Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-09-30 20:00:19    
Barua 0930

cri

Wasikilizaji wapendwa, ni watangazaji wenu Chen na Pili Mwinyi tunawakaribisha katika kipindi hiki cha sanduku la barua Leo kwanza tunawaletea barua tulizotumiwa kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483, Dubari United Arab Emirates ametuletea barua akisema, Ndugu wapendwa, Ni furaha ilioje kusikia kwamba Jamhuri ya Watu wa China imeweka historia hivi karibuni pale mwanaanga Zhai Zhigang aliposhuka katika Chombo Cha Shenzhou No.7 na kutembea kwa dakika 20 katika anga ya juu. Kwa kweli tukio hilo ni la Kihistoria katika shughuli za anga ya juu za Jamhuri ya Watu wa China kunatuthibitishia sisi Walimwengu juu ya ufanisi mkubwa wa sayansi na teknolojia uliokwisha fikiwa na taifa la China.

Yeye binafsi kama msikilizaji wa Redio China Kimataifa wa muda mrefu , ameingiwa na furaha kubwa iliyoje juu ya kukua kwa kiwango cha juu kabisa cha elimu ya kisayansi na kiufundi nchini Jamhuri ya Watu wa China kadri siku zinavyosonga mbele. Bila shaka yo yote mafanikio hayo yanazidi kuisogeza China katika safu ya mbele kabisa ya mataifa yaliyoendelea sana kiufundi na kisayansi hapa duniani na ni matumaini yetu makubwa kwamba mafanikio hayo yataweza pia kuyanufaisha mataifa mengine yanayoinukia.

Tunamshukuru kwa dhati Bw. Mbarouk Msabah kwa barua yake ya pongezi kuhusu China kufanikiwa kurusha chombo cha Shenzhou No.7 kilichobeba wanaanga watatu kwenye safari ya anga ya juu, ambapo mwanaanga mmoja alitoka nje ya chombo na kutembea kwenye anga ya juu. Sisi wachina kweli tunaona fahari na furaha kubwa kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya safari ya anga ya juu, China itaendelea na juhudi zake za kuendeleza teknolojia za chombo kinachobeba binadamu kwenye safari ya anga ya juu, na kutumia nafasi ya anga ya juu kwa amani.

Msikilizaji wetu Xavier Telly Wambwa wa Bongoma Kenya ametuletea barua pepe akisema Pokea salaamu kutoka hapo Bungoma Kenya, ni matumaini yake kwamba sisi sote tu wazima. Yeye pia ni mzima pamoja na familia yake na wasikilizaji wenzake. Ametuambia kuwa amefurahia kupata cheti na zawadi yake pamoja na gazeti la China Today tuliyomtumia, anatushukuru sana. Na hakusahau kumsalimia Bw. Fadhili Mpunji, Mama Chen na wote wa ofisi ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Hapa tunamwambia kuwa, Bw. Fadhili ameondoka Beijing baada ya kukamilisha muda wake wa miaka mitano hapa Idhaa yetu. Labda sasa yuko Uingereza ataendelea na masomo.

Msikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie ambaye barua zake huhifadhiwa na Karie Ndumbi Shule ya msingi ya Muchagara S.L.P 601 Maragua-Kenya ametuletea barua akisema, kwanza salamu zake ziwaendee watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili China Radio Kimataifa.

Anaomba kuchukua fursa hii ili kutoa maoni kuhusu "Ajira ya watoto na madhara yanayotokana na ajira ya watoto". Kama mfanyakazi wa kujitolea kutoa huduma kwa watoto na familia ambazo huwa zinaathiriwa na suala la ajira ya watoto, humo nchini Kenya akiwa wilaya ya Murang'a kusini katika mkoa wa kati.

Kwanza anaelezea ajira ya watoto ni nini na kisha baadaye ataendelea kutaja baadhi ya kazi ambazo hufanywa na watoto na pia jinsi ajira ya watoto inavyopunguza na kuhangaisha maisha ya watoto na pia uwezo wa kuwa na kizazi kizuri cha baadaye cha taifa lao na hata pia dunia nzima.

Ajira ya watoto ni nini? Watoto kufanya kazi ili walipwe. Kufanya kazi ambazo haziambatani na umri wao. Kazi ambazo humfanya mtoto kutopata elimu. Kazi ambazo huathiri tabia, usalama uzima na pia afya ya mtoto. Kazi za kulazimishwa. Hata hivyo kuna tofauti kubwa kati ya ajira ya watoto na baadhi ya kazi ambazo huwa ni za kuelimisha mtoto ambazo kwa kawaida wanapewa na wazazi wao. Baadhi ya kazi ambazo ni hatari kwa watoto wa siku hizi .

Huduma za kinyumbani, vijana kwenda shambani na wasichana kubaki nyumbani. Kuchimba mchanga. Uuzaji wa mihandarati na vileo vilivyo haramishwa. Kuchuma kahawa, majani ya chai. Kushiriki katika kutoa huduma kwa makundi ya waasi na pia jeshi haramu la kivita. Majanga au madhara ambayo huibuka katika harakati za watoto au mtoto kujiingiza kwenye ajira ya watoto ni: Kukosa kujiendeleza kielimu, kiufundi na kitechnolojia?kwani muda mwingi huwa anatumika kazi fulani.

Tabia ya kutumia madawa ya kulevya na pombe haramu. Kuchanganyikiwa na kupoteza mwelekeo katika maisha na pia kukosa tumaini la maisha kwa watoto wetu. Watoto wa chini ya umri wa miaka 18 kupata uja uzito. Kupata magonjwa ya zinaa kama vile ukimwi na mengineyo.

Mambo hayo yote huwa yanapunguza na kuzuia taifa lolote au bara lolote kujiendeleza kiuchumi, kibiashara na pia masikilizano kati ya watu na uchafuzi wa mazingira. Pia huchangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa majanga mengi ambayo yanaikumba dunia nzima.

Baadhi ya mambo ambayo huwafanya watoto kujiingiza kwenye ajira ni: maradhi ya ukimwi ambayo yamefanya watoto wengi kuwa mayatima. Unywaji wa pombe kupindukia. Hii ni kutoka kwa wazazi. Kutahiri mapema kwa vijana ambao huwafanya watoto kufikiri kuwa masomo hayana faida

Matumizi ya madawa ya kulevya. Wazazi kutodhamini masomo. Umasikini?hii imechangia na mabadiliko ya hali ya hewa kwani familia nyingi hufanya kazi ya ukulima huku hali ya hewa ikibadilika na kuwaacha bila tegemeo lolote.

Tumaini lake ni kwamba wafanyakazi wa Redio China kimataifa tutachangia zaidi katika kuwaelimisha na kuwafahamisha wasikilizaji jinsi wanavyoweza kuwahamasisha watoto na wazazi wao kwenye jamii kuhusu elimu, haki za watoto, kuwa na kizazi kizuri cha baadaye, kujitolea kuwa Mawakili wa watoto, na kufanya taifa lao na hata dunia nzima isiwe na ajira ya watoto.

Anamalizia hapo kwa leo huku akiwa na matumaini kwamba suala la "Ajira ya watoto" litatangazwa katika vipindi vya idhaa yao wanayoipenda ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa.

Tunamshukuru Philip Ng'ang'a Kiarie kwa barua yake ambayo imetoa maoni kuhusu "Ajira ya watoto na madhara yanayotokana na ajira ya watoto", ambayo huenda yatawasaidia baadhi ya wasikilizaji wetu. Ni matumani yetu kuwa, wasikilizaji wetu waliopo popote pale barani Afrika wataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo, ama maelezo kuhusu maisha na kazi zenu. Asante sana.