Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-21 18:40:09    
Hekalu la Tathagata la mkoa wa Tibet

cri

China ni nchi yenye aina nyingi za dini zikiwa ni pamoja na dini za Kidao, Kibudha, Kiislam na Kikristo, hivyo kuna majengo mengi ya kidini kwenye sehemu mbalimbali za China. Majengo ya kila aina ya dini yana umaalumu wake, pamoja na mambo mengi ya kiutamaduni na kihistoria. Katika kipindi hiki cha leo, tutawaelezea hekalu la kale la Tathagata, ambalo ni hekalu la dini ya kibuddha. Tathagata ni sauti ya matamshi ya maneno ya lugha ya Kitibet. Mwongoza watalii Bw Jiangyong Badeng alieleza maana ya neno hilo, akisema,

"Maana ya Tathagata ni kuwa, kutoka mbali hekalu hilo linaonekana ni kama rundo kubwa la mchele."

Hekalu la Tathagata lilijengwa kwenye mtelemko wa mlima, umbo lake ni kama pembe tatu, sehemu ya juu ni ndogo na sehemu yake ya chini ni kubwa, jinsi lilivyo ni kama lundo la mchele, kwa hiyo hekalu hilo lilipewa jina la lundo la mchele.

Hekalu la Tathagata ni moja ya mahekalu 6 makubwa ya dhehebu la Gelu la dini ya kibudha ya kitibet, vilevile ni hekalu linalochukua nafasi ya kwanza kwa ukubwa duniani. Hekalu hilo lilijengwa pamoja na majumba ya mfalme mwaka 1416. Hekalu la Tathagata lilijengwa kwenye mtelemko wa mlima, eneo lake ni mita za mraba laki 2, ndani ya hekalu hilo kuna vyuo 7 vya kufundisha elimu ya jadi. Mwongoza watalii Bw. Jangyong Badeng alisema,

"Hekalu hilo lilijengwa na mwalimu mkuu Zonggeba pamoja na wanafunzi wake, katika wakati ule hekalu hilo lilikuwa na watawa zaidi ya elfu 10. Hivi sasa idadi ya watawa wa hekalu hilo ni kiasi cha 800 hivi."

Hekalu la Tathagata halikujengewa uzio, lakini majengo yake yalijengwa kwa utaratibu mzuri, mlango mkubwa wa hekalu uko kwenye sehemu ya chini, majengo yake yanaelekea sehemu ya juu kama ngazi. Bw. Jangyong Badeng alisema

"Hapa ni mahali pa kusoma vitabu vya dini kwa watawa hapo zamani, sasa tuna vyuo 4. "

Vyuo ni sehemu moja isiyokosekana katika dini ya kibudha ya kitibet, kati ya vyuo vya hekalu kuna chuo kikuu chake, ambacho kiko kwenye sehemu ya kati ya hekalu la Tathagata, eneo la chuo kikuu hicho ni kiasi cha mita za mraba 4,500, mbele ya chuo kikuu hicho kuna kiwanja kilichotandikwa kwa vipande vya mawe, mtu akitaka kuingia kwenye chuo kikuu hicho anapanda ngazi saba kwanza. Kumbi mbili za kutoa mihadhara ni kubwa na kupambwa kwa ufahari, kumbi hizo zina nguzo 183, na eneo lake ni kiasi cha mita za mraba 1,800. Wakati wa kusoma vitabu vya dini, watawa mia kadhaa wanaketi chini ya nguzo hizo.

Majengo ya mahekalu yenye mtindo wa kitibet kama hekalu la Tathagata, yanaweza kugawanyika katika aina mbili, aina ya kwanza ni yenye majengo makubwa ya kifahari, kama kumbi za chuo kikuu cha hekalu la Tathagata. Aina nyingine ya majengo yake ni makazi ya watawa, ambayo yanafanana na nyumba za wakazi wa kawaida. Nyumba hizo zenye ua zilijengwa pia kwenye mtelemko wa mlima, nyumba hizo ni zenye mtindo tofauti kabisa na nyumba wa watu wa kabila la Wahan. Nyumba hizo zenye kuta zilizojengwa kwa vipande vya mawe na kupakwa rangi nyeupe, sehemu ya juu ya nyumba hizo ni ndogo na sehemu yake ya chini ni kubwa. Maua yaliyowekwa kwenye madirisha ya nyumba yanaongeza furaha ya maisha. Wageni wanaweza kuongea na watawa wakati wakirudi katika makazi yao.

Katika chuo kikuu cha hekalu la Tathagata kuna jiko kubwa linalochukua nafasi ya kwanza kwa ukubwa mkoani Tibet. Hekalu la Tathagata katika wakati fulani lilikuwa na watawa zaidi ya elfu 10, hebu tufikirie sufuria ya kupikia chakula cha idadi kubwa ya watawa ingekuwa kubwa kiasi gani. Bw. Jangyong Badeng alisema

"Huu ni ubao wa kukatia mboga, unahitaji kubebwa na watu wanne au watano hivi, hii ni sufuria kubwa ya kupikia chakula cha watawa 10, 500, katika hekalu la Tathagata kuna sufuria kubwa 5. Sufuria hizo bado zinatumika. Sufuria moja ina uwezo wa kupika wali kwa kutumia kilo 150 za mchele, watawa wakipika wali kwa sufuria hizo 5, wanatumia kilo 500 za mchele".

Kama ukiingia kwenye hekalu la Tathagata kwa kupanda ngazi kwenye upande wa magharibi, baada ya kupita mlango mkuu kuna njia moja nyembamba kwenye upande wa kushoto, kando ya njia hiyo kuna kimfereji kidogo. Baada ya kufika kwenye kiwanja kidogo kilichoko mlimani, watu wanaweza kuona mandhari nzuri ya bondeni. Watu wakiendelea kupanda juu, kwenye upande wa kushoto kuna michoro ya Buddha kwenye jiwe kubwa, na nyuma yake kuna fremu za chuma zilizojengwa kwa ajili ya kuanika picha ya Buddha katika siku ya Xuedun. Kila ikifika alasiri ya siku hiyo, watawa wa hekalu la Tathagata hutoa picha kubwa ajabu ya Sakyamuni kwenye mtelemko wa mlima ili iabudiwe na watu. Katika siku hiyo, mwangaza wa jua lililokuwa likichomoza huangaza picha ya Buddha kutoka kwenye kichwa cha Buddha hadi kwenye miguu yake, kadiri picha ya Buddha inavyokunjuliwa. Bw. Jiangyong Badeng alisema,

"Tangka, yaani picha ya Buddha, ina urefu wa zaidi ya mita 20, picha hiyo inakunjwa na kuwekwa ndani ya kabati kubwa. Tangka iliyo kubwa kabisa kwenye mkoa wa Tibet ni tangka ya hekalu la Tathagata."

Hivi sasa, picha hiyo kubwa ya Sakyamuni iliyotarizwa imehifadhiwa vizuri kwenye hekalu la Tathagata kama kitu chenye thamani kubwa. Watu hawawezi kuiona tangka hiyo ila tu katika siku ya Xuedun. Licha ya picha kubwa ya Sakyamuni, hekalu la Tathagata limehifadhi vitu vingine vya kiutamaduni zaidi ya elfu 10. Vitu hivyo vina thamani kubwa kwa utafiti wa historia, dini na sanaa za Tibet.