Msuluhishi wa msukosuko wa kisiasa nchini Zimbabwe ambaye ni rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki tarehe 11 huko Harare alisema, makubaliano ya kugawa madaraka yamefikiwa kwenye mazungumzo kati ya vyama mbalimbali vya Zimbabwe, makubaliano hayo yatasainiwa rasmi tarehe 15 huko Harare, ambapo serikali ya umoja wa kitaifa ya Zimbabwe pia itatangazwa kuanzishwa.
Duru jipya la mazungumzo hayo lilifanyika kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 11 huko Harare, mji mkuu wa Zimbabwe. Kiongozi wa chama cha ZANU PF ambaye ni rais wa sasa wa Zimbabwe Robert Mugabe, kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC Bw. Morgan Tsvangirai, na kiongozi wa kundi jingine la chama cha MDC Arthur Mutambara pamoja na rais Mbeki ambaye ni msuluhishi aliyekabidhiwa jukumu hilo na Umoja wa maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC walihudhuria mazungumzo hayo.
Usiku wa siku hiyo ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, rais Mugabe alitoa hotuba kwa njia ya radio akiwatangazia watu wa nchi nzima habari hiyo kuhusu vyama mbalimbali vimefikia makubaliano ya kugawa madaraka, na serikali ya umoja wa kitaifa itaundwa.
Msemaji wa kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC Bw. Nelson Chamisa alisema, chama hicho kinafurahia matokeo ya kufikiwa kwa makubaliano kwenye mazungumzo. Alisema, kusainiwa kwa makubaliano hayo si kama tu ni habari nzuri kwa chama cha ZANU PF na chama cha MDC, bali pia ni habari ya kufurahisha kwa Zimbabwe nzima. Siku zijazo watu wa nchi nzima wataungana pamoja na kufanya juhudi kwa ajili ya maslahi ya taifa.
Msemaji wa kundi la Mutambara la chama cha MDC pia alipongeza kufikiwa kwa makubaliano kwenye mazungumzo, alisema hii imeonesha kuwa viongozi wa vyama mbalimbali wamezingatia kwanza maslahi ya taifa.
Msuluhishi wa msukosuko wa kisiasa wa Zimbabwe ambaye ni rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki alisema, vyama mbalimbali vya Zimbabwe vimefikia makubaliano ya kugawa madaraka na kukomesha msukosuko wa kisiasa, hii inategemea uungaji mkono wa Umoja wa SADC, nchi mbalimbali za bara la Afrika na nchi nyingi duniani, ni uungaji huo ambao uliiwezesha Zimbabwe ijikwamue jangani.
Wachambuzi wanaona kuwa, kutokana na hali ya hivi sasa, kiongozi wa chama cha upinzani MDC Morgan Tsvangirai atapata madaraka zaidi kwenye serikali ya awamu mpya, huenda atadhibiti madaraka ya usalama wa nchi. Kabla ya hapo Bw. Tsvangirai aliwahi kusema, kamwe hatasaini kwenye makubaliano ambayo hatapata madaraka halisi. Na suala kuhusu udhibiti wa nguvu za usalama za Zimbabwe lilikuwa suala kubwa kwenye mikwaruzano ya pande mbalimbali katika mazungumzo.
Wachambuzi wameona kuwa, makubaliano ya kugawa madaraka yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya vyama mbalimbali vya Zimbabwe yatakomesha kimsingi msukosuko wa kisiasa uliosababishwa na uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu, Zimbabwe inatazamiwa kushinda taabu kubwa zinazoikabili hivi sasa chini ya hali tulivu ya kisiasa, ambapo itafanya ujenzi wa mambo ya uchumi na kuinua kiwango cha maisha ya wananchi. Aidha, kufikiwa kwa makubaliano hayo ya kugawa madaraka pia kunasaidia amani na utulivu wa kusini mwa Afrika. Lakini wachambuzi wamesema pia, baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya kugawa madaraka, chama tawala na chama cha upinzani kama vitaweza kuishi kwa masikilizano na kutendeana kwa usawa ili kujadili mambo makuu ya nchi na kutuliza hali ya kisiasa au la, hii bado inafuatiliwa na watu.
|