Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-16 16:46:55    
Vyama mbalimbali vya Zimbabwe vyasaini makubaliano ya ugawaji wa madaraka

cri

Viongozi wa vyama mbalimbali vya Zimbabwe tarehe 15 huko Harare walisaini makubaliano ya ugawaji wa madaraka na kutangaza kuunda serikali ya maafikiano ya taifa. tukio hilo ni alama ya kuelekea kumalizika kwa mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Machi nchini humo, na Zimbabwe imeingia kwenye kipindi kipya cha utawala wa pamoja wa vyama viwili.

Kwa mujibu wa makubaliano ya ugawaji wa madaraka, serikali hiyo mpya inaundwa kwa pamoja na chama cha ZANU-PF (Zimbabwe African National Union-Patriotic Front) ambacho ni chama tawala cha nchi hiyo na chama cha MDC (Movement for Democratic Change), na madaraka yanagawanyika kwa usawa. Kiongozi cha chama tawala Bw. Robert Mugabe ataendelea kushika wadhifa wa urais na kudhibiti mamlaka ya jeshi la nchi hiyo; kiongozi cha chama cha upinzani Bw. Morgan Tsvangirai atakuwa waziri mkuu wa nchi hiyo na kuongoza baraza la mawaziri na idara za usalama wa taifa zikiwemo polisi na kikosi cha upelelezi. Bw. Tsvangirai atawajibika na kazi za usimamizi wa uchumi na jamii ya nchi hiyo.

Imefahamika kuwa, chama cha ZANU-PF kinachukua viti 15 na chama cha MDC kinachukua viti 13 katika baraza la mawaziri, kundi jingine la Arthur Mutambara la chama cha MDC linachukua viti 3 katika baraza hilo.

Msuluhishi wa mgogoro wa siasa wa Zimbabwe ambaye ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC Bw. Thabo Mbeki, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye ni rais wa Tanzania Bw. Jakaya Kikwete, na viongozi wa nchi na sehemu za Afrika ya kusini zikiwemo Botswana, Swaziland, Namibia na Zambia walihudhuria na kushuhudia sherehe ya kusaini makubaliano hayo.

Bw. Mbeki alisema, kusainiwa kwa makubaliano hayo na kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa hakumaanishi kukomoshwa kwa mgogoro huo, na hatua inayofuata inapaswa kuweka mkazo katika kuhimiza ushirikiano mapema kati ya vyama hivyo viwili. Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika rais Kikwete wa Tanzania pia alisema, ingawa makubaliano ya ugawaji wa madaraka yamesainiwa, lakini suala la hivi sasa la Zimbabwe bado linakuwepo. Viongozi hao wote walisema, kusainiwa kwa makubaliano hayo ni jambo la kufurahisha, ambalo limethibitisha tena kuwa mambo ya Afrika yanapaswa kutatuliwa na waafrika wenyewe, na pia limeweka mfano mzuri na kutoa uzoefu kwa utatuzi wa migogoro ya kikanda kama huo.

Wachambuzi wanaona kuwa, kusainiwa kwa makubaliano hayo ni mwanzo tu wa utatuzi wa masuala ya siasa na uchumi nchini Zimbabwe, masuala mengi ya kisiasa, kiuchumi, kidiplomasia na kijamii yanayokuwepo nchini humo yanahitaji kutatuliwa kwa ushriikiano wa pamoja wa vyama hivyo viwili katika muda mrefu ujao. Hii pia ni changamoto kwa utaratibu mpya wa utawala wa pamoja wa vyama viwili.

Wachambuzi pia wanaona kuwa, katika serikali ya muungano iliyoanzishwa kwa mujibu wa makubaliano ya ugawaji wa madaraka, chama tawala na chama cha upinzani ambavyo madaraka yanagawanyika kwa usawa kabisa huenda vitakuwa na hali ya mvutano katika kazi za baadaye, hatimaye hali hiyo itaathiri uwezo wa kutawala wa serikali hiyo. Aidha katika utaratibu ambao Bw. Mugabe anadhibiti mamlaka ya jeshi na Bw. Tsvangirai kuongoza polisi, kama mgogoro ukilipuka tena katika vyama hivyo viwili, utasababisha matokeo mabaya zaidi.