Tarehe 26 ubalozi wa China nchini Kenya ulifanya sherehe ya kuwaaga wanafunzi 42 wa Kenya watakaosoma nchini China ambao wamepata udhamini wa masomo na serikali ya China.
Pamoja na wanafunzi hao 42, kwa mwaka huu jumla ya wanafunzi 113 wa Kenya wamepata udhamini wa masomo ulitolewa na serikali ya China, kati yao 71 bado wanaendelea na masomo yao nchini China. Hii ni idadi kubwa ya wanafunzi watakaosoma nchini China katika historia yake. Kwenye sherehe hiyo, balozi wa China Bw. Zhang Ming aliwapongeza wanafunzi hao na kuwashajiisha wasome kwa bidii siku za baadaye wajenge taifa lao na waimarishe zaidi urafiki kati ya China na Kenya.
"Nina imani kuwa mtajifunza kwa juhudi. Nina imani nanyi kwamba hakika mtawaoneshea wanafunzi wa China na wa nchi nyingine uhodari wenu na kuthibitisha kwamba ninyi ni hodari kama mabingwa wenu wa michezo ya Olimpiki Samwel Kamau na Pamela Jelimo. Nakutakieni furaha ya masomo na maisha nchini China."
Waziri wa Elimu ya Juu wa Kenya Bi. Sally Kosgei alitoa shukrani kwa serikali ya China kutoa udhamini wa msomo kwa wanafunzi wa Kenya, na alieleza matumaini yake kuwa wanafunzi hao watathamini fursa hiyo ambayo haipatikani kwa urahisi, na pia aliwataka wajifunze kwa juhudi na baadaye walijenge taifa lao. Kwenye sherere Bi. Sally Kosgei alisifu sana Michezo ya Olimpiki ya Beijing akisema mafanikio ya michezo hiyo imeonesha sura ya China kwa dunia, aliwapa moyo wanafunzi wajifunze teknolojia ya kisasa kwa bidii ili baadaye watoe mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa. Alisema,
"Michezo ya Olimpiki ya Beijing imefanikiwa sana. Kenya imepata mafanikio makubwa ya kihistoria katika michezo hiyo na China imeonesha mvuto wake kwa dunia na imethibitisha kwamba China ina uwezo wa kufanya michezo ya Olimpiki kwa kiwango cha juu. Nakupongezeni, naipongezaChina! Baada ya ninyi kufika nchini China tutafuatilia sana hali ya masomo yenu. Popote mtakapofanya kazi baadaye, tuna matarajio kuwa mtalijenga taifa letu kwa elimu mliyoipata. Nakutakieni mrudi nyumbani na mafanikio!"
Imefahamika kwamba wanafunzi hao watatumia muda wa mwaka mmoja hivi kujifunza lugha ya Kichina na kuanzia mwaka wa pili wataanza kuchukua kozi mbalimbali. Wanafunzi hao watakuja China mwezi Septemba na watasoma katika vyuo vikuu kumi kadhaa. Kati yao Nura Mohamed atasomea shahada ya kwanza ya taaluma ya mambo ya fedha katika Chuo Kikuu cha Fedha na Uchumi cha China. Kuhusu maisha yake ya miaka minne ya masomo Nura Mohamed anajiamini kabisa, akisema,
"Sikuwahi kwenda China, hii ni fursa yangu isiyopatikana kwa urahisi, huko naweza kufahamu utamaduni wa China na kutafiti jinsi uchumi wa nchi hiyo ulivyoendelea. Kasi ya maendeleo ya China inavutia kote duniani, nitaona kwa macho yangu mwenyewe jinsi China inavyoendelea, na baada ya kurudi nchini Kenya nitakapofanya kazi serikalini, nitatumia uzoefu nitakaopata nchini China kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa taifa langu Kenya."
|