Mkutano wa 15 wa mawaziri wa Harakati zisizofungamana na upande wowote ulifungwa tarehe 30 Julai huko Tehran. "Waraka wa mwisho" uliopitishwa kwenye mkutano huo umeona kuwa, mkutano huo unasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya kusini na kusini, kuzihimiza nchi zinazoendelea zifikie makubaliano kuhusu mambo ya kisiasa, na kusaidia kufanya ushirikiano kwa kujiendeleza na kustawisha tena Harakati zisizofungamana na upande wowote. Wajumbe kutoka nchi 118 zinazoshiriki kwenye harakati hizo, nchi 15 za wachunguzi na jumuiya 8 za Kimataifa na kikanda walihudhuria mkutano huo.
Waziri wa mambo ya nje wa Cuba ambayo ni nchi mwenyekiti wa zamu wa Harakati zisizofungamana na upande wowote Bw. Felipe Perez Roque aliona kuwa, majadiliano ya mkutano huo kuhusu mada yoyote yalifanyika kwenye hali ya kiujenzi inayohimiza watu wafanye juhudi, na hali ya mshikamano wa kauli moja ilijaa kwenye mkutano tangu mwanzo hadi mwisho. Nchi zaidi ya 60 zilituma mawaziri wao wa mambo ya nje kuhudhuria mkutano huo, hali ambayo imeonesha nguvu ya Harakati zisizofungamana na upande wowote, pia imeonesha kuwa nchi zinazoshiriki kwenye harakati hizo zimesifu tena nguvu zenye uhai za harakati hizo. Bw. Perez aliona kuwa mkutano huo utainua hadhi na ushawishi wa Harakati zisizofungamana na upande wowote kwenye jukwaa la kimataifa.
"Waraka wa mwisho" uliopitishwa kwenye mkutano huo umeona kuwa, katika hali ya utandawazi wa uchumi duniani, nchi za Harakati zisizofungamana na upande wowote zinakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na masuala ya kikanda ya usalama na amani, maendeleo ya uchumi na jamii, haki za binadamu na utawala wa kisheria. Katika mambo ya Kimataifa, maamuzi ya upande mmoja wa nchi kubwa yamekuwa changamoto kubwa zaidi inayozikabili nchi za Harakati zisizofungamana na upande wowote. Mkutano huo unapinga kwa kauli moja nchi kubwa kutekeleza sera za kutoa maamuzi ya upande mmoja katika mambo ya Kimataifa, na kuchukua hatua za upande mmoja za kuziwekea nchi ndogo na dhaifu vikwazo vya kiuchumi. Mkutano huo uliendelea kutetea kauli mbiu ya mkutano wa 14 wa mawaziri wa nchi za Harakati zisizofungama na upande wowote, kutetea kuhimiza kuwepo kwa ncha nyingi duniani, na kusukuma mbele maendeleo ya ushirikiano wa pande nyingi.
Kuhusu suala la haki za binadamu, mkutano huo umesisitiza kuwa, demokrasia ni lazima iwekwe kwenye msingi wa nia ya wananchi. Mkutano huo umeona kwa kauli moja kuwa, wananchi wa nchi mbalimbali wana haki ya kuchagua mifumo ya siasa, uchumi, jamii na utamaduni ya nchi zao. Mkutano huo umelaani "kutembeza" kwa makusudi ya kisiasa ati suala la "haki za binadamu katika mambo ya Kimataifa", na kupinga nchi fulani kufuata vigezo viwili wakati wa kushughulikia migogoro ya Kimataifa na mambo ya kikanda.
Taarifa kuhusu suala la nyuklia la Iran na suala la Zimbabwe zilizopitishwa kwenye mkutano huo zimeona kuwa, kutumia na kuendeleza kiamani nishati ya nyuklia ni haki isiyonyimika kwa kila nchi, mkutano huo unaunga mkono kwa kauli moja Iran itumie kiamani teknolojia ya nyuklia, na Shirika la Kimataifa la nishati ya atomiki ni Shirika pekee halali la kutoa maamuzi kuhusu shughuli za nyuklia za nchi wanachama wake. Taarifa kuhusu suala la Zimbabwe imeeleza ufuatiliaji mkubwa juu ya msukosuko wa kisiasa nchini Zimbabwe, na kupinga nchi za magharibi kutekeleza sera ya upande mmoja na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi ya Zimbabwe iliyoko kwenye hali ya kukwama kisiasa.
Kwenye mkutano huo Cuba iliendesha mkutano wa Kamati ya Harakati zisizofungamana na upande wowote kuhusu suala la Palestina. Wajumbe waliohudhuria mkutano huo wanaona kuwa suala la Palestina ni moja kati ya masuala makubwa ya Harakati ya nchi zisizofungamana na upande wowote, na kutoa mwito wa kuanzisha utaratibu wa mkutano wa Kimataifa wa kusaidia kuanzisha nchi ya Palestina.
Aidha mkutano huo pia umejadili kwa kina kuhusu masuala ya upunguzaji wa silaha duniani, ugaidi wa kimataifa, mabadiliko ya hali ya hewa na usalama wa nafaka kote duniani. Mkutano huo umesisitiza tena kuwa ni lazima kutimiza upunguzaji wa silaha kwa pande zote, hasa upunguzaji wa silaha za nyuklia. Mkutano pia unapinga na kulaani vikali vitendo vya ugaidi wa aina yoyote.
|