Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-23 19:02:12    
Dunia nzima yatakiwa kuchangia maendeleo ya Afrika

cri

Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya maendeleo ya Afrika ulifanyika tarehe 22 huko New York. Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 160, wakiwemo wakuu na viongozi wa serikali zaidi ya 40 walihudhuria mkutano huo. Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Bw. Ban Ki-Moon, alitoa wito kwa nchi mbalimbali duniani, hususan nchi zilizoendelea zitekeleze ahadi ziliyoitoa ya kuongeza misaada kwa bara la Afrika na kuzisaidia nchi mbalimbali za Afrika kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia.

Katika miaka kadhaa iliyopita, nchi nyingi barani Afrika zilipata ongezeko la kasi la uchumi, na kupata maendeleo katika kutimiza malengo ya milenia. Hata hivyo kupanda kwa bei za chakula na mafuta, mabadiliko ya hali ya hewa na migogoro ya kikanda zinazuia ongezeko hilo. Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa inasema, kutokana na hali iliyopo sasa, inaelekea hakuna nchi hata moja barani Afrika ambayo itaweza kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia ifikapo mwaka 2015.

Bw. Ban Ki-Moon akihutubia mkutano huo, alisema mkutano huo unatoa nafasi kwa viongozi wa nchi mbalimbali duniani wawe pamoja na kusisitiza ahadi waliyotoa ya kuipa Afrika misaada ya maendeleo, na kuzingatia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali. Alisema "Tunapaswa kukabiliana na changamoto hizo, pamoja na sababu ya kihali, utulivu na amani ya dunia inajengwa kwa msingi wa ustawi wa nchi zinazoendelea, hayo yamethibitishwa kutokana na mapambano ya kugombania chakula na maliasili yaliyotokea hivi karibuni. Ndiyo maana mambo ya kulinda amani, kupata maendeleo na kuheshimu haki za kimsingi za binadamu yanaambatana."

Bw. Ban Ki-Moon alisema, ili kutimiza malengo ya manedeleo ya milenia kwa mpango uliowekwa, inakadiriwa kuwa nchi za Afrika zinahitaji misaada ya dola za kimarekani bilioni 72 kwa mwaka. Fedha hizo zinaonekana ni nyingi sana, lakini hazijazidi uwezo wa nchi zilizoendelea, pia zinalingana na ahadi iliyotolewa na nchi hizo. Bw. Ban Ki-Moon alisisitiza kuwa, hivi sasa jambo muhimu zaidi linalotakiwa kufanywa na serikali za nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa si kutoa ahadi mpya, bali kutekeleza kwa vitendo ahadi iliyopo, na kuibadilisha kauli mbiu ya kisiasa kuwa matokeo halisi ya kuboreshwa kwa maisha ya watu.

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Yang Jiechi alipohutubia mkutano huo, alisisitiza kuwa, amani na ustawi wa dunia hautatimizwa bila maendeleo ya Afrika. Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuongeza nguvu barani Afrika, kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali za nchi mbalimbali za Afrika na watu wake, na kuisaidia Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia nzima. Bw. Yang Jiechi alisema, China itaendelea kuimarisha mawasiliano na nchi za Afrika, kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa wakuu wa Beijing wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika. Aidha China inachukua hatua halisi za kusaidia maendeleo ya Afrika na kusukuma mbele uhusiano wa kiwenzi wa kimkakati wa aina mpya kati ya China na Afrika.

Bw. Yang Jiechi alisema "Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, tutazidi kuzipatia nchi za Afrika misaada ya maendeleo katika sekta za kilimo, elimu, afya, matibabu na nishati safi."