Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-23 17:44:49    
Serikali ya Singh yapata kura ya uungaji mkono

cri

Mkutano maalumu wa baraza la chini la bunge la India ulimalizika mjini New Delhi saa mbili usiku ya tarehe 22. mkutano huo ulifanya upigaji kura za uaminifu kuhusu serikali ya chama cha UPA inayoongozwa na waziri mkuu Manmohan Singh wa chama cha Congress, serikali hiyo itaendelea na utawala wake kwa kura 275 za ndiyo, na kura 256 za hapana.

Chanzo cha mgogoro huo wa kisiasa nchini India ni makubaliano ya ushirikiano wa nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia yaliyosainiwa mwezi Machi mwaka 2006. Makubaliano hayo yanaagiza kuwa, India inaweza kupata nishati na teknolojia ya nyuklia kutoka kwa Marekani bila ya kusaini "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia, lakini India inapaswa kutenganisha zana za nyuklia za kiraia na za kijeshi, iahidi kutotumia teknolojia na vifaa vya nyuklia zilizotolewa na nchi za nje katika mambo ya kijeshi, pia ikubali usimamizi wa shirika la nishati ya atomiki la duniani. Mgogoro mkubwa ulizuka nchini India mara tu baada ya makubaliano hayo kutangazwa.

India ilianza kuendeleza nishati ya nyuklia tangu miaka mingi iliyopita, na iliwahi kufanya majaribio ya mlipuko wa zana za nyuklia mwaka 1974, tena ilifanya majaribio ya silaha ya nyuklia mwezi Mei mwaka 1998. Lakini katika upande wa teknolojia ya nyuklia, siku zote India inakabiliwa na shida ya upungufu wa wataalamu na zana za miundo-mbinu. Hususan katika upande wa teknolojia ya nyuklia ya matumizi ya kiraia, India inakabiliwa na shida nyingi isizoweza kuziondoa. Katika miaka mingi iliyopita, India ilijitahidi kwa kutegemea nguvu zake yenyewe kuendeleza mfumo wa nyuklia, lakini mfumo huo haukuweza kuwa chombo chenye nguvu cha kukuza uchumi wa taifa na kutatua upungufu wa nishati, kinyume chake ulikuwa mzigo mkubwa wa kutumia fedha nyingi. Hivyo India ina haraka ya kupata misaada kutoka nchi za nje. Mwaka 2005, rais George Bush wa Marekani alikuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa India Bw. Manmohan Singh huko Washington, ambapo Marekani na India zilianza rasmi mazungumzo kuhusu ushirikiano wa nyuklia. Baada ya kufanya mazungumzo magumu, mwezi Machi mwaka 2006, wakati rais George Bush wa Marekani alipofanya ziara nchini India, nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya ushirikiano wa nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia.

Lakini, mapatano hayo yanayoonekana ni ya kuinufaisha sana India, yalipingwa vikali nchini India. Watu wa mrengo wa kushoto walisema, makubaliano ya nyuklia ya India na Marekani yanafanya India itii matakwa ya Marekani, na kukubali shirika la nishati ya nyuklia la dunia, ambalo linadhibitiwa na Marekani kihalisi, kukagua zana za nyuklia zilizopo sasa za nchini India, hatua hii itatishia vibaya maslahi na heshima ya taifa la India. Chama cha Bharatiya Janata kilisema, toka miaka mingi iliyopita Marekani imekuwa ikitekeleza sera za "kudhibiti kwa mbinu ya kushiriki" teknolojia za kisasa za nchi nyingine, mapatano ya nyuklia ya India na Marekani yatafanya mpango wa nyuklia wa India kuwa mfumo mdogo katika mpango wa nyuklia wa Marekani, iko siku moja Marekani itadhibiti maendeleo ya India kwa kutumia mpango huo, na kunyakua maslahi ya kimsingi ya India.

Tarehe 9 mwezi huu, vyama vinne vya mrengo wa kushoto, kikiwemo chama cha Kikomunisti cha India, viliondoa uungaji mkono kuhusu serikali ya Singh. Hivyo, muungano wa Utawala uliokuwa na wingi mdogo sana wa viti kwenye bunge la taifa, umekuwa na viti vichache. Kwa hiyo, chama kikubwa cha upinzani nchini India, yaani chama cha Bharatiya Janata kilitaka baraza la chini la bunge kuitisha mara moja mkutano maalumu na kupiga kura za uaminifu kuhusu serikali ya Singh.

Kwa mujibu wa sheria za India, chama tawala chochote kikitaka kuendelea na utawala wake, kinapaswa kupata wingi wa kura zote za 543 bunge. Kwa kuwa baadhi ya viti katika bunge viko wazi, kwa hiyo serikali katika upigaji kura huo ikipata kura 271, itakuwa imeshinda. Matokeo ya upigaji kura ni kuwa serikali ya Singh ilipata kura 275 za ndiyo, hivyo serikali ya Singh itaweza kuendelea na utawala hadi kufikia muda wake mwakani.

Wachambuzi wanasema, hata hivyo malalamiko na maandamano yaliyotokea nchini India ya kupinga makubaliano ya ushirikiano wa nyuklia, yatazidisha kikwazo kwa kupitishwa kwa makubaliano hayo ya ushirikiano wa nyuklia.