Mkutano wa 40 wa mawaziri wa uchumi wa nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki na mikutano husika imefanyika mfululizo nchini Singapor. Mawaziri wa uchumi wa nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki wamejadili na mawaziri wa uchumi wa nchi zinazofanya mazungumzo na umoja huo, ili kuimarisha zaidi ushirikiano na kusukuma mbele maendeleo ya uchumi wa sehemu hiyo.
Kwenye mkutano wa 7 wa mawaziri wa uchumi wa China na nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki uliofanyika tarehe 27 Agosti, pande mbili zilijadili masuala ya Kimataifa na kikanda, hasa kujadili masuala kuhusu makubaliano matatu yanayohusika na "Makubaliano ya ushirikiano kati ya China na Umoja wa Asia ya kusini mashariki kwenye sekta ya uchumi". Tarehe 4 Novemba mwaka 2002, viongozi wa China na nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki walisaini "Makubaliano ya ushirikiano kati ya China na Umoja wa Asia ya kusini mashariki kwenye sekta ya uchumi", na kuzindua rasmi mchakato wa kuanzisha sehemu ya biashara huria ya China na Umoja wa Asia ya kusini mashariki. Mwaka 2004, mazungumzo kuhusu "Makubaliano ya biashara ya bidhaa" yalikamilika, na mwaka 2006 mazungumzo kuhusu "Makubaliano ya biashara ya huduma" yalikamilika. Hivi sasa pande hizo mbili zinaendelea na mazungumzo kuhusu "Makubaliano ya uwekezaji kati ya China na Umoja wa Asia ya kusini mashariki". Mawaziri wa uchumi wameahidi kuendelea kuhimiza mazungumzo hayo, na kujitahidi kuyakamilisha mazungumzo hayo mwishoni mwa mwaka huu, ili kuhakikisha kazi ya kujenga sehemu ya biashara huria ya China na nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki itakamilika mwaka 2010.
Mawaziri wa uchumi wa nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki wamebadilishana maoni kuhusu mapendekezo ya China juu ya kuendeleza sehemu ya ghuba ya kaskazini na uwezekano wa ushirikiano kati ya China na umoja huo kwenye sekta ya uchumi ya ghuba ya kaskazini. Tangu mpango wa ushirikiano kwenye eneo la ghuba ya kaskazini utolewe mwaka 2006, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kwenye eneo hilo umeendelezwa kwa kasi, ambapo thamani ya biashara kati ya China na nchi 6 za eneo la ghuba ya kaskazini ilifikia dola za kimarekani bilioni 164.65 mwaka 2007, hili lilikuwa ongezeko la asilimia 26 kuliko ile ya mwaka 2006, eneo hilo linaendelezwa kuwa soko kubwa. Ushirikiano kati ya China na nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki kwenye eneo hilo umekuwa nguzo kubwa ya kuharaikisha kazi ya kujenga sehemu ya biashara huria kati ya China na nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki.
Kwenye mkutano wa 11 wa mawaziri wa uchumi wa nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki pamoja na China, Japan na Korea ya kusini uliofanyika tarehe 28, mawaziri wa nchi mbalimbali wameeleza imani yao kuwa, makubaliano ya biashara huria kati ya nchi 10 za Umoja wa Asia ya kusini mashariki na nchi za China, Japan na Korea kusini yatasaidia kutimiza malengo ya jumla ya utandawazi wa uchumi wa Asia ya kusini mashariki na Asia ya kaskazini mashariki. Mawaziri hao wametoa mwito wa kuyataka makampuni na mashirika yote ya biashara yajiunge na mchakato wa ushirikiano kati ya nchi 10 za Umoja wa Asia ya kusini mashariki pamoja na China, Japan na Korea kusini, ili kusukuma mbele maendeleo ya utulivu ya uchumi wa Asia ya mashariki.
Kwenye mkutano wa mawaziri wa uchumi wa nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki pamoja na China, Japan, Korea kusini, India, Australia na New Zealend, mawaziri wamebadilishana maoni kuhusu sekta za ushirikiano kati ya nchi hizo chini ya utaratibu wa mkutano wa wakuu wa Asia ya mashariki.
|