Katika mwisho wa juma lililopita, kimbunga"Ike" kilikumba sehemu ya pwani jimboni Texas, Marekani na kusababisha vifo vya watu 9 pamoja na hasara kubwa. Shughuli za uokoaji ambazo ni kubwa zaidi katika historia ya jimbo hilo zimeanza, na maofisa wa huko walikadiria kuwa, itachukua muda mrefu kabla ya maisha kurejea katika hali ya kawaida.
Kimbunga Ike alfajiri ya tarehe 13 kilivuma kwenye majimbo ya Texas, Louisiana na Arkansas, ambapo kasi ya upepo ilifikia kilomita 170 kwa saa. Maofisa wa huko waliripoti tarehe 14 kuwa, mji wa Galveston ulioko kwenye rasi ya ghuba jimboni Texas ulikumbwa na hasara kubwa zaidi, ambapo maji yalifurika mjini, nyumba zilibomoka, na huduma za umeme, gesi na mawasiliano zote zilikatika. Hivi sasa waokoaji wanaangalia kutoka nyumba moja hadi nyingine kuwatafuta watu waliokwama ambao walikuwa wakikataa kuondoka kabla ya maafa hayo. Habari zinasema kuwa, watu zaidi ya elfu 2 wameokolewa. Meya wa mji huo alisema, itachukua miezi kadhaa kabla ya shughuli za huko kurejea katika hali ya kawaida.
Kimbunga Ike pia kiliukumba mji wa Houston ambao ni mji wa nne kwa ukubwa nchini Marekani, ambapo shule na shughuli za biashara zilisimamishwa, uwanja wa ndege ulifungwa na watu zaidi ya milioni 4 kuathirika kutokana na kukatika kwa huduma za umeme. Kwa sababu ya tatizo la umeme, mji huo ulipaswa kutekeleza amri iliyopiga marufuku kutembea nje kuanzia saa 3 usiku mpaka saa 12 asubuhi katika kipindi cha wiki moja. Sehemu ya katikati ya mji wa Houston pia ilikumbwa na hasara kubwa, ambapo madirisha ya jengo la kampuni ya JP Morgan lenye urefu wa mita 300 yalivunjika, vitu vya ofisini vikiwemo kompyuta, meza na viti vikasambaa hapa na pale barabarani. Mbali na jimbo la Texas, kimbunga Ike pia kiliharibu mamia ya nyumba jimboni Louisiana, ambapo watu wa familia karibu laki 2 walikuwa hawana umeme.
Kabla ya kutokea kwa kimbunga Ike, watu wapatao milioni 2.2 walihamishwa kutoka sehemu ya pwani ya jimbo la Texas, hata hivyo baadhi ya watu waliamua kubaki nyumbani. Rais George W. Bush wa Marekani tarehe 13 alizitangaza wilaya 29 za jimbo la Texas kuwa ni eneo la maafa, ambapo yeye anatarajiwa kutembelea jimbo hilo tarehe 16 na kuwapa pole waathirika wa maafa hayo. Vile vile rais Bush aliwaomba watu waliohamishwa wasirudi nyumbani wakati huu, na badala yake wasubiri mpango wa serikali. Waziri wa usalama wa ardhi wa Marekani Michael Chertoff tarehe 13 alikwenda jimbo la Texas kusimamia kazi ya uokoaji, nae alisema serikali ya Marekani ilituma waokoaji 3,500 na kutoa chakula cha seti milioni 2.4 na mitambo 200 ya kuzalisha umeme ili kuwasaidia wakazi waliokwama.
Wadau wa sekta ya bima wamekadiria kuwa, hasara zilizosababishwa na kimbunga Ike zitakuwa kati ya dola za kimarekani bilioni 8 na bilioni 18, maafa hayo yatakuwa mabaya zaidi kutokea katika miji yenye msongamano mkubwa wa watu baada ya kutokea kwa kimbunga Katrina mwaka 2005. Zaidi ya hayo kimbunga Ike kilisababisha robo ya visima vya mafuta na gesi nchini Marekani kusimamisha uzalishaji. Hata hivyo maofisa wa huko walisema, kimbunga Ike hakikupita kwenye sehemu yenye viwanda vingi vya kutengeneza mafuta jimboni Texas, kwa hiyo athari zake kwa uzalishaji wa mafuta ni ndogo zaidi kuliko makadirio ya awali.
|