Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-22 16:46:53    
Ziwa Houhai ni mahali pazuri pa mapumziko

cri

Kama utafika Beijing, Ziwa Houhai ni mahali ambapo usikose kupatembelea. Sehemu hiyo ni sehemu ya makazi inayostawi sana mjini Beijing. Ingawa sehemu hiyo ni yenye shughuli nyingi, lakini watu wanaweza kupata mahali pasipo na kelele, huko ni makazi ya jadi ya wenyeji wa Beijing, ambayo mambo ya kisasa yameungana na mambo ya jadi.

Houhai pia inaitwa Shichahai, iko kwenye sehemu ya katikati ya Beijing, umbali wa kilomita kadhaa tu kutoka uwanja wa Tiananmen, sehemu hiyo inaungana na Ziwa Beihai, na inatazamana kwa mbali na Mlima Jing na majumba ya wafalme wa zama za kale. Ziwa Houhai lilikuwa la ukoo wa mfalme. Toka karne ya 13 sehemu hiyo ilianza kustawi kutokana na shughuli za biashara mjini Beijing. Sehemu hiyo ni mahali panapounganisha Beijing ya kale na Beijing ya zama za hivi sasa na penye mgongano kati ya utamaduni wa kale wa mashariki na utamaduni wa zama za hivi sasa wa magharibi. Endapo unafika huko katika nayakati za alasiri au usiku, hukosi utaona mambo ya kuvutia.

Wakati giza inapoingia, taa za neon zinawaka, uzuri wa

Ziwa Houhai unaonekana kwa taratibu. Kuna baa nyingi kwenye kandokando ya ziwa, na kila moja ina umaalumu wake, na zinatofautiana kwa mazingira, mapambo, chakula na vinywaji. Baa nyingine ni zenye shamrashamra ya furaha na baadhi yao ni zisizo na kelele, na kila baa ina mazingira yake ya kipekee. Unaweza kujiburudisha kwa chai ya huko, huku ukiangalia maua ya yungiyungi ya ziwani.

Yamewekwa makochi ya raha kwenye baa moja iliyoko katika kando ya kushoto ya ziwa. Baada ya chakula cha mchana, watu wanaona starehe sana kama wanakaa karibu na dirisha lenye mwangaza wa jua pamoja na marafiki zao. Baada ya kufungua mlango wa rangi ya buluu wenye umbo la ua la yungiyungi, utaweza kusikia harufu nzuri ya mapapai ya Thailand. Watumishi wote wa baa hiyo wanavaa mavazi ya kithaland. Wanatabasamu kwa wageni huku wakikutanisha viganja viwili kifuani kwa kutoa heshima, ambapo wageni wanasikia furaha nyoyoni.

wakati wa usiku chini ya mbalamwezi, marafiki walikaa kwenye ghorofa ya baa inayoitwa Jiadingerfang wakisikiliza muziki uliopigwa kwa vinanda vya kichina kwenye mashua, kuangalia taa za sanaa zenye maumbo ya maua ya yungiyungi. Watu wanapiga soga, kujiburudisha kwa vinywaji na mvivyo. Fundi wa kuchanganya vinywaji wa baa hiyo, Bw. Yao Bin alisema,

"Vinywaji vingi vinachanganywa pamoja, watu wanapata radha mbalimbali. Wachina wanapenda kupata kwanza mwonjo wa uguadu, kisha mwonjo wa tamu na kufuatiwa na uchungu. Kwa hiyo kuchanganya aina nyingi za vinywaji ni kazi yenye ufundi mkubwa."

Kutoka kwenye baa, unaweza kupata chakula katika mkahawa wenye umaalumu au mkahawa mdogo wa kawaida.

Mkahawa unaoitwa "Kaorouji" ni mkahawa wa miaka mingi unaouza chakula cha kiislamu ulioko kwenye kando ya daraja la Yinding. Chakula cha mgahawa huo ni kizuri sana, tena walaji wanaweza kula huku wakijiburudisha kwa mandhari ya huko na kuangalia watu waliokuwa wakipita pale.

Kuna migahawa mingi kwenye barabara nyembamba iitwayo Yangfang, iliyoko katika eneo la makazi. Jambo linaloshangaza watu ni kuwa wateja hawaruhusiwi kuchagua vitoweo, kila siku mgahawa unatoa menu yake, wageni wanakula vitoweo vilivyopangwa katika mpango, awe mtu mashuhuri au ni rais wote wanapaswa kufuata mpango wa mgahawa. Mandhari ya kando la ziwa Xihai yenye madaraja madogo, mito, wakazi wa sehemu ya kusini, ustadi wa chai, chakula kwenye mashua ili kupatanisha chakula na muziki.

Licha ya vyakula vya aina nyingi vya Kibeijing vinavyowafanya watu kumezea mate, pia naweza kutembelea vichochoro kwa baiskeli yenye magurudumu matatu na kuangalia wa makazi yenye mtindo wa jadi wa Kibeijing yaani nyumba zenye ua wa mraba, au nyumba za zamani walizoishi watu mashuhuri.

Bw. Dai Hongzhang mwenye umri wa miaka 68 ni mwendeshaji wa baiskeli yenye magurudumu matatu katika eneo hilo, alizaliwa na kukua katika nyumba ya kichochoroni na sasa anaendelea kukaa kwenye nyumba. Bwana huyo anapenda sana maisha ya kichochoroni, alisema hadithi za vichochoroni ni nyingi. Alisema,

"Ninawakaribisha myashuhudie maisha ya vichochoroni, ni maisha halisi ya wakazi wa Beijing, na kuhisi mwenyewe maisha katika nyumba zenye ua wa mraba mjini Beijing au kutembea tembea vichochoroni hapa Beijing."

Kwenye Ziwa Houhai pia kuna maduka mengi yasiyo ya kawaida.

Barabara ya Yan Dai Xie Jie ni barabara finyu yenye historia ya miaka zaidi ya mia moja. Kwa maana ya Kichina, jina la barabara hiyo lina maana ya kiko, kwani hapo zamani biashara kwenye barabara hiyo ilikuwa ni kuuza viko vya tumbaku, lakini sasa kumekuwa na maduka ya aina mbalimbali ya kushonea nguo, kuuzia vitu vya kale, na duka la kinyozi. Ukikaa kwenye baa lenye vinywaji vya kisasa na vya zamani unaweza kusikia wafanyabiashara wadogo kunadi biashara yao na wazawa wa Beijing wanavyosalimiana wanapokutana, au uingie ndani ya duka dogo uchague chupio ya nywele unayopenda.

Duka la "Jicho la Peponi" ni duka dogo linalouza mapambo ya Kitibet. Mwenye duka hilo Bw. Nimazamche alisema, anapenda sana sehemu ya Ziwa Houhai kwa sababu mazingira ya huko ni yasiyo na kelele na ni nadra kupatikana mahali pengine mjiniBeijing. Alisema,

"Barabara ya Yan Dai Xie Jie ni moja ya barabara za zamani sana mjini Beijing, kwa hiyo utamaduni wa kale wa mji huo pamoja na utamaduni wa makabila unafaa kuwepo kwenye barabara hiyo."

Pambezoni mwa Ziwa Hou Hai kuna wasanii wengi wa kienyeji, watalii wanaweza kuona jinsi msanii anavyotengeneza sanamu za wanyama wadogo kwa kupuliza kidonge cha mchanganyiko wa unga na sukari. Kwanza msanii anasugua sugua kidonge kilicho bado ki moto kwenye kiganja kwa kidole gumba na kukifanya kiwe tupu ndani, kisha anapuliza kutoka kitundu kwa mrija huku anavuta vuta na dakika chache akapata sanamu za mnyama mdogo kama kuku, panya na tunguri, watoto wanapoona humlilia mama kuwanunulia.

Idhaa ya kiswahili 2008-09-22