Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-11 17:57:57    
Mlemavu anayependa kuwasaidia wengine Bw. Shen Fucai

cri

Katika mji wa Baotou wa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, kaskazini mwa China, ukimtaja meneja wa kampuni ya biashara ya Aixin Bw. Shen Fucai, watu wanaomfahamu wote wanamsifu sana. Bw. Shen Fucai ni mtu asiyeweza kuona, lakini anapenda kuwasaidia watu wenye hali dhaifu. Katika miaka 6 iliyopita, siku zote anawasaidia walemavu wengine, watu wenye matatizo ya kiuchumi na watoto waliokosa masomo yao.

Bw. Shen Fucai ana umri wa miaka 57, na anaishi katika nyumba ndogo ambayo eneo lake halijatimia mita za mraba 50. Katika nyumba hiyo yeye na mkewe wanawapokea marafiki wao walemavu mara kwa mara.

Mwaka 1982, Bw. Shen Fucai alikuja mjini Baotou pamoja na mkewe na binti yake. Kutokana na kufanya kazi kwa bidii, Bw. Shen alikuwa mkuu wa kikundi cha ujenzi wa mradi cha kampuni ya ujenzi wa majengo ya biashara ya mji wa Baotou. Lakini kwenye ajali iliyotokea mwaka 1987, kipande cha kioo cha miwani yake kilichoma macho yake na kusababisha macho yake kutoweza kuona. Hivyo alikuwa mlemavu kutoka mtu wa kawaida. Baadaye Bw. Shen Fucai alijaribu kufanya biashara ndogo, lakini kutokana na kuwa mlemavu, alidanganywa kila mara alipofanya biashara. Wakati huo alifikiri kuwa, lazima afanye vizuri biashara, na kuwasaidia walemavu wengine.

Mwezi Julai mwaka 1997, Bw. Shen Fucai aliuza nyumba yake kwa Yuan za RMB 50,000, na baada ya kufanya juhudi kwa miezi kadhaa, alianzisha kampuni ya biashara ya Caifuda. Lakini kwa kuwa alikosa uzoefu wa kufanya biashara, kampuni yake ilikuta matatizo. Baadaye kutokana na misaada ya shirikisho la walemavu la mji wa Baotou, mwaka 2001 alibadilisha jina la kampuni yake kuwa kampuni ya biashara ya Aixin. Anataka kuwashirikisha walemavu wote kwa moyo wa upendo, ili wote wawe na maisha bora. Kwa kuwa yeye na wafanyakazi wake wanafanya kazi kwa bidii, na kufanya biashara kwa kufuata maadili, hivyo kampuni yake ilijikwamua tatizo la kiuchumi haraka.

Sasa Bw. Shen Fucai amekuwa mkuu wa kampuni hiyo yenye mitaji mingi, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hatasahau ufuatiliaji wa serikali kwake. Alisema,

"Mimi ni tofauti na wanaviwanda wengine, wao wanategemea uwezo wao, lakini kampuni yangu kweli inanufaika na sera nzuri ya serikali na misaada ya shirikisho la walemavu, hivyo baada ya kuchuma pesa, nyingi nitazirudisha kwenye jamii, ninatoa kodi zote, pia baada ya kutajirika, hatutasahau watu wote wenye hali dhaifu au walioko karibu nasi."

Aliahidi rasmi kwa shirikisho la walemavu la mji wa Baotou kuwa, katika siku zijazo akipata faida ya Yuan moja, atatoa senti 50 kuwasaidia watu wenye matatizo. Anafanya kama alivyosema. Mwaka 2002 alitoa Yuan za RMB 1,500 kumsaidia Bw. Luo Zhiqiang, ambaye alikuwa bingwa wa kunyanyua uzito wa Michezo ya Olimpiki ya walemavu, kuanzisha kituo cha utoaji mafunzo ya ukandaji wa walemavu.

Bw. Wang Zhongmei alikuja Baotou kutoka sehemu nyingine. Katika mkutano wa miaka kadhaa iliyopita, aliambiwa kuwa Bw. Shen Fucai ni mtu anayependa kuwasaidia wengine, hivyo alimtafuta Bw. Shen Fucai, na kutaka kupata msaada kutoka kwake. Bw. Wang alisema,

"Mkuu Shen aliniuliza kuwa ninataka kufanya nini? Nilimwambia nataka kuanzisha duka la chuma, unipe Yuan za RMB 2,000. Kisha nikaanzisha duka la chuma, hadi sasa, biashara ya duka hilo ni nzuri mwaka hadi mwaka. Bw. Shen alitoa msaada mkubwa kwangu. Yeye mwenyewe amepoteza uwezo wa kuona, lakini anafanya shughuli nyingi, jambo hilo linanitia sana moyo."

Mwaka 2007, Bw. Shen Fucai alitoa fedha kwa walemavu wengi mjini Baotou kufanya ukaguzi wa afya, na kununua bima za uzeeni na bima za kukosa ajira kwao, na kila mwaka atalipa gharama hizo. Pia alitoa fedha kuwasaidia wanafunzi maskini zaidi ya 120 wa mjini Baotou kumaliza masomo yao. Kuanzia mwaka 2002 hadi sasa, fedha zilizochangiwa na Bw. Shen Fucai kwa walemavu na watu maskini zimefikia karibu Yuan za RMB milioni 1.

Mwaka 2007 Bw. Shen Fucai alisifiwa kuwa "mtu wa kuigwa katika utoaji huduma kwa umma nchini China", na vyombo vingi vya habari vilitangaza mambo aliyofanya. Kuhusu heshima hiyo, Bw. Shen Fucai alisema, jambo linalomfurahisha ni kuwa, walemavu wale waliosaidiwa naye na kutajirika sasa pia wanafanya wawezavyo kuwasaidia wengine, hii ndiyo faraja kubwa kwake.

Kampuni ya Aixin ikiwa kampuni moja ya kuchangia huduma kwa jamii, inaweza kusamehewa kodi, lakini kila mwaka Bw. Shen Fucai alitoa kodi za Yuan za RMB zaidi ya laki 6 kwa taifa. Hadi sasa, kampuni yake ina wafanyakazi 50, miongoni mwao kuna wafanyakazi walemavu 32. Kampuni yake inaendelea kuwa kubwa mwaka hadi mwaka, Bw. Shen Fucai alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:

"Nataka kujenga idara ya kuwatunza wazee walemavu. Niliwaahidi walemavu 32 kuwa, siku moja nitakapozeeka, hakika wataweza kulipwa bima ya uzeeni."