Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-16 20:04:08    
Barua 0916

cri

Msikilizaji wetu Mchana J. Mchana wa Morogoro Tanzani ametuletea barua pepe akisema, anapenda kuungana na wananchi wa China kwenye ufunguzi wa Michezo ya Olmpiki na kuahidi kuwa siku ya ufunguzi wasijione wapo upweke bali wajione wenye amani na upendo kwani yeye kama mchana tayari amechukua likizo ili kuungana na wenzake walioko viwanja vya Michezo ya Olimpiki akifuatilia kupitia televisheni matangazo ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Anaitakia heri na Baraka michezo hiyo.

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai United Arab Emirates ametuletea barua pepe akisema kuwa, ni matumani yake kuwa sote hatujambo hapa tuliko, kwanza kabisa angependa kutoa shukrani zake za dhati kwa uwongozi wote wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI kutokana na zawadi nzuri kama ni tuzo la kuchaguliwa kuwa miongoni mwa washindi wa nafasi ya kwanza katika Chemsha Bongo "Tukutane Beijing 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki ", kwa kweli ametiwa moyo sana na ushindi huo katika kushiriki mara kwa mara kwenye chemsha bongo za CRI kila mwaka.

Anasema pia anachukua nafasi hii kuipongeza Jamhuri ya Watu wa China kwa kufanikisha vyema Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 , ambayo ilimalizika hivi karibuni na cha kusisimuwa zaidi ni ushindi mkubwa wa medali za dhahabu iliyojinyakulia Jamhuri ya Watu wa China katika Michezo hiyo kutokana na umahiri, ari, nguvu na juhudi kubwa za wanamichezo wake katika ulingo huo ili kulipatia taifa lao sifa kubwa mbali na kuwa waandalizi wa michezo hiyo.

Bw. Mbarouk anasema kwa kweli yeye binafsi alisisimka sana kwa jinsi gani michezo ya Olimpiki mjini Beijing ilivyojaa shamrashamra na ufanisi wa hali ya juu kabisa kutokana na maandalizi makubwa na ya muda mrefu yaliyoandaliwa ili kulikaribisha tamasha hilo adhimu la Michezo hapa duniani Hongereni sana rafiki zangu wa China !!!.

Tunawashukuru kwa dhati Mchana J. Mchana na Mbarouk Msabah kwa barua zao za kufuatilia na kupongeza Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 iliyofanyika mjini Beijing, kweli safari hii marafiki wengi wa Afrika wamefurahia zaidi na kupongeza kwa dhati Beijing kufanikiwa kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008. Kwenye michezo hiyo pia tumeona wanamichezo wengi wa Afrika wamefanya juhudi kubwa na kupata medali kwenye mashindano ya michezo mbalimbali hasa mchezo wa mbio, sisi pia tunafurahia sana na kuwapongeza kwa dhati.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub S. Shariff wa sanduku la posta 72, Bungoma Kenya ametuletea barua pepe akisema, tupokee salamu kutoka kwake hapo mjini Bungoma. Ni muda sasa tangu atuandikie barua pepe. Anasema ni hakika kuwa tunafikiria labda kuna shida. La hasha, angependa kutufahamisha kuwa yeye ni mzima na anaendelea kuchapa kazi vizuri licha ya kuwa na shida hapa na pale. Ana matumaini kuwa nasi twaendelea vizuri kuchapa kazi vilivyo. Natumia fursa hii pia kuwashukuru Wasikilizaji wote ambao wameendelea kutuma barua pamoja na kadi za salamu hii yote imechangia sana kuiendeleza idhaa ya CRI, angependa kuwasihi tuendelee vivyo hivyo.

Bw. Shariff anasema, angependa kutoa maoni yake kuhusu michezo ya Olimpiki iliyomalizika juzi, kwa kinaga ubaga hana maneno ya kutuelezea vile ambavyo sherehe ya ufunguzi wa michezo hiyo ilivyokuwa. Aliweza kuvutiwa na wachezaji ngoma, vinanda pamoja na dansi walipozunguka ndani ya kiota. Yote yalikuwa kama ni mwanzo wa miujiza ulimwenguni. Hataweza kusahau jinsi ambavyo wasichana warembo walivyoweza kuzunguka kwenye uwanja wa Kiota wakionyesha alama ya mnyama dragon. Ilikuwa ya kuvutia sana watazamaji wengi kutoka nchi nyingi kote ulimwenguni. Hayo yote yalithibitisha jinsi China ilivyokuwa imejiandaa kwa ajili ya michezo hii. Jambo ambalo anaweza kusema sasa ni kuwa China iliweza kuvunja rekodi kwa michezo mingi duniani ambayo ameweza kutazama na kusikia. Sifa zote anaipa kamati ya mandalizi ya Olimpiki 2008 ya Beijing. Kwa kweli walifanya kazi nzuri sana.Vilevile timu ya China iliweza kufanya vyema sana kwa kunyakuwa medali nyingi sana ikifuatwa na Marekani. Shukurani zake pia ni kwa timu za Africa haswa Kenya na Jamaica Kwa kuonesha umaarufu wao katika mchezo wa riadha.Vijana wa nyumbani Kenya kwa kweli walivutia na kufurahisha watu wengi siku ya mwisho.

Kulingana na matarajio ya wengi wakiwemo wageni mashuhuri, wachezaji, mashabiki, na watali kwa jumla ambao walikuwa na hofu ya kutokuweko kwa usalama katika maeneo ya michezo. Pongezi kwa serikali ya China kwa kuhakikisha kuwa kuna usalama wa kutosha. Na hali ya sifa ya hewa mjini Beijing vilevile ilikuwa ni nzuri mpaka siku ya mwisho ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing.

Bw. Shariff anasema, sasa macho yote kwenye televisheni yanafuatilia tena Michezo ya Olimpiki ya walemavu. Kulingana na maandalizi mema hana budi kusema kuwa michezo hiyo itakuwa ya hali ya juu. Shukurani zake ni kwa timu ya Kenya kwa matumaini waliyonayo

Kulingana na vile walivyohojiwa na idhaa ya Radio China Kimataifa juzi pamoja na kocha wao wana matumaini makubwa sana. Mmoja wao alisema, kulingana na mazingira ambayo anayaona kule Beijing medali ameshaiweka mfukoni tayari. Ana furaha na kumuombea ushindi mchezaji huyo pamoja na wenzake.

Na Bw. Shariff anasema, angependa kuchukuwa fursa hii kuwapa pongezi wote walioshiriki kwa mashindano ya chemsha Bongo Tukutane Beijing2008. Anawashukuru wale waliopata nafasi ya kwanza, nafasi ya pili na nafasi ya tatu. kama vile Bw.Mbarouk Msabah Mbarouk wa Dubai, Bw.Mogire Machuki wa Kisii-Kenya, Bw.Ras Franz Mango Ngongo wa Tarime-Mara-Tanzania, Bw.Xavie Telle-Wambwa wa Bungoma-Kenya pamoja na yeye Bw Mutanda Ayub Shariff wa Bungoma-Kenya.Vilevile anawapa heko walioweza kujitokeza kwa mara ya kwanza kama vile Edward Kavai Abuogi-kitale Kenya, Gabriel Simiyu Wekesa wa Kimilili Kenya, Martin Wekesa Wanyama wa Bungoma Kenya, Omari Idi wa Thika- Kenya, Okongo Okeyo wa Iganga-uganda, Dominic Nduku Muholo wa Kakamega Kenya, Patrick Kangae wa Nairobi Kenya, Paston Gunyanyai wa Maragoli-Kenya na wengine wote asioweza kuwatambua kwa sasa. Hata hivyo siwezi kukosa kumshukuru Mzee John Stephen Akhwari aliyealikwa kama mgeni rasmi kwa kuwa shujaa wa Olimpiki wa Tanzania.

Anasema, kama inavyokuwa kwa mashindano yaliyopita ama kulingana na desturi ya Radio China Kimataifa kila baada ya kumalizika kwa mashindano, baadaye kamati ya uthibitishaji huchagua wasikilizaji washindi wa nafasi ya kwanza, pili na tatu pamoja na nafasi maalumu ambavyo imefanya mwaka huu. Hatimaye hawa washindi wote hutuzwa kwa kutumiwa vyeti pamoja na zawadi kulingana na uwezo wa idhaa ya Radio China Kimataifa. Hii kweli huwa inawatia moyo wasikilizaji waweze kushiriki wakiwa na lengo ya kutuzwa pamoja na kufahamu mengi kuhusu CRI. Lakini kwa mwaka huu hajui ni kwake pekee au kwa wasikilizaji wengine. Licha ya kupata habari kuwa alifanikiwa kuwa katika nafasi ya kwanza mpaka leo hajapata chochote kutoka kwa cri ila tu kadi za salamu na maswali Mengine ya chemsha Bongo kuhusu ujuzi wa vivutio vya utali mkoani Guangxi,China. Hata hivyo ataendelea kushiriki ili kufahamu mengi. Kwani mwito na lengo kuu ni kuimarisha uhusiano na Radio China Kimataifa na wachina kwa jumla.

Tunamshukuru kwa dhati Bw. Mutanda Ayub S. Shariff barua yake iliyotuelezea mengi kuhusu Michezo ya Olimpiki ya Beijing, pongezi zake kwa China kufanikiwa kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, furaha aliyonayo kuhusu wanamichezo wa Kenya na Jameca waliopata medali za dhahabu kwenye mchezo wa mbio, alisema Vijana wa nyumbani Kenya kwa kweli walivutia na kufurahisha watu wengi siku ya mwisho ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing ilipofanyika, kila tulipoona wanamichezo wa Afrika walionyakua medali kwenye mashindano, kweli tulifurahi sana. Na kuhusu zawadi ya Chemsha bongo ya mwaka jana, tunadhani Bw. Shariff atapata bila shaka lolote. Labla kutokana na sababu ya posta, kutumia zawadi kwa njia ya posta kunahitaji muda. Mhusika wa ofisi yetu hakika ameshawatumia wasikilizaji wetu watakaopata zawadi mbalimbali.