Jeshi la Marekani nchini Iraq tarehe 1 Septemba asubuhi huko Ramadi, mji mkuu wa mkoa wa Anbar, lilifanya sherehe ya kuikabidhi rasmi serikali ya Iraq mamlaka ya ulinzi wa mkoa wa Anbar. Hadi sasa, Iraq imekabidhiwa mamlaka ya ulinzi wa mikoa 11 kati ya mikoa 18. Hii ni mara ya kwanza kwa jeshi la Marekani kukabidhi mamlaka ya ulinzi wa mkoa unaoishi Waislam wa madhehebu ya Suni kwa serikali ya Iraq. Makabidhiano hayo unaufanya mkoa huo ufuatiliwe tena na watu.
Mwezi Machi mwaka 2003 kutokana na kutokea kwa vita dhidi ya Iraq, Iraq ilikuwa medani ya vita kati ya jeshi la Marekani na makundi ya kijeshi ya kuipinga Marekani. Mkoa wa Anbar ukiwa mkoa mkubwa kabisa nchini Iraq ulikuwa "sehemu yenye mapambano mengi zaidi", sio tu mapambano ya makundi ya kijeshi yanayopinga Marekani yalilifanya jeshi la Marekani liwe na vifo na majeruhi mengi, hata kundi la al-qaeda pia liliufanya mkoa huo uwe kituo chake kikubwa nchini Iraq.
Mwaka 2004 mkoa wa Anbar ulikumbwa na mapambano makali kabisa baada ya Marekani kuivamia Iraq, yaani vita vya Fallujah. Mwezi Novemba mwaka huo jeshi la Marekani nchini Iraq lilitumia silaha za kisasa, na kufanya mapambano makali kati yake na makundi ya kijeshi yanayopinga Marekani huko Fallujah. Mwishoni jeshi la Marekani lilinyakua mji wa Fallujah, lakini wanajeshi mia kadhaa wa jeshi hilo walikufa au kujeruhiwa.
Ingawa jeshi la Marekani lilikalia mji wa Falluja na mkoa mzima wa Anbar mwaka 2004, lakini halikuleta usalama na utulivu wa mkoa huo. Makundi yanayoipinga Marekani na watu wenye silaha wa kundi la al-qaeda walioficha katika sehemu mbalimbali walifanya mashambulizi ya kigaidi mara kwa mara mkoani Anbar, hata mkuu wa mkoa huo aliwahi kutekwa nyara. Maofisa maandamizi wa jeshi la Marekani nchini Iraq siku zote wanaona kuwa mkoa wa Anbar ni mkoa wenye hali mbaya kabisa ya usalama nchini Iraq.
Lakini mwezi Julai na Agosti mwaka 2007, hali ya usalama wa mkoa huo ilibadilika kuwa nzuri, na matukio ya kimabavu pia yalipungua kidhahiri. Marekani iliona kuwa kutokea kwa mabadiliko hayo kunatokana na rais Bush wa Marekani kuongeza wanajeshi 30,000 nchini Iraq. Lakini wachambuzi wanaona kuwa, mabadiliko hayo yanatokana na kutokea kwa "harakati za kuamka". Harakati hizo ni jumuia ya watu wa madhehebu ya Suni wa mkoa huo, ambao wanapinga kundi la "al-qaeda", na inatetea kushirikiana na jeshi la Marekani ili kupambana na watu wenye silaha wa kundi la al-qaeda. Jumuia hiyo iliwahi kuwa na wanachama 80,000, nayo ilifanya kazi muhimu katika kutuliza hali ya mkoa wa Anbar.
Mwezi Septemba mwaka 2007, rais Bush wa Marekani alizuru ghafla Iraq pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Bw. Robert Gates. Rais Bush hakwenda Baghdad, bali alikwenda kituo cha jeshi la Marekani mkoani Anbar, ambapo alifanya ziara yake ya saa 6 huko, ili kuonesha kuwa hali ya usalama wa mkoa huo kweli imekuwa nzuri kidhahiri.
Ingawa katika nusu ya pili ya mwaka 2007, hali ya usalama wa mkoa wa Anbar imekuwa nzuri, lakini sasa umekuwa mwaka mmoja baada ya rais Bush kuzuru mkoa huo, ndipo jeshi la Marekani lilipoikabidhi serikali ya Iraq mamlaka ya ulinzi ya Anbar, hii pia inaonesha kuwa, hali ya usalama wa Anbar bado haijatulia kabisa. Kama ilivyosema kwenye taarifa iliyotolewa na jeshi la Marekani nchini Iraq katika sherehe ya siku hiyo, "kukabidhi mamlaka ya ulinzi ya mkoa wa Anbar ni mnara muhimu, lakini haumaanishi kuwa hali ya Anbar imetulia au kuwa nzuri, bali unamaanisha kuwa serikali ya Iraq inaweza kushughulikia mambo ya usalama wa huko."
|