Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-07-31 21:03:44    
Je hali ya kupungua kwa bei ya mafuta ni ya muda?

cri

Baada ya bei ya mafuta kupanda na kufikia kiwango cha juu kabisa mwanzoni mwa mwezi Julai, bei hiyo ilianza kupungua kwa mfululizo. Tarehe 29 mwezi Julai bei ya mafuta ilikuwa dola za Marekani 122.19 kwa pipa ambayo ilishuka kwa 2.5% ikilinganishwa na siku ya biashara iliyotangulia, na bei hiyo ilikuwa ni chini kabisa tokea mwezi wa Mei na ilipungua kwa zaidi ya dola za Marekani 23 ikilinganishwa na bei ya mwanzoni mwa mwezi huo Julai. Bei ya mafuta nchini Marekani ilipungua kwa dola nne za kimarekani kwa galoni kutokana na watu wanaotumia magari kupungua kwa kiasi kikubwa, na bei ya gesi pia imepungua kwa 33% kuliko ile ya mwanzoni mwa mwezi huo Julai.

Kupungua kwa bei ya mafuta kumeleta faraja kwa kiasi fulani katika mazingira ambayo nchi mbalimbali zinakumbwa na mfumuko wa bei, na hali ya uchumi wa dunia kudidimia. Kupungua kwa bei ya mafuta duniani kunatokana na mabadiliko ya bei ya mazao, kama vile mahindi, ngano na mpunga, hali imeonesha kwamba bei ya mafuta iliyopanda haraka tokea mwanzoni mwa mwaka huu ilipita kiasi bila sababu ya msingi. Wachambuzi wanaona kuwa bei ya mafuta itaendelea kupungua. Mwenyekiti wa OPEC Bw Chakib Khelil alisema huenda bei ya mafuta itapungua hadi kufikia dola za kimarekani 70 kwa pipa.

Wataalamu wanaona kuwa kabla ya hapo bei ya mafuta ilipanda haraka kutokana na kushuka kwa thamani ya dola ya kimarekani. Kushuka kwa thamani ya dola za Marekani kulisababisha bei ya mafuta na madini ya chuma inayohesabiwa kwa thamani ya dola za kimarekani kupanda na kusababisha kupanda kwa bei ya mazao yanayotokana na maliasili hizo. Kwa hiyo hali ya uchumi nchini Marekani itaathiri bei ya mafuta.

Lakini kupungua kwa bei ya mafuta kwenye soko la kimataifa pia kumesababisha kupungua kwa bei ya mafuta nchini Marekani, ingawa kiasi cha kupungua huko hakijawafuatiliwa sana na Wamarekani, lakini watu wanafikiri kuwa pengine kupungua kwa bei ya mafuta kutasaidia kufufuka kwa uchumi nchini humo. Bila shaka yoyote kupungua kwa bei ya mafuta kutahimiza ustawi wa sekta za usafiri wa ndege na umeme. Baadhi ya wataalamu wa uchumi wanasema, kama bei ya mafuta ikiendelea kupungua, wateja wa Marekani wanaamini kuwa hali hiyo itadumu na wala sio ya muda, kwa hiyo watajitahidi kufufua uchumi.

Sambamba na hayo, kupungua kwa mahitaji ya mafuta kwa nchi fulani pia yamesababisha kupungua kwa bei ya mafuta. Bw. Chakib Khelil alisema, katika miaka ya hivi karibuni kasi ya maendeleo ya uchumi wa nchi kubwa zinazoendelea kama China, India na Brazil imepungua, hali hiyo pia imezuia kupanda kwa bei ya mafuta. Mchambuzi wa kampuni ya Raymond James & Associates Bw. Scott Brown alisema, kasi ya maendeleo ya uchumi barani Ulaya pia imepungua, na mahitahi ya mafuta yamepungua.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa hali ya kushuka kwa bei ya mafuta ni ya muda mfupi, kwa mtazamo wa muda mrefu hali ya kupanda kwa bei haiepukiki. Kwanza, kiasi cha mafuta duniani kinapungua na mahitaji ya mafuta hayatapungua. Pili, hali ya uchumi nchini Marekani mpaka sasa haina dalili yoyote ya kuimarika, na kushuka kwa thamani ya dola za Marekani hakujadhibitiwa, na itakuwa ni vigumu kwa hali ya kupanda kwa bei ya mafuta kubadilika.

Baadhi ya wataalamu wanaonya kuwa kimbunga kwenye sehemu ya kuzalisha mafuta ya Ghuba ya Mexico na hali ya wasiwasi wa kisiasa katika Ghuba ya Uajemi itasababisha kupanda tena kwa bei ya mafuta. Mchambuzi wa mambo ya uchumi wa kundi la Economic Outlook Bw. Bernard Baumohl alisema, "Ingawa bei ya mafuta inaendelea kupungua kwa mfululizo lakini hatuwezi kuhakikisha kuwa hali hiyo itadumu, huenda bei ya mafuta itapanda tena kwa haraka baadaye kama inavyoshuka sasa."

Na hali ya bei ya mafuata duniani ya tarehe 30 Julai kama imethibitisha maoni hayo ya wachambuzi hao.