Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-22 17:03:47    
Kilimo cha mzunguko mkoani Qinghai chabadilisha maisha ya wakulima

cri

Kupanda mazao ya kilimo kwenye mabanda ni jambo la kawaida katika vijiji vingi nchini China. Lakini hilo si jambo rahisi kwa wakazi wa sehemu zilizoko nyuma kiuchumi kwenye uwanda wa juu.

Uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet ni uwanda wenye mwinuko mkubwa zaidi kutoka usawa wa bahari duniani, ambao unasifiwa kuwa ni "paa la dunia". Mkoa wa Qinghai uko kwenye uwanda huo, ambao wastani wa urefu kutoka usawa wa bahari wa mkoa huo ni zaidi ya mita elfu 3. Hali ya hewa ya huko ni ya baridi na unyevu, mazao ya kilimo yanaweza kukua kwa muda mfupi tu kila mwaka, tena kuna aina chache za mazao, na maafa ya kimaumbile yanatokea mara kwa mara, hivyo mazao ya biashara yanayoweza kuleta thamani kubwa ya nyongeza hayawezi kupandwa kwenye sehemu hizo, na kuwasaidia wakulima kuongeza mapato siku zote ni kazi ngumu kwa serikali ya huko. Zamani njia muhimu ya kuwasaidia wakazi wa wilaya zilizoko nyuma kiuchumi ilikuwa ni kuwapatia ruzuku ya nafaka, lakini katika miaka ya hivi karibuni, watu wa mkoa huo walianza kufanya majaribio ya kubadilisha njia za jadi za kupanda mazao, na wamegundua njia mpya za kujiendeleza kwa kueneza matumizi ya mabanda ya kupanda mazao kwenye sehemu zenye mwinuko mkubwa kutoka usawa wa bahari. Hivi sasa njia hiyo imekubaliwa na kutumiwa na wakulima wengi wa huko.

Wilaya inayojiendesha ya kabila la Wa-tu ya Huzhu ni moja kati ya sehemu zinazofanya majaribio ya kuendeleza kilimo cha mzunguko kwa kutumia mabanda ya kupanda mazao. Kwa mujibu wa hali ya huko ya soko lisilokamilika la mboga, idara husika zinawaongoza wakulima wa miji midogo mitano ya wilaya hiyo kushughulikia upandaji wa mazao ya biashara kwenye mabanda hayo ikiwa ni pamoja na mboga zisizo na uchafuzi, uyoga mweupe, mawaridi na mapichi, ambao umeleta mapato karibu yuan milioni 1.3 na umekuwa njia mpya ya kuongeza mapato kwa wakulima.

Bw. Yang Youchang ni mkuu wa kijiji cha Xiayi cha mji mdogo wa Wufeng wa wilaya hiyo. Alipozungumzia mapato yanayopatikana kwa kupanda mazao kwenye mabanda alisema,

"Tumejenga mabanda zaidi ya 400 ya kupanda mazao, tukipata mapato ya yuan elfu 5 kwa kila banda kwa mwaka, kwa ujumla tunaweza kupata yuan milioni 2. Hayo si mapato makubwa, wakulima kadhaa wanaweza kupata yuan elfu 10 kila banda kwa mwaka. Mwaka jana wastani wa mapato kwa mtu ulikuwa ni yuan 2920, tutafanya juhudi kuhakikisha mapato hayo yanafikia yuan elfu 8 hadi elfu 10 katika siku za usoni."

Ikiwa ni njia mpya ya maendeleo ya uchumi, uchumi wa mzunguko umetimiza matumizi ya takataka. Serikali ya wilaya ya Huzhu imetenga fedha nyingi ili kuwasaidia wakulima kujenga mabanda ya kupanda mazao, kubadilisha njia ya zamani ya kupanda mazao nje, na kuwaongoza kupanda mazao yanayoweza kuleta nyongeza kubwa ya thamani. Hatua hizo zimewapatia wakulima wa huko mapato mengi ambayo hawakujayatarajia.

Katika kijiji cha Xiayi, serikali ya huko si kama tu imetenga fedha kuwasaidia wakulima kujenga mabanda, bali pia inawasaidia kujenga vifaa husika vikiwemo mashimo ya kuzalisha gesi ya kinyesi. Wameunganisha pamoja mabanda ya kufuga nguruwe, choo, mashimo ya kuzalisha gesi ya kinyesi na mabanda ya kupanda mazao, na wamejenga nyumba mpya za wakulima na kuweka vyombo vya kupika chakula kwa nishati ya jua, ambavyo vinaweza kuhifadhi mazingira ya viumbe. Katika kijiji cha Xiaji, mwandishi wetu wa habari aliona mabanda ya kupanda mazao yako karibu na nyumba mpya na safi za mkulima. Katika nyumba moja ya wakulima, nguruwe wanafugwa kwenye mabanda, chini ya mabanda hayo kuna shimo la kuzalisha gesi ya kinyesi, na mawaridi yanapandwa katika mashamba yaliyo karibu na mabanda hayo. Mama mmoja aliyekuwa akichuma mawaridi alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,

"Tulipanda mawaridi hayo mwezi Machi mwaka jana, hadi sasa nimepata yuan 1300 kwa kuuza mawaridi, na tutaweza kupata yuan 400 hivi kwa kuuza mawaridi ninayovuna leo. Chini ya ardhi kuna shimo la kuzalisha gesi ya kinyesi. Gesi hiyo safi inaweza kutumiwa jikoni, hatuna haja ya kununua makaa ya mawe, na kuni na mabua ya ngano zilizotumiwa zamani sasa zinauzwa, tumebana matumizi ya fedha."

Miji midogo ya Nanmenxia ya wilaya ya Huzhu pia inaendeleza matumizi ya mabanda ya kupanda mazao. Serikali ya huko inawaongoza wakulima kuotesha uyoga mweupe kwenye mabanda kwa kutumia mabua na vinyesi vya ng'ombe. Uyoga huo unafaa kukua kwenye sehemu zenye baridi, na unauzwa mwaka mzima kwa bei kubwa. kuotesha uyoga kumekuwa njia mpya ya kujiendeleza kwa wakulima wa huko. Bw. Lei Youwu ambaye alikuwa mtu wa mwanzo kuotesha uyoga alisema,

"kama hakutatokea maafa ya kimaumbile, tukipanda mazao ya kawaida yakiwemo cole, shayirli na viazi kwenye hekta 0.067 za mashamba, tunaweza kupata yuan 400 hadi 500, lakini tukiotesha uyoga kwenye hekta 0.027, tunaweza kupata yuan elfu 3 hadi elfu 4. Mapato hayo ni makubwa zaidi. Kutokana na maafa ya kimaumbile yanatokea mara kwa mara hapa, kupanda mazao ya kawaida nje yanaathiriwa na hali ya hewa, lakini kupanda mazao kwenye mabanda hayaathiriwi na maafa ya ukame au mafuriko."

Bw. Lei Youwu alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kuotesha uyoga si kama tu kunalenga kumudu maisha yao, bali pia ni kufanya uwekezaji, alisema,

"Matumizi ya fedha kwa ajili ya kuotesha uyoga mweupe ni madogo, lakini mapato ni makubwa, hivyo wakulima wanafanya juhudi kuotesha uyoga. Tunahitaji kutumia yuan mia kadhaa kununua mbegu za uyoga, na tunatumia mabua ya ngano, vinyesi vya ng'ombe na masalio ya kuzalisha mafuta kuotesha uyoga, na kutumia maji ya shimo la kuzalisha gesi ya kinyesi kuwa mbolea ya kuotesha uyoga, ambayo inaweza kuongeza uzalishaji wa uyoga kwa asilimia 40 bila ya kutumia fedha. Si kama tu tumeinua sifa za uyoga, bali pia tumeongeza mapato yetu, na kuanzisha mzunguko mzuri."

Uzoefu wa mkoa wa Qinghai unaonesha kuwa kilimo cha mzunguko kinaweza kuinua ufanisi wa matumizi ya maliasili, kuongeza mavuno, na kufanya mambo yasiyowezekana zamani kuwa mambo halisi ya hivi sasa. Wakulima wa mkoa huo wametimiza njia mpya za kuendeleza uchumi wa mzunguko kwa kutumia teknolojia za kisasa.