Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-22 18:17:36    
Rais Thabo Mbeki ajiuzulu na siasa nchini Afrika Kusini kuingia katika awamu mpya

cri

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini alitangaza kujiuzulu usiku wa tarehe 21 alipohutubia taifa kwa kupitia televisheni. Kwenye hotuba yake, alikanusha madai kwamba aliingilia kesi ya ufisadi dhidi ya mwenyekiti wa chama cha ANC Bw. Jacob Zuma, hata hivyo aliamua kujiuzulu kwa ajili ya kulinda mshikamano ndani ya chama cha ANC.

Hatua hiyo inamaanisha kuwa, awamu ya Mbeki imemalizika kabla ya muda uliowekwa na siasa nchini Afrika Kusini itamkumbatia kiongozi mpya.

Rais Thabo Mbeki mwenye umri wa miaka 66 alichaguliwa kuwa rais wa Afrika Kusini mwaka 1999, yeye ni rais wa pili wa Afrika Kusini tangu utawala wa ubaguzi wa rangi ukomeshwe nchini humo. Hivi sasa rais Mbeki ni mwenyekiti wa zamu wa jumuiya ya SADC, nae katika nafasi yake ya msuluhishi, alitoa mchango mkubwa katika kuondoa msukosuko wa kisiasa wa Zimbabwe, ambayo ni nchi jirani ya Afrika Kusini. Katika hali ya kawaida rais Mbeki anatazamiwa kumaliza muda wake wa urais katikati ya mwaka 2009, na kiongozi wa sasa wa chama cha ANC Bw. Jacob Zuma ni mgombea mwenye nguvu zaidi wa kiti cha urais.

Bw. Thabo Mbeki na Bw. Jacob Zuma walikuwa marafiki na wenzi wa zamani, Mbeki alichaguliwa kuwa rais wa Afrika Kusini na Zuma akawa makamu wake mwaka 1999, lakini baadaye walianza kupingana. Wachambuzi wanasema, hali ya mvutano wa kisiasa ilianza kutokea ndani ya chama cha ANC mwaka 2005 wakati rais Mbeki alipomwondoa madarakani Jacob Zuma aliyekuwa makamu wa rais kutokana na kuhusika na kesi ya ufisadi. Mwaka jana baada ya Zuma achaguliwe kuwa mwenyekiti wa chama cha ANC, hali hiyo ilikuwa mbaya zaidi siku hadi siku. Hususan tarehe 12 mwezi huu, mahakama kuu ya Afrika Kusini ilitipilia mbali mashtaka ya ufisadi dhidi ya Zuma, jambo ambalo liliondoa vikwazo vya mwisho vilivyoweza kumzuia Zuma kushiriki kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2009. Baadhi ya watu wanaona rais Mbeki alishirikiana na waendesha mashitaka dhidi ya Jacob Zuma, kwa hiyo watu wengi ndani ya chama cha ANC walitoa malalamiko makubwa dhidi ya rais Mbeki, hali ambayo ilisababisha kujiuzulu kwa Mbeki.

Rais Mbeki mwenyewe hakushangazwa na umauzi huo wa chama wa kumtaka ajiuzulu, kwa sababu dalili zilionekana tangu zamani. Kwa mujibu wa katiba ya Afrika Kusini, rais anapaswa kuteuliwa kwanza na chama tawala cha ANC na baadaye uteuzi huo kupitishwa na bunge, kwa hiyo chama cha ANC kina nguvu kubwa ya ushawishi kuhusu uteuzi wa rais. Mwaka jana Mbeki alishindwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho, hali hii ilionesha kuwa, nafasi yake ya urais ilianza kuyumba. Na baadaye matukio mbalimbali yaliyotokea nchini Afrika Kusini yalithibitisha kuwa rais Mbeki alikuwa akikabiliwa na hali ngumu, kuanzia mwazoni mwa mwaka jana Afrika Kusini ilipokumbwa na upungufu mbaya wa umeme, hadi kutokea kwa matukio ya kimabavu dhidi ya wageni. Rais Mbeki alishindwa kukabiliana vizuri na matukio hayo kutokana na kukosa uungaji mkono wa chama cha ANC, na kushindwa kwake kulisababisha malalamiko makubwa ya wananchi na rais Mbeki mwenyewe akachoka sana. Ndiyo maana katika miezi ya hivi karibuni, rais Mbeki alijikita zaidi kwenye usuluhishi wa msukosuko wa Zimbabwe, na hatimaye makubaliano ya kugawa madaraka yaliyofikiwa kati ya vyama vya kisiasa vya Zimbabwe kama yaliweka alama ya mwisho inayowafurahisha watu kabla ya Mbeki kujitoa kwenye medani ya kisiasa.

Baada ya kujiuzulu kwa rais Mbeki, bunge la Afrika Kusini linakabiliwa na masuala mbalimbali, na suala la kwanza ni jinsi ya kupata rais mpya atakayeziba pengo aliloacha Bw. Mbeki.