Mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 16 ulifunguliwa katika makao makuu ya umoja huo huko New York. Mwenyekiti mpya wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa Bw. Miguel d'Escoto Brockman aliyekuwa waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Nicaragua kwenye ufunguzi wa mkutano huo alieleza matumaini yake kuwa baraza kuu la awamu hii la Umoja wa Mataifa litakuwa baraza lenye udhati na kufanya kazi kwa juhudi kwa ajili ya kutimiza amani na kutokomeza umaskini na njaa duniani.
Bw. Brokman alipotoa hotuba alitaja baadhi ya changamoto kubwa zinazoikabili dunia zikiwa ni pamoja na njaa na umaskini, bei kubwa ya chakula na mafuta, mageuzi ya Umoja wa Mataifa, mabadiliko ya hali ya hewa, upungufu wa maliasili ya maji, ugaidi, haki za bianadamu, kukinga ueneaji wa silaha za nyuklia, utoaji wa misaada ya kibinadamu, usawa wa kijinsia, n.k., na changamoto hizo pia ni masuala ambayo Umoja wa Mataifa unapaswa kuyakabili na kuyatatua. Na hasa alitaja jukumu la mkutano huo ambalo ni kuufanya Umoja wa Mataifa uwe wa kidemokrasia zaidi, kwani kufanya hivyo ndipo Umoja wa Mataifa utakapoweza kuyakabili masuala hayo kwa ufanisi zaidi. Alisema:
"Umoja wa Mataifa una wajibu na majukumu ya kupambana na changamoto hizo. Kazi kuu ya mkutano huu ni kuufanya Umoja wa Mataifa uwe wa kidemokrasia zaidi. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo tutakapoweza kuhakikisha Umoja wa Mataifa unaendelea kuwa na hadhi isiyoweza kukosekana mioyoni mwa watu wa dunia katika juhudi za kupigania amani na usalama."
Bw. Brockman alizitaka serikali zote ziwe na nia thabiti na ushupavu zaidi katika kazi ya kutokomeza umaskini na njaa, anaona kwamba katika suala hilo nchi zote zinapaswa kuvuka mipaka yao na kushirikiana pamoja ili kutoa misaada kwa watu wanaohitaji. Alitoa wito wa kuwaunga mkono wale watu wasioweza kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuzitaka nchi zote ziwe na nia ya kisiasa ya kweli kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoathiri dunia nzima.
Aidha, Bw. Brockman alisema mkutano huo utaendelea kujadili kuhusu chanzo cha kusababisha msukosuko wa chakula duniani ili kupata utatuzi wa msukosuko huo. Alisema,
"Wakati wa mkutano wa 63 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, tutajadili sababu za moja kwa moja na za kimsingi za msukosuko huo wa chakula na athari kubwa za namna gani zilizosababishwa na msukosuko huo katika masuala ya umaskini na njaa duniani. Kwa hiyo nakaribisha jumuyia zisizofungamana na upande wowote kupendesha kuitisha mkutano kuhusu usalama wa chakula wakati wa kufanyika kwa mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa."
Bw. Brockman ni padri wa Katoliki na amekuwa padri wa kwanza aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, na hotuba yake pia ni tofauti na nyingine zilizotolewa na kwenye ufunguzi wa mkutano wa baraza kuu hilo la awamu zilizopita. Kwenye mwisho wa hotuba yake alisisitiza zaidi matumaini yake akisema:
"Ni matumaini yangu kwamba Baraza kuu la awamu hii la Umoja wa Mataifa litakuwa baraza kuu lenye udhati, tutafanya juhudi kwa ajili ya kutimiza amani na kutokomeza umaskini na njaa duniani. Lakini kama Umoja wa Mataifa usipokuwa na msimamo imara ulio wazi, hautaweza kuyashughulikia kwa ufanisi masuala hayo sugu na yanayotakiwa kutatuliwa haraka."
Kabla ya mkutano huo kumalizika, bendi yenye watu wanne walialikwa kupiga muziki, na hii pia ni nadra kutokea katika ufunguzi wa mkutano kama huo. Kutokana na mabadiliko hayo mapya pengine watu wataamini kwamba mkutano huo utaleta hali mpya ya kazi za Umoja wa Mataifa.
|