Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-06 14:54:13    
Vyakula vitamu vya Kiislamu katika mtaa wa Niujie mjini Beijing

cri

Vyakula vya Kibeijing viko vya aina nyingi, na miongoni mwa vyakula hivyo, vingi ni vya Kiislamu. Vyakula vya Kiislamu vya aina nyingi vinapikwa kwa nyama ya ng'ombe au mbuzi. Katika mtaa wa Niujie mjini Beijing wanakoishi Waislamu wengi, vyakula vya Kiislamu vinajulikana zaidi.

Katika karne ya 14 Waarabu na Waajemi walihamia kwa sehemu ya mashariki na baadhi yao walifika na kuishi nchini China, na huku walileta mapishi yao ya vyakula vya Kiislamu. Baadaye mapishi yao yalienea hadi mjini Beijing, na vyakula vya Kiislamu vya Kibeijing vilivyochanganywa na mapishi ya jadi ya Kibeijing vikapatikana. Tokea hapo vyakula vya Kiislamu vilienea, mtaa wa Niujie ni sehemu wanayoishi Waislamu wengi na pia ni chanzo cha vyakula vya Kiislamu mjini humu.

Mkahawa wa Jimbini wa Ukoo wa Wei ulio maarufu kote mjini Beijing uko katika mtaa huo. Mkahawa huo si mkubwa, meza ndani yake ni za mtindo wa zamani wa Kibeijing. Bosi wa mkahawa huo Bi. Li Shumin alisema, mkahawa huo umekuwa na historia ya miaka mia moja. Alisema,

"Mkahawa wa Jimbini wa Ukoo wa Wei ulianzishwa mwaka 1888 na kuendelea mpaka mwaka 1954. Mwaka 1988 mkahawa huo ulianza tena biashara yake na uliendeshwa na Bw. Wei Guanglu ambaye alikuwa kizazi cha tatu cha ukoo wa Wei, na sasa mkahawa huo unaendeshwa na Bw. Wei Ning ambaye ni mtu wa kizazi cha nne cha ukoo huo."

Bosi Li Shumin alisema, "mwanzilishi wa mkahawa huo Bw. Wei Hongchen alijifunza namna ya kupika jimbini kutoka kwa rafiki yake aliyekuwa mpishi wa chakula cha mfalme. Jimbini ya Kibeijing ni tofauti na jimbini ya kimagharibi. Jimbini ya Kibeijing inatiwa pombe iliyotengenezwa kwa mchele ndani ya maziwa, kisha maziwa yakaganda kuwa jeli, baadaye yakaokwa na kisha kuwekwa ndani ya friji. Jimbini ya Kibeijing ina ladha tofauti, na lakini inayonunuliwa vizuri zaidi ni jimbini ya aina ya jadi inayouzwa katika mkahawa wa ukoo wa Wei. Watu wengi wanakwenda mkahawa huo kutoka mbali kwa ajili tu kuonja jimbini iliyotengenezwa na mkahawa huo. Kuhusu jinsi jinbini ya mkahawa huo inavyowavutia wateja Bi. Li Shumin alisema,

"Kila siku mabakuli 1000 hivi ya Jinbini ya aina ya jadi yananunuliwa na wateja, wateja ni wengi kiasi ambacho tunashindwa kufunga mkahawa saa tatu za usiku kama tulivyopanga, baadhi ya wakati tulifunga mkahawa mpaka saa tano usiku hata zaidi."

Katika mtaa huo pia kuna mkahawa mmoja ambao ingawa hauna historia ndefu kama mkahawa wa jimbini ya ukoo wa Wei, pia unajulikana sana miongoni mwa wakazi wa Beijing. Mteja mmoja aliyesimama foleni alisema,

"Mara kwa mara nakuja kununua vyakula vya mkahawa huu. Nimezoea vyakula vya hapa."

Mkahawa huo unaitwa Mkahawa wa Ukoo wa Hong, vyakula vyake viko vya aina nyingi. Bosi wa mkahawa huo ni mtu wa kizazi cha pili cha ukoo wa Hong, anaitwa Hong Yuchun, alisema,

"Mwanzoni tulipika vyakula vya aina chache, baadaye aina za vyakula ziliongezeka. Vyakula vyetu vinanunuliwa vizuri kwa sababu tunazingatia zaidi sifa za malighafi na viungo."

Chakula kilicho maarufu zaidi cha mkahawa huo ni chakula cha vipande vidogo vya nyama ya ng'ombe vilivyokaangwa. Watu wengi walikwenda kununua chakula hicho baada ya kuambiwa na wateja wengine waliowahi kuonja. Nyama ya ng'ombe ilikaangwa kwa kiasi cha kufaa, ni laini na ina ladha ya shamari. Mteja mmoja alisema siku moja alinunua nusu kilo ya nyama hiyo na kula pamoja na chapati mbele ya mkahawa, dakika chache tu alimaliza.

Yeyote anayekwenda mtaa wa Niujie lazima atakula chakula cha baodu ambacho ni utumbo wa ng'ombe au mbuzi uliokatwa kwa vipande vyembamba na kuchovywa ndani ya maji ya kuchemka na kula baada ya kutiwa viungo. Chakula hicho cha mkahawa wa ukoo Feng ni maarufu zaidi. Mwaka 1875 mtu wa kwanza aliyetembeza chakula hicho vichochorani mjini Beijing aliitwa Feng Lishan, kadiri muda ulivyopita, chakula hicho kilizidi kujulikana. Hivi sasa anayepika chakula hicho ni mtu wa kizazi cha tano. Watu wengi mashuhuri waliwahi kwenda kwenye mkahawa huo. Bw. Feng Qiusheng ambaye ni wa kizazi cha nne cha ukoo Feng anaona fahari sana alipotaja kwenda kuwapikia chakula hicho mabalozi na viongozi wa mataifa. Alisema,

"Katika sherehe ya kuadhimisha miaka 50 tangu Jamhuri ya Watu wa China izaliwe nilialikwa kwenda Hoteli ya Wageni wa Mataifa ya Diaoyutai kuwapikia chakula cha baodu katika dhifa ya taifa, naona fahari kubwa."

Kama watu wasipokuwa na nafasi za kutosha kutembea mikahawa ya vyakula vya Kiislam katika mtaa wa Niujie mjini Beijing, wanaweza kwenda kwenye "Mji wa Vyakula Vitamu vya Kiislamu" uliopo katika soko la Kiislam. Huko kuna magenge mengi yanayouza vyakula vya kila aina vya Kiislamu. Meneja wa soko hilo Bw. Ping Guodong alisema,

" 'Mji wa Vyakula Vitamu vya Kiislamu' umekusanya karibu vyakula vya Kiislamu vya aina zote vinavyopatikana katika sehemu ya kaskazini ya China. Licha ya wakazi, pia wako Waislamu wengi wa nchi za nje wanakula katika mji huo baada ya kusali kwenye msikiti uliopo mtaani humo."

Idhaa ya kiswahili 2008-10-06