Tarehe 16 serikali ya Marekani ilitangaza kuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Williams Burns anayeshughulikia mambo ya siasa atahudhuria mazungumzo ya mwanzo ya suala la nyuklia yatakayofanyika tarehe 19 huko Geneva kati ya mjumbe mwandamizi wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya kidiplomasia na usalama Bw. Solana na mwakilishi mkuu wa Iran kwenye mazungumzo ya suala la nyuklia Bw. Saeed Jalili. Hii inadhihirisha kwamba Marekani imelegeza msimamo wake katika suala la nyuklia la Iran.
Tokea mwaka 1980 uhusiano wa kibalozi kati ya Marekani na Iran ulipokatishwa hadi sasa, uhusiano kati ya nchi hizo mbili bado haujawa wa kawaida. Mwaka 2002 Rais George Bush wa Marekani aliiweka Iran kwenye orodha ya "nchi ovu" duniani na kusisitiza kwamba Marekani haitafanya mazungumzo na Iran moja kwa moja kabla ya Iran haijasimamisha shughuli za kusafisha uranium, na haitaondoa uwezekano wa kutumia nguvu dhidi ya Iran. Lakini sasa kwa ghafla Marekani imetangaza kutuma kiongozi mwenye nafasi ya tatu katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani Bw. Williams Burns kuhudhuria mazungumzo hayo, na kwa kusaidiwa na waziri wa mambo ya nje Bw. Williams Burns ameanza kughuhulika na mambo ya kuanzisha ofisi ya mawasiliano ya kidiplomasia nchini Iran. Bw. Williams Burns atakutana na Bw. Saeed Jalili, huu ni mkutano wa ngazi ya juu wa nchi hizo mbili katika muda wa miaka 30 iliyopita. Na kuanzishwa kwa ofisi hiyo pia ni mara ya kwanza kwa Marekani kutuma wanadiplomasi nchini Iran katika muda wa miaka 30 iliyopita.
Mabadiliko ya sera za Marekani sio tu yanaonekana kwenye mkutano wa maofisa waandamizi wa pande mbili, tena wiki kadhaa zilizopita Ikulu ya Marekani ilitangaza sera za kutoa kipaumbele kwa Iran ikiwa ni pamoja na kuahidi kutotumia nguvu kutatua suala la nyuklia la Iran, kujadiliana na Iran kwa kina suala hilo, kuunga mkono Iran itoe mchango muhimu katika mambo ya kimataifa. Pamoja na hayo Marekani inaunga mkono Umoja wa Ulaya ifanye mazungumzo na Iran na kuiarifu Israel isichukue hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran kwa upande mmoja. Isitoshe, Marekani imetangaza kuwa inaunga mkono mpango uliotolewa na Bw. Solaya wa "kusimamisha kwa kusimamisha", yaani katika muda wa wiki sita wa mazungumzo ya hatua ya mwanzo, Marekani pamoja na nchi washirika zitasimamisha kuongeza vikwazo dhidi ya Iran, na Iran itasimamisha kupanua mpango wake wa nyuklia. Kama Iran itasimamisha kabisa mradi wake wa nyuklia, pande mbili zitaanza mazungumzo rasmi.
Ofisa wa Marekani amesisitiza kuwa mabadiliko hayo ya sera yanatokana na hali ambayo Marekani imeona athari ya vikwazo vilivyochukuliwa na jumuyia ya kimataifa, na sera za Iran kuhusu Marekani pia zimebadilika, na katika masuala kadhaa imechukua msimamo wa kufikia maafikiano. Zaidi ya hayo Ikulu ya Marekani imetambua kwamba ni lazima irekebishe sera zake dhidi ya Iran na imeanza kusisitiza umuhimu wa juhudi za kidiplomasia. Katika miaka kadhaa iliyopita Marekani ilikwepa kuwasiliana moja kwa moja na Iran na kuzikabidhi nchi washirika wake za Ulaya kazi ya kufanya mazungumzo na Iran. Lakini hata hivyo, Marekani ilikuwa na matumaini kuwa Iran ingeweza kusikia kauli ya Marekani moja kwa moja. Marekani inaona kuwa mazungumzo ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama na mazungumzo kati ya Ujerumani na Iran hayawezi kupata mafanikio yoyote kutokana na maslahi yanayong'ang'niwa na kila nchi, Marekani ina matumaini kuwa kushiriki kwenye mazungumzo ya Geneva kunaweza kuzuia mazungumzo yasiachane na "njia sahihi" inayotarajiwa na Marekani.
Lakini vyovyote itakavyokuwa, hatua zilizochukuliwa na Marekani hivi karibuni zimeonesha kuwa serikali ya Rais George Bush imeweka kando mpango wake wa kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran, na msimamo huo kwa kiasi kikubwa umeondoa wasiwasi wa jumuyia ya kimataifa inayohofia Marekani na Israel kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran. Kwa sababu Iran ni nchi inayozalisha mafuta kwa wingi, kuondoa wasiwasi kutasaidia kuzuia bei ya mafuta kuendelea kupanda juu .
|