Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-15 17:09:49    
Maendeleo makubwa ya shughuli za utengenezaji wa soksi mjini Datang

cri

Mji mdogo wa Datang haujulikani kwa watu wengi, lakini unajulikana kwa wanaviwanda kutokana na shughuli zake za soksi. Shughuli kamili za kutengeneza malighafi mbalimbali na soksi na kuuza soksi zimeanzishwa huko. Baada ya kusitawisha shughuli hizo kwa miaka 20 iliyopita, watu wengi zaidi wa mji huo wametambua kuwa, mji huo hauwezi kuwa kituo muhimu cha soksi duniani kwa kuongeza utengenezaji wa soksi tu, bali ni lazima wafanye uvumbuzi ili bidhaa zao ziingie kwenye masoko ya kimataifa. Kwenye kipindi hiki cha nchi yetu mbioni, tunawaelezea jinsi uvumbuzi unavyohimiza maendeleo mapya ya uchumi wa mji huo.

Mji mdogo wa Datang uko mjini Zhuji mkoani Zhejiang. Shughuli za utengenezaji wa soksi zimeufanya mji huo mdogo ambao zamani ulikuwa na wakazi zaidi ya elfu 1 kuwa mji wenye wakazi zaidi ya elfu 60 ambao unatengeneza jiozi bilioni 8 za soksi kwa mwaka. Mkuu wa mji mdogo wa Datang Bw. Guo Jianbo alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kati ya jozi kumi za soksi duniani, jozi tatu zilitengenezwa mjini humo, alisema,

"Mji wetu una sifa tatu. Kwaza, mji wetu ni mji mdogo maarufu, pili shughuli zetu zimekuwa soko kubwa, tatu mamia na maelfu ya familia hapa zote ni karakana za utengenezaji wa soksi."

Shughuli za utengenezaji wa soksi mjini Datang ni mfano wa uchumi wenye sifa ya kipekee mkoani Zhejiang. Hivi sasa shughuli hizo zimeanzishwa kwenye miji midogo 12 kando ya mji mdogo wa Datang, na zimeshirikiwa na watu zaidi ya laki 1 wanashiriki kwenye shughuli hizo. Eneo hilo linasifiwa kuwa ni eneo maalumu la utengenezaji wa soksi la Datang. Kwa mujibu wa takwimu, mwaka 2006 eneo hilo lilikuwa na mashine laki 1 za kutengeneza soksi, lilizalisha jozi bilioni 11.8 za soksi kwa mwaka, na thamani ya utengenezaji ilikuwa karibu yuan bilioni 28.

Lakini wakazi wa Datang hawajatosheka na maendeleo hayo. Wameanza kufikiria kuingia kwenye soko la kimataifa. Bw. Guo Jianbo alisema,

"Siku zote tunafikiria maendeleo ya shughuli hizo. Kwa mujibu wa hali halisi ya mji wa Datang, tumetoa mpango wa kuendeleza uchumi wa makao makuu ya utengenezaji wa soksi, na kujenga kituo cha utafiti wa utengenezaji wa soksi hapa. Ili kutimiza mpango huo, mwaka huu tumeanzisha mfumo wa huduma za umma kuhusu utengenezaji wa soksi."

Mfumo huo wa huduma za umma umejengwa kwa gharama ya yuan milioni 20, ambao ni pamoja na idara ya utafiti wa soksi, kituo cha upimaji wa sifa ya bidhaa, kituo cha biashara ya elektroniki, kituo cha kutoa idhini, tovuti ya shughuli za utengenezaji wa soksi ya Datang na mfumo wa habari za viwanda vya Datang kupitia mtandao wa Internet.

Habari zinasema idara ya utafiti wa soksi inabuni mitindo 1000 ya soki kwa siku, na kila siku watu zaidi ya mia 5 wanakwenda kwenye mji huo kutafuta mitindo mipya ya soksi. Hivi sasa idara hiyo imebuni mitindo milioni kadhaa ya soksi. Licha ya hayo, ni rahisi kubuni mitindo mpya ya soksi kwenye idara hiyo, na watu wanaweza kubuni mitindo mipya ya soki kwa kutumia sekunde 10 tu ambao muda mfupi zaidi. Idara hiyo imeyasaidia makampuni ya huko kutengeneza soksi zinazokidhi mahitaji ya soko.

Baada ya mfumo huo wa huduma za umma kuanza kufanya kazi rasmi mwezi Septemba mwaka jana, umesifiwa na makampuni mengi yanayotengeneza soksi. Kwa mujibu wa takwimu za mwanzo, mfumo huo unaweza kuyasaidia makampuni yabane matumizi ya fedha karibu yuan milioni 2 kwa mwaka, na kuongeza uagizaji wa bidhaa wenye thamani ya yuan bilioni 2.

Licha ya hayo, ili kuyahimiza makampuni kuanzisha chapa maarufu, serikali ya huko imetunga sera husika. Makampuni yanayopata chapa maarufu ya ngazi ya kitaifa yatapewa yuan laki 5, na makampuni yanayopata chapa maarufu ya ngazi ya mkoa yatapewa yuan laki 2. Bw. Guo Jianbo alisema,

"Kufanya uvumbuzi wa kiteknolojia ni jambo la muhimu zaidi kwa makampuni na shughuli za utengenezaji wa soksi hapa Datang. Licha ya kuanzisha mfumo wa huduma za umma, tumetenga fedha maalum ili kutoa tuzo kwa makampuni ambayo yanafanya uvumbuzi wa kiteknolojia na kuomba hakimiliki ya ubunifu. Hatua hizo zimehimiza juhudi za kuongeza thamani ya nyongeza ya utengenezaji wa soksi na maendeleo ya uchumi wa hapa."

Kampuni ya Danjiya ni kampuni iliyotenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya utafiti wa kisayansi huko Datang. Mwaka 2003 kampuni hiyo ilianzisha taasisi ya utafiti na kituo cha huduma kuhusu uvumbuzi wa kiteknoljia. Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. Zhu Tianyong alisema,

"Kampuni yetu inashirikiana na Chuo Kikuu cha Donghua na Chuo cha uhandisi cha Zhejiang. Hadi hivi sasa matokeo matatu ya utafiti wa kisayansi na kiteknolojia yametumiwa katika kutengeneza bidhaa. Na matokeo ya utafiti mmoja yamepewa tuzo ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya ngazi ya kitaifa na mkoa. Bidhaa zinazotengenezwa kwa kutumia teknolojia hizo ni pamoja na soksi zinazotengenezwa kwa nyuzi za mianzi na nyuzi za maharagwe na soksi zinazozuia vijijidudu na harufu mbaya. Teknolojia za kutengeneza bidhaa hizo ni za kisasa duniani."

Kampuni ya Spandex ya Huahai ni moja kati ya makampuni mawili ya teknolojia mpya za hali ya juu mjini Datang. Naibu meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Du Chunshu alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa spandex ni nyuzi nzuri za kikemikali ambazo ni vigumu kuzitengeneza. Katika miaka mingi iliyopita, kampuni hiyo imekuwa inashughulikia utafiti wa nyuzi hizo, alisema,

"Kampuni yetu ina kituo cha utafiti wa kisayansi, ambacho kinafanya uvumbuzi na majaribio kwa mujibu wa mahitaji ya soko. Tuna vifaa vidogo vya majaribio."

Kuna makampuni mengi yanayotilia maanani utafiti wa kisayansi na uvumbuzi kwa kujitegemea kama kampuni ya Danjiya na Huahai huko Datang. Bw. Guo Jianbo alisema,

"Ni lazima makampuni yafanye uvumbuzi kwa makini, ama sivyo thamani ya nyongeza ya bidhaa zao haitaongezeka, na bidhaa hizo hazitatengenezwa kwa muda mrefu."

Hivi sasa mfumo kamili wa uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia wa utengenezaji wa soksi umeanzishwa huko Datang. Kufanya uvumbuzi kwa kujitegemea kumehimiza maendeleo mapya ya utengenezaji wa soksi, na chapa ya soksi ya Datang imekuwa maarufu zaidi kwenye soko la kimataifa.