa wanachama wa umoja huo. Ujerumani ilipinga hadharani kuanzishwa kwa umoja huo, ikisema hatua hiyo itaweza kusababisha mfarakano kwa Umoja wa Ulaya. Nchi nyingine za Umoja wa Mataifa zikiwemo Uingereza, Austria, Poland, Finland na nchi za Ulaya Kaskazini pia zilionesha kuwa na wasiwasi huo.
Kutokana na sababu zilizotajwa hapo awali, suala linalofuatiliwa ulimwenguni ni kama nchi wanachama wa umoja huo zitaweza kuwa na mshikamano na kutekeleza kihalisi shughuli za umoja huo au la.
|