Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-24 20:03:53    
Mazungumzo kuhusu suala la nyuklia yafanyika Singapore

cri

Mazungumzo yasiyo rasmi ya mawaziri wa mambo ya nje wa pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea yalifanyika tarehe 23 huko Singapore. Waziri wa mambo ya nje wa nchi mwenyekiti wa mazungumzo ya pande 6 Bw. Yang Jiechi aliendesha mkutano, waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Bw. Pak Ui Chun, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice, waziri wa mambo ya nje wa Japan Bw. Komura Masahiko, waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergey Lavrov na waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya Kusini Bw. Liu Ming-hwan walishiriki kwenye mazungumzo hayo. Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mazungumzo kumalizika, Bw. Yang Jiechi alisema,

"Mazungumzo yasiyo rasmi ya mawaziri wa mazungumzo ya pande ni muhimu sana, yameonesha matarajio ya pande 6 ya kuendelea na mazungumzo. Pande mbalimbali zilibadilishana maoni kuhusu mchakato wa mazungumzo ya pande 6 na baadhi ya masuala muhimu. Mazungumzo yamezidisha maoni ya namna moja, kuimarisha maelewano na yamefanya maandalizi kwa ajili ya mazungumzo rasmi ya mawaziri wa mambo ya nje wa pande 6."

Kuhusu hotuba ya waziri Yang, waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya Kusini Bw. Liu Ming-hwan alisema,

"Ingawa hayo ni mazungumzo yasiyo rasmi, lakini kufanyika kwa mazungumzo kunaonesha utaratibu wa mazungumzo ya pande 6 umekomaa."

Kwenye mazungumzo hayo pia ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mawaziri wa mambo ya nje wa Korea ya Kaskazini na Marekani kukutana tangu mazungumzo ya pande 6 yaanzishwe. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Rice alipohojiwa na mwandishi wa habari baada ya mazungumzo, hakutaja vifungu kamili vya mazungumzo, lakini alisema hali ya mazungumzo ilikuwa "nzuri sana". Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Bw. Pak Ui Chun, ambaye alikuwa mtu mwingine aliyefuatiliwa sana kati ya watu walioshiriki kwenye mazungumzo, hakueleza moja kwa moja kuhusu kukutana kwake na Bi. Rice. Msemaji mwingine wa wizara ya mambo ya nje wa Korea ya Kaskazini alisema,

"Bw. Pak Ui Chun kwenye mazungumzo alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mazungumzo ya pande 6, na majukumu ya pande mbalimbali yaliyotajwa katika taarifa ya pamoja ya tarehe 19 Septemba. Na alieleza kwa kirefu kuhusu matarajio ya Korea Kaskazini ya kutekeleza nia ya taarifa ya pamoja, na alitarajia kuwa pande mbalimbali husika pia zitafuata kanuni za vitendo kwa vitendo."

Bw. Yang Jiechi akiwa mwenyekiti wa mazungumzo ya pande 6, alijumuisha mafanikio yaliyopatikana kwenye mazungumzo hayo. Alisema katika mazungumzo ya safari hii, pande mbalimbali zilifikia maoni ya namna moja, kwanza zinaona kutokana na jitihada za pamoja, mazungumzo ya pande 6 yamepata mafanikio muhimu ya kipindi. Pili, pande mbalimbali zimesisitiza kuwa, zitatekeleza kwa makini ahadi zilizotolewa na kila upande katika taarifa au waraka wa pamoja. Tatu, pande zote zinaona kuwa, mazungumzo ya pande 6 yametoa nafasi muhimu kwa pande hizo kuzidisha maelewano na uaminifu, na kufanya mazungumzo kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la peninsula ya Korea, kutimiza hali ya kawaida ya uhusiano wa nchi husika pamoja na kujenga utaratibu mpya wa masikilizano kwenye sehemu ya Asia kaskazini mashariki. Nne, pande zote zinakubali kutekeleza mpango wa vitendo wa kipindi cha pili kwa pande zote, ulingano na kwa njia ya kuweza kuthibitishwa, ikiwa ni pamoja na kuafikiana kwa haraka kuhusu makubaliano ya ukaguzi na uthibitishaji. Tano, pande zote zinaona kuwa, uhimizaji wa mazungumzo ya pande 6 unaambatana na maslahi ya pamoja ya pande 6. Sita, pande zote zinakubali kuitisha mazungumzo rasmi ya mawaziri wa mambo ya nje wa pande sita katika wakati unaofaa.