Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-11 20:04:15    
Wimbo wa Michezo ya Olimpiki "Beijing"

cri

Wanamuziki wa Bendi ya The SMU ya Ujerumani walikuja Beijing wakiwa na wimbo wao uitwao "Beijing" walioutunga kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing 2008.

"Hamjambo wasikilizaji, mnayosikiliza ni idhaa ya Redio China Kimataifa CRI, sisi ni wa Bendi ya The SMU, ni matumaini yetu kuwa mtapenda wimbo wetu uitwao 'Beijing'. Tunaipenda China!"

Mliosikia ni wimbo uitwao"Beijing", huu ni wimbo uliotungwa na Bendi ya The SMU ya Ujerumani kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, wimbo huu wenye maudhui ya "Dunia Moja na Ndoto Moja" unagonga hisia za watu unapoimbwa na wanamuziki vijana kadhaa wa bendi hiyo kwa mtindo wa rock and roll.

Wimbo huu unaimbwa hivi, "Beijing, marafiki wakuzunguka pembezoni mwako. Wewe ni taa yangu inayong'ara, dunia yote iko moyoni mwako, wewe ni mali yangu yenye thamani."

Bendi ya The SMU ilianzishwa mwaka 2004, baada ya mwaka mmoja tu bendi hiyo imeshabikiwa na vijana wengi kutokana na mtindo wake wa rock and roll. Wanamuziki wa bendi hiyo ni vijana watano Daniel, Martin, Uli na Felix. Kwa kuunganisha muziki wa disco na muziki wa vijijini wa Ulaya na Marekani pamoja na sura za kupendeza za hao wanamuziki, bendi hiyo mara ikapendwa na watu wengi wenye rika tofauti.

Mwaka jana bendi hiyo iliwahi kutembelea miji mingine nchini China, hii ni mara ya kwanza kuja hapa Beijing. Kwa kuona jinsi Beijing ilivyo walishangaa na kufurahi sana kuja tena nchini China katika kipindi cha Michezo ya Olimpiki inapofanyika. Bw. Felix alisema,

"Hisia yangu ni tofauti na ya mwaka uliopita, sasa tuko mjini Beijing katika kijiji cha Olimpiki na kufanya maonesho ya muziki wetu kwa ajili ya wachezaji wa nchi mbalimbali tukisherehekea michezo ya Olimpiki pamoja na watu waliotoka nchi mbali mbali na watu wa China, tunaona furaha na fahari."

Wimbo uitwao "Beijing" ulikamilishwa kwa mwezi mmoja toka ulipotungwa mpaka kumalizika kurekodiwa. Lakini kwa nini bendi hiyo ambayo ni ya nchi ya nje ilitunga wimbo huo wa kuisifu Beijing? Mwanamuziki wa bendi hiyo Bw. Steve alisema,

"Tunataka kuonesha matumaini ya watu wote kwa michezo yetu ya Olimpiki kwa kuimba wimbo huu. Michezo ya Olimpiki ni tamasha la watu wote, maudhui ya wimbo wetu na kauli mbiu ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing 'Dunia Moja na Ndoto Moja' ni ya namna moja, ambayo imeoneshwa katika maneno ya wimbo huu. Toka tulipoanza kutunga mpaka kuukamilisha tulitumia mwezi mmoja, hili ni tunda la akili zetu za pamoja."

Wanamuziki wa bendi hiyo walimwambia kwa furaha mwandishi wetu wa habari kuwa bendi yao ina jina jingine la Kichina "Si Meng" yaani kufuatilia ndoto, jina hilo linatokana na matamshi ya jina la Kiingereza la bendi hiyo SMU. Hivi sasa wamekuja Beijing wakati wa michezo ya Olimpiki, ndoto yao imetimizwa, wanaona furaha mno.

Kuhusu kauli mbiu ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya "Dunia Moja na Ndoto Moja", mwanamuziki Daniel ana fikra zake, akisema,

"Michezo ya Olimpiki ni tamasha kubwa la watu wote, watu kutoka nchi zaidi ya 200 wamekusanyika kwenye michezo hiyo na wote wanatamani amani na maendeleo ya pamoja, hii ni ndoto ya kila mmoja. Wimbo wetu umeonesha matumaini ya 'Dunia Moja na Ndoto Moja' ."

Kama Bendi ya The SMU inavyoelewa kwamba dunia ni familia moja japokuwa inatofautiana kwa lugha na rangi za ngozi za watu, lakini muziki unafahamika kwa wote. Bendi ya The SMU licha ya kuwa imekuja China na wimbo wake uitwao "Beijing", pia imeiwezesha dunia kuifahamu China na China kuielewa dunia.

Wanamuziki wa Bendi ya The SMU wamesema wataendelea kutunga nyimbo kuhusu China na kuhusu Beijing, wanasema, wasingeweza kuja Beijing wasingeweza kujionea jinsi Beijing inavyopendeza. Kabla ya kipindi hiki kumalizika, tusikilize tena wimbo huu uitwao "Beijing".