Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-25 17:10:07    
Kitabu kikubwa cha historia ya China "Rekodi ya Historia"

cri

"Rekodi ya Historia" ni kitabu cha kwanza kabisa cha kueleza historia ya China kwa wasifu. Kitabu hicho kiliandikwa toka mwaka 104 K.K. hadi mwaka 91 K.K. Na mambo yaliyoelezwa ni ya miaka 3,000 tangu enzi na dahari mpaka mfalme Hanwu wa Enzi ya Han ya Magharibi yaani mwaka 91 K.K. Kitabu hicho kiliandikwa kwa mfululizo kuhusu mambo makubwa ya kihistoria katika enzi mbalimbali na huku kilieleza historia ya koo mbalimbali za watu mashuhuri na watu hodari, licha ya hayo pia kilieleza uchumi, mambo ya kijeshi, miradi ya maji, shughuli za matambiko, adabu na muziki katika enzi mbalimbali.

"Rekodi ya Historia" sio tu kitabu kikubwa cha historia na ya fasihi bali pia ni kitabu kinachohusika na falsafa, siasa, uchumi, mambo ya kijeshi, sheria, unajimu na jiografia, ni kitabu chenye elimu mbalimbali kama ensiklopidia.

Mwandishi wa kitabu hicho Sima Qian alizaliwa mwaka 145 K.K. katika ukoo wa ofisa wa mambo ya historia na kufariki mwaka 90 K.K. Alipokuwa na umri wa miaka 34 baba yake Sima Tan alipokuwa mahututi alimwambia akamilishe kitabu cha "Rekodi ya Historia". Tokea hapo Sima Qian alianza kukusanya habari kujiandaa kuandika kitabu hicho. Lakini mambo yanaweza kuzuka bila kutarajiwa, kwamba alipokuwa na umri wa miaka 36 alimkasirisha mfalme Hawu kutokana na kumtetea jemadari mmoja aliyetekwa nyara vitani, akamtia gerezani na kisha akatoa hukumu ya adhabu kali ya kudhalilisha ya "kukatwa uume". Kisa chenyewe ni hivi, kwamba mwaka 99 K.K. Jemadari wa Dola la Han Magharibi Li Ling alichaguliwa na mfalme Hanwu kwenda medani ya vita kupambana na wavamizi wa Xiong Nu kwenye sehemu ya mpaka wa kaskazini. Mwanzoni, habari njema za matokeo ya vita zilikuwa zikimjia mfalme mfululizo ambapo mawaziri wengi walimpongeza mfalme kwa chaguo lake la hekima. Lakini baadaye hali ilikwenda kombo, jemadari huyo na askari wake walivamiwa na maadui kutoka pande zote; ingawa walipigana kufa na kupona kwa siku nane mfululizo lakini mwishowe karibu wote waliuawa, naye jemadari Li Ling akasalimu amri kwa askari wa Xong Nu. Kusikia hayo mfalme alikasirika mno, na mawaziri waliomsifu mfalme kumchagua vizuri jemadari huyo, wote wakaanza kumshutumu jemadari huyo isipokuwa tu Sima Qian ambaye alimtetea jemadari huyo apimwe kwa pande zote, ushupavu wake katika vita, na kushindwa kwake. Kusikia utetezi wake mfalme akaghadhibika vibaya akamtia Sima Qian gerezani papo hapo na akatoa hukumu ya adhabu kali ya kumdhalilisha ya "kukatwa uume". Kutokana na mateso hayo Sima Qian alikufa moyo hata alitaka kujiua. Lakini jukumu aliloagizwa na baba yake lilimtia moyo wa kuendelea na uhai wake. Baadaye mfalme Hanwu alitambua kosa lake akamwachia huru na kumpa cheo kikubwa katika serikali, lakini wakati huo Sima Qian hakuwa tena na hamu ya kushughulika na mambo mengine, aliona kwamba yeye ni mtu mwenye kasoro, na umuhimu pekee katika maisha yake ni kukamilisha kitabu chake cha "Rekodi ya Historia". Sima Qian alitumia miaka 13 kumaliza kitabu chake ambacho kina sura 103 na maneno zaidi ya laki tano.

"Rekodi ya Historia" ni kitabu chenye thamani kubwa, thamani yake sio tu kwa sababu ya maelezo ya historia bali pia ni kwa sababu ya fasihi yake kubwa. Alionesha ustadi mkubwa wa kueleza watu muhimu wa histoira kwa kina. Licha ya kueleza mambo ya watu hao Sima Qian pia alizingatia mazingira ya familia ya watu hao, kiwango cha elimu yao na uzoefu wao wa kijamii na kufanya uchambuzi sababu ya matokeo yaliyowatokea watu hao.

Idhaa ya kiswahili 2008-09-25