Mkutano wa pili wa Baraza la Tokyo-Beijing ulifungwa tarehe 17 huko Tokyo, nchini Japan. Mkutano huo wa siku nne uliwashirikisha wajumbe 110 kutoka sekta mbalimbali za China na Japan, na masuala mengi zaidi yalijadiliwa.
Baraza hilo lilianzishwa na kufadhiliwa kwa pamoja na Gazeti la China Daily na Shirika lisilo la kibiashara la utoaji maoni la Japan, nalo linafanya mkutano kila mwaka kwa zamu nchini China na Japan. Baraza hilo sasa limetoa jukwaa kwa wananchi wa China na Japan kuwasiliana tangu lianzishwe mwaka 2005, ingawa majukwaa ya namna hili bado ni machache kwa hivi sasa. Lengo la baraza hilo ni kusukuma mbele maingiliano ya kirafiki kati ya wananchi wa China na Japan, na kutoa nafasi ambayo wataalamu wa kisiasa, kiuchumi, kitaaluma na kiutamaduni kutoka nchi hizo mbili kuweza kujadiliana kwa uwazi.
Kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, uchunguzi wa maoni ya wananchi wa China na Japan ulifanyika kwa mara ya nne kabla ya kufunguliwa kwa mkutano wa mwaka huu. Matokeo ya uchunguzi huo yanaonesha kuwa, wananchi wa China na Japan wametambua kuwa, uhusiano kati ya nchi hizo mbili ni muhimu sana kwa kila upande, lakini masuala yaliyopo hivi sasa ni kutokuwepo kwa maelewano ya kutosha, na bado haijaanzisha msingi imara katika uhusiano kati ya China na Japan. Kwa mfano watu wa nchi hizo mbili wanaona, kutokana na kutembeleana kwa viongozi wa nchi mbili katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, uhusiano kati ya nchi hizo mbili uliboreshwa kidhahiri, lakini maoni tofauti bado yapo kidhahiri. Asilimia 74.9 ya watu wa China walioulizwa waliona uhusiano kati ya China na Japan uliboreshwa katika mwaka mmoja uliopita, ambalo ni ongezeko la asilimia 16, lakini kwa upande wa Japan, watu wenye maoni ya namna hii wanachukua asilimia 25.2 tu, japokuwa idadi hiyo iliongezeka kwa asilimia 6.1 kuliko mwaka 2007.
Kuhusu matokeo ya uchunguzi huo, ajenda kuu ya mkutano huo iliamuliwa kuwa "mustakabali wa Asia na kazi za China na Japan". Mkutano huo uliwaalika wataalamu kutoka nchi hizo mbili washiriki kwenye mijadala inayohusu mambo ya pande 7 zikiwemo siasa, vyombo vya habari, mambo ya mikoa, usalama, mazingira, usalama wa chakula na uchumi.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa kabla ya kufungwa kwa mkutano huo inasema, watu wakiweza kukabiliana moja kwa moja na masuala yaliyopo kwenye uhusiano kati ya China na Japan na masuala yanayohusu mustakabali wa Asia, wakiweza kuheshimiana na kujitahidi kutafuta ufumbuzi wa masuala, hakika wanaweza kutoa mchango wa kihistoria katika kuhimiza uboreshwaji wa uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Taarifa hiyo pia inaeleza nia ya kuliendeleza zaidi baraza hilo na kulibadilisha kuwa jukwaa la mazungumzo kuhusu mambo ya Asia na hata ya dunia nzima. Baraza hilo limetoa mchango katika kuboresha uhusiano kati ya China na Japan, na watu wa nchi hizi mbili wametambua umuhimu wa uhusiano huo kwa kila upande. Pande hizo mbili zinapaswa kukuza zaidi uhusiano unaoungwa mkono na wananchi wengi zaidi na watu wa hali mbalimbali, ili wananchi wa nchi hizo mbili waweze kushirikishwa kwa wingi kwenye mjadala kuhusu uhusiano kati ya China na Japan.
Wachambuzi wanaona, wakati uhusiano kati ya China na Japan unapozidi kuboreshwa, kazi muhimu ya kwanza kwa hivi sasa ni kuimarisha hali ya kuaminiana kati ya watu wa nchi hizi mbili. Ila tu kufanya uratibu na ushirikiano katika ngazi za serikali, umma, na vyombo vya habari, ndipo itaweza kuondoa mikwaruzano na kuongeza maelewano na uaminifu kati ya watu wa China na Japan.
|