Takwimu mpya zilizotolewa na Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, hivi sasa upungufu mkubwa wa chakula unawatishia watu wapatao milioni 15 wanaoishi nchini Somalia, Ethiopia, Djibouti na kaskazini mwa Kenya, sehemu inayojulikana kama pembe ya Afrika. Msemaji wa shirika hilo Bw. Peter Smerdon ametoa onyo kuwa, janga la kibinadamu linaweza kuikumba sehemu hiyo kama hatua za kutoa msaada hazitachukuliwa haraka.
Miongoni mwa nchi hizo, hali nchini Ethiopia ni mbaya zaidi, ambapo watu milioni 10 hivi wanahitaji msaada, huku msaada wa dharura unapaswa kupelekwa kwa watu milioni 4.6 wanaotishiwa na njaa. Idadi hiyo ni mara moja zaidi kuliko ile ya watu milioni 2.2 ya mwanzoni mwa mwaka huu. Zaidi ya hayo nchini Ethiopia, watoto wapatao elfu 75 wana utapiamlo. Nchini Somalia watu milioni 2.6 hawawezi kumudu mlo mmoja kwa siku, kutokana na shughuli za kilimo nchini humo kuharibiwa vibaya kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, idadi hiyo huenda itaongezeka hadi kufikia milioni 3.5 ndani ya muda mfupi. Hivi sasa nchini Kenya, watu milioni 1.2 wanakabiliwa na upungufu wa chakula, na idadi hiyo ni kubwa zaidi kwenye sehemu ya Karamoja ya Uganda.
Wachambuzi wanasema sababu mbalimbali zinachangia hali ya upungufu wa chakula katika sehemu ya pembe ya Afrika, sababu hizo ni pamoja na ukame unaoendelea, maafa ya wadudu, kupanda kwa bei ya mafuta na sababu kadhaa za kisiasa.
Kutokana na athari ya kuongezeka kwa joto duniani, sehemu ya Afrika Mashariki haikupata mvua za kutosha katika miaka kadhaa ya hivi karibuni. Mtaalamu wa idara ya utabiri wa hali ya hewa ya Kenya amedokeza kuwa, mwaka huu kiwango cha wastani cha mvua kitapungua kwa asilimia 12 katika sehemu ya Afrika Mashariki, na kwa uhakika hali hii itaathiri mavuno.
Msukosuko wa kisiasa katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki pia uliathiri mavuno ya kilimo. Ghasia baada ya uchaguzi mkuu zilizotokea mwishoni mwa mwaka jana nchini Kenya zilisababisha wakulima wengi washindwe kupanda mbegu katika muda mwafaka, hivyo mavuno yalipungua kwa kiasi kikubwa. Somalia nchi inayosumbuliwa na vita, shughuli za kilimo zimeachwa, na watu wa huko wanategemea kabisa msaada wa chakula kutoka jumuiya ya kimataifa.
Ili kukabiliana na msukosuko wa chakula katika sehemu ya Afrika Mashariki, shirika la mpango wa chakula limeomba jumuiya ya kimataifa itoe msaada wenye thamani isiyopungua dola za kimarekani milioni 400 kwa sehemu ya pembe ya Afrika. Shirika hilo pia limenunua chakula kutoka India na Afrika Kusini na kupeleka kwenye sehemu hiyo. Mbali na hayo nchi za Afrika Mashariki zilianza kuchukua hatua za kuzuia kuenea kwa janga la kibinadamu.
Serikali ya Kenya itajenga mfumo wa umwagiliaji katika sehemu kame nchini humo na kuongeza eneo la mashamba yanayopandwa mimea ya chakula kutoka hekta laki 2.5 hadi hekta milioni moja. Serikali hiyo pia itachukua hatua zenye unafuu za kusaidia wakulima wapande kwa wingi mimea ya chakula, hatua hizo ambazo zitaanza kuchukuliwa mwakani ni pamoja na kutoa ruzuku kwa mbolea na mbegu na kuwapa wakulima mikopo ya kilimo. Imefahamika kuwa Kenya ilianza kujenga vituo vya biashara ya chakula katika miji mitano mikubwa nchini humo ikiwemo Nairobi, na kila kituo kitakuwa na majokofu makubwa ya kuhifadhia chakula. Aidha serikali ya Kenya ilitoa idhini kuagiza kwa dharura tani laki 2.7 ya mahindi kutoka nchi za nje.
|