Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-17 20:38:22    
Kwaya ya Kenya "Kayamba Africa" itakuja China

cri

Mwishoni mwa mwezi Julai makundi saba ya nyimbo na ngoma kutoka Afrika yataonesha michezo yao yenye jina la "Usiku wa Afrika" kwenye Jumba la mikutano ya Umma la Beijing yakichangia shamrashamra za Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Moja ya makundi hayo ni kwaya ya Kenya "Kayamba Afrika". 

Mliosikia ni wimbo wa kabila la Wamasai nchini Kenya wa kufurahia mavuno mazuri. Wanakwaya wa Kayamba Afrika wanafanya mazoezi ya wimbo huo wakijiandaa kufanya maonesho ya michezo ya sanaa mjini Beijing. Kati ya wanakwaya, wengi hawakuwahi kuja China, wanaona furaha kubwa kwa kuwa watakuja wakati Michezo ya Olimpiki inapokaribia kufanyika. Kiongozi wa kwaya Bw. Juma Odemba alisema,

"Tunaona furaha kubwa kwenda China wakati Michezo ya Olimpiki ya Beijing inapokaribia, hii inaonesha kwamba China iko wazi kwa nchi za nje. Kwaya yetu ni jumuyia ya umma, nia yetu ni kutetea haki sawa kwa watu wote bila kujali tofauti za rangi ya ngozi, makabila, lugha, mila na desturi, sote tuishi kwa amani, tufunzane na tusonge mbele kwa pamoja. Kwa hiyo wakati tunapotangaza utamaduni wa Kenya pia tutafahamu China na watu wa China."

Kwaya ya Kayamba Africa ilianzishwa mwaka 1998. Neno "kayamba" ni aina moja ya ala za muziki inayotumika sana miongoni mwa watu wa makabila mbalimbali nchini Kenya. Kutokana na kuchanganya mitindo ya muziki wa makabila mengi ya nchini Kenya na sanaa ya kisasa, muziki wa kwaya hiyo umekuwa muziki unaopendwa sana nchini Kenya na hata kwenye bara zima la Afrika. Mwaka 2001 kwaya hiyo ilichukua nafasi ya tano kati ya makundi yote ya muziki barani Afrika, na mwaka 2004 ilipata tuzo kubwa ya "Kisima" ya Kenya.

Kwaya hiyo ina matumaini ya kwamba kwa kufanya juhudi itaweza kueneza muziki wa Afrika kwenye dunia nzima. Licha ya hayo, cha muhimu zaidi ni kwamba kwa kutumia fursa ya kuonesha michezo yake inaweza kuchangia heri kwa Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Kiongozi wa kwaya hiyo Bw. Juma Odemba alisema, wanataka kuimba nyimbo kwa kutoa mkono wa pole kwa nyimbo zao kwa watu walioathirika katika maafa ya tetemeko la ardhi mkoani Sichuan. Alisema,

"Tulikuwa na masikitiko makubwa tuliposikia tetemeko kubwa la ardhi lilipotokea nchini China. Kwa huzuni kubwa tunawaomboleza watu waliokufa kwa sababu wangekuwa hai wangeweza kusikia nyimbo zetu na kuburudika na utamaduni wa Afrika. Pamoja na hayo pia tunatoa mkono wa pole kwa watu walioathirika na maafa hayo. Hapa ningependa kusema kwa marafiki wa China kwamba vyovyote itakavyotokea watu wa Afrika daima watakuwa pamoja nanyi."

Katika kwaya hiyo, wanakwaya sita wanatoka makabila tofauti nchini Kenya, wanaweza kuimba kwa lugha zaidi ya 20 za kikabila. Kwenye maonesho yao mjini Beijing pia wataimba nyimbo za China kwa lugha ya Kichina ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Kenya na China. Bw. Juma Odemba alisema hapo kabla hawakuwa na ujuzi wowote wa lugha ya Kichina, kwa ajili ya kuimba nyimbo za China Mama balozi wa China nchini Kenya aliwafundisha maneno ya nyimbo na namna ya kutamka maneno hayo, na wao wenyewe pia wanajitahidi sana kujifunza, mara kwa mara wanasikiliza mkanda wa nyimbo hizo kila walipopata nafasi.

Bw. Juma Odemba alisema wimbo huu unafahamika sana nchini China, na muziki wake ni mtamu, wanaimba wimbo huo kwa kuonesha urafiki wao na watu wa China.

"Tunapoimba wimbo wa 'Mimi bado ni Mchina Moyoni Mwangu' tunaungana na Wachina kwa moyo. Tunawakumbuka watu waliokufa katika maafa ya tetemeko la ardhi kwa sababu tunaelewa kwamba tukiwa pamoja nao katika furaha na uchungu tumekuwa marafiki wao wa dhiki na faraja. Hii ndio nguvu ya muziki."