Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-28 21:21:08    
Msitu wa mawe nchini China

cri

Sehemu yenye mandhari ya msitu wa mawe mkoani Yunnan, kusini magharibi mwa China ni sehemu ya utalii ya mjini Kunming toka miaka mingi iliyopita, sehemu hiyo inajulikana sana duniani kwa kuwa na mawe mengi makubwa ya chokaa yenye maumbo ya ajabu yanayojitokeza kwenye ardhi. Wakati michezo ya Olimpiki inapokaribia kufanyika, sehemu hiyo yenye mandhari ya msitu wa mawe inajiandaa kuwapokea watalii wa nchini na kutoka nchi za nje.

Sehemu yenye msitu wa mawe iko umbali wa kilomita 100 kutoka mji wa Kunming, sehemu hiyo kubwa inaweza kugawanyika katika sehemu 8 ndogo zenye vivutio mbalimbali ikiwemo msitu mkubwa na mdogo wa mawe, msitu wa mawe ya kale, maporomoko makubwa ya maji, ziwa refu, na ziwa la mwezi. Zaidi ya miaka milioni 270 iliyopita, msitu wa mawe ulikuwa bahari, mawe ya chokaa yaliyoko baharini yalibadilika kuwa vifereji na nguzo za mawe kwa kuchimbwa na maji ya bahari, na baadaye sehemu hiyo iliinuka juu ya ardhi, ikawa sehemu yenye mandhari nzuri ajabu kama ilivyoelezwa katika hadithi za watoto.

Katika miaka ya 50 ya karne ya 20, serikali ya China ilishirikisha wataalamu kwenda kufanya upimaji na usanifu kwenye msitu wa mawe, na kujenga miundo mbinu, sehemu hiyo ilifunguliwa rasmi kwa nje mwaka 1976, ambapo watalii waliotoka sehemu mbalimbali wameweza kuiona mandhari hiyo ya ajabu ya kimaumbile, ambayo inaonekana kwa nadra sana. Wakazi wa sehemu ya msitu wa mawe ni wa makabila madogo madogo, ambao wengi wao ni wa kabila la Wa-sani, ambalo ni tawi moja la kabila la Wayi. Mara tu watu wakiingia kwenye sehemu ya msitu wa mawe, wanaweza kuhisi uchangamfu na ukarimu wa wakazi wa makabila madogo wa huko na umaalumu wa kikabila.

kwenye mlango wa kuingia kwenye sehemu ya msitu wa mawe, wasichana na wavulana wa kabila la Wa-sani walijipanga kwenye mistari miwili, wavulana wanapiga ala za muziki na wasichana wakiimba huku wakicheza ngoma kuwakaribisha wageni waliotoka sehemu nyingine. Ala za muziki wanazoshika mkononi wavulana Wa-sani pamoja na mavazi yao ya kikabila yenye rangi mbalimbali, zinawafurahisha sana watalii.

"Mwandishi habari: Ala ya muziki unayotumia ni ya aina gani?

Kijana M-sani: ni kama zeze yenye nyuzi tatu.

Mwandishi habari: inaonekana kidogo inafanana na gambusi, ni ala ya muziki ya jadi ya hapa?

Kijana: Sawa.

Mwandishi habari: Ala za muziki mnazopuliza ni za aina gani?

Kijana: Ni ala za muziki za jadi za hapa kwetu, zinaitwa filimbi za Men, kuna vitundu 7 juu yake, na ni tofauti kidogo na filimbi za kawaida."

He Jialan ni msichana mzuri wa kabila la Wasani, ambaye ni mmoja wa waongoza hodari kabisa wa matembezi ya watalii kwenye sehemu ya msitu wa mawe, aliwahi kuongoza watalii wengi mashuhuri wa nchini na wa nchi za nje kutembelea msitu wa mawe. Alisema,

"Sura ya ardhi ya msitu wa mawe ni yenye mawe ya chokaa, inayoumbika katika mazingira fulani ya kijiografia, hali ya hewa na mazingira. Msitu wa mawe uliumbika zaidi ya miaka milioni 270 iliyopita katika kipindi cha permian."

Msichana huyo alituambia, misitu mikubwa na midogo ya mawe ni sehemu ambazo watalii hawapaswi kukosa kuziona. Moja ya sababu zake muhimu ni kuhusika na msichana Ashima, msichana mzuri na mwema wa kabila la Wasani. Hivi sasa msichana huyu amekuwa alama ya mkoa wa Yunnan, Wa-sani wa siku hizi wana maneno mengi ya kueleza wakati wanaposimulia hadithi ya msichana huyo. Alisema

"Wakati ule, Ashima alikuwa akichumbiana na kaka Ahei, lakini mtoto wa mtemi wa huko Azhi, pia alimpenda msichana Ashima. Azhi alijaribu kumwoa Ashima kwa nguvu, baada ya kupata habari, Ashima na Ahei walikimbia, wakafika kwenye sehemu ya msitu wa mawe. Azhi alikasirika, akatoa maji ya ziwa, Ashima na Ahei walizama kwenye maji, baada ya maji ya ziwa kuondoka, Ashima akageuka kuwa sanamu ya mawe, akimngoja Ahei hadi hivi sasa. Sasa watu wanapomkumbuka msichana Ashima, wanafika kwenye sanamu na kuita jina lake, wakahisi kama Ashima bado yuko pamoja nao."

Baada ya kupita sehemu hiyo, watalii wanaweza kuona nguzo nyingi za mawe ambazo maumbo yao ni kama vitara zinasimama mbele, ambapo wanashangazwa na mandhari ya msitu wa mawe ulio wa kweli mbele yao.

"Nguzo hizo ni mawe marefu yaliyo kama upanga, baada ya kuliwa na maji ya mvua katika miaka mingi iliyopita, jiwe hilo kama upanga wenye makali, chini ya jiwe hilo ni mawe yanayoonekana kama miale ya moto, inasemekana kuwa mwaka ule kaka Ahei alipotaka kumwokoa Ashima, alipita kwenye sehemu hiyo bila kujali kuchomwa na upanga na moto mkali."

Watu wakiendelea mbele kwa kufuata njia hiyo nyembamba, wataweza kuona jiwe moja lenye mfano wa jino. Watalii wanaofika huko hupenda kupapasa jiwe hilo.

"Kule juu kuna jiwe moja linalofanana na jino la binadamu, inasemekana kuwa watu wakipapasa jiwe hilo, hawatakuwa na haja ya kumwona daktari wakati wanapoumwa meno."

Ukienda mbele kidogo kuna pango moja, ambalo sehemu yake ya juu ni ndogo na sehemu yake ya chini ni pana, na ukitazama kutoka ndani umbo lake ni kama kengele, mwongoza watalii dada He Jialan alisema, mtu akiimba wimbo ndani ya pango, ni kama anaimba kwenye ukumbi maalumu wa muziki, ili kuonesha namna yake, dada He aliimba wimbo ulioimbwa kwenye sinema ya Ashima.

mbali na hayo, kuna mawe mengi kwenye msitu wa mawe yanayofana na paka, panya, mamba, mhusika Bajie wa kwenye hadithi ya "Safari ya Magharibi", tausi, kifaru na phoenix ilimradi kila mtu afikiri anavyopenda.