Mawaziri kutoka nchi kubwa 35 wanachama wa Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) tarehe 21 Julai huko Geneva kwenye makao makuu ya shirika hilo walianza kufanya mkutano wa wiki moja, na kujaribu kufanya mazungumzo ya Doha yaliyoendelea kwa miaka saba yamalizike kwa mafanikio. Sasa mazungumzo ya doha yako mbele ya kivuko kingine muhimu.
Mkutano wa namna hiyo ni mkutano mdogo wa ngazi ya mawaziri. Huu si utaratibu wa mazungumzo ya Shirika la WTO kwa kufuata sheria yake, bali ni desturi iliyoanzishwa kutokana na mazungumzo ya zamani. Mkutano huo huitishwa na nchi fulani mwanachama wa WTO, na kuzishirikisha baadhi ya nchi wanachama, kwa ajili ya kujadili masuala muhimu ya mazungumo yanayohusika sera, ili kuhimiza mazungumzo hayo yafikie makubaliano.
Mkutano huo uliitishwa na katibu mkuu wa WTO Bw. Pascal Lamy. Bw Lamy anaona kuwa sasa ni wakati mzuri wa kuitisha mkutano wa ngazi ya mawaziri, na amebashiri kuwa uwezekano wa kufikia makubaliano kwenye mkutano huo ni zaidi ya asilimia 50.
Kwa kweli hivi sasa kuna sababu kadha wa kadha zinazoweza kusaidia kufanikisha mazungumzo ya Doha. Kwanza, nia ya kisiasa ya pande mbalimbali inaongezeka. Muda usiofikia mwezi mmoja tangu mkutano huo uamuliwe kuitishwa hadi kuanza kwa mkutano huo, nchi 35 wanachama wakubwa wa WTO zote zimetuma wajumbe wao wa ngazi ya juu kuhudhuria mkutano huo, na hali hii inaonesha kuwa pande mbalimbali zinatilia maanani sana mkutano huo. Kuongezeka kwa nia ya kisiasa ya pande hizo kunatokana na hali ya uchumi duniani. Tokea nusu ya pili ya mwaka jana, uchumi wa dunia umekuwa unakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo msukosuko wa soko la fedha, mfumuko wa bei, kupanda kwa bei ya chakula. Mazungumzo ya Doha yakipata mafanikio, thamani ya biashara ya kimataifa itaongezeka kwa dola za kimarekani kati ya bilioni 50 na 100, na hali hii bila shaka itasaidia sana uchumi wa dunia. Hivyo hivi sasa nchi yoyote haipendi kulaumiwa kuwa ni nchi inayosababisha kukwama kwa mazungumzo hayo.
Pili, maoni tofauti kati ya pande mbalimbali yanapungua. Tangu kurejeshwa kwa mazungumzo ya Doha mwaka jana, mipango miwili kuhusu kilimo na bidhaa zisizo za kilimo imetolewa. Mipango hiyo imezingatia maslahi ya pande zote, pia imesahihishwa na kuboreshwa mara tatu, na imekabidhiwa kwa mkutano huo wa ngazi ya mawaziri ili kujadiliwa. Ingawa hivi sasa nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea bado zinagongana kuhusu masuala kadhaa, lakini zikionesha busara na ushujaa kwenye mkutano huo, makubaliano yanaweza kufikiwa.
Kwa upande mwingine, matokeo ya mazungumzo ya Doha yanahusu maslahi ya kimsingi ya nchi mbalimbali wanachama duniani, hivyo hazitalegeza msimamo wao kwa urahisi, na hivi sasa hasa nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea zina migongano mikubwa. Tangu mwanzoni mazungumzo yalipoanza, madhumuni yake ni kuondoa hali isiyo ya haki kwenye biashara ya kimataifa, ili kuwezesha nchi zinazoendelea kupata fursa nyingi, na hali hiyo isiyo ya haki inatokana na Marekani na Umoja wa Ulaya kutoa ruzuku kubwa ya kilimo kwa nchi zao huku zikitoza ushuru mkubwa kwa bidhaa za kilimo zinazoagizwa kutoka nchi nyingine. Kwenye mazungumzo ya Doha, Marekani na Umoja wa Ulaya hazitaki kupunguza ruzuku hizo, bali zinazifanya ziwe masharti ya kuzilazimisha nchi zinazoendelea zifungue soko la bidhaa za viwanda na huduma kwao. Takwimu zinaonesha kuwa nchi zinazoendelea zina nafasi ndogo ya biashara ya kimataifa huku zikitozwa asilimia 70 ya ushuru wa forodha duniani, hali hii inaonesha wazi kuwa, nchi zinazopaswa kupunguza ushuru wa forodha si nchi zinazoendelea, bali ni nchi zilizoendelea.
|